HALMASHAURI ya Msalala
wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imewavua madaraka walimu wakuu 15 wa
shule za msingi wilayani humo, kwa kosa la kuandikisha wanafunzi hewa
883 na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh milioni 3.4.
Akitoa taarifa hiyo kwa
vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege,
alisema hatua hiyo imetekelezwa baada ya kufanya uchunguzi wa kuhakiki
wa wanafunzi hao kwa kipindi cha kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka jana
katika shule za msingi.
Berege alisema katika uhakiki wa kwanza uliofanyika Agosti hadi Oktoba, mwaka jana, ilibainika kuwepo kwa wanafunzi hewa 639.
Aliongeza kuwa katika
uhakiki mwingine uliofanyika Oktoba mwaka huo kwa kushirikiana Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) walibainika
wanafunzi hewa 244.
Alisema kutokana na
tatizo hilo, halmashauri hiyo iliwaita walimu hao wakuu na kuwataka
warudishe fedha hizo na walikubali kuzirudisha fedha katika Ofisi ya
Mkurugenzi kabla ya kuvuliwa madaraka yao rasmi kuanzia Desemba 7, mwaka
huu walipokabidhiwa barua zao.
Mkurugenzi huyo
aliwataja waliovuliwa madaraka na shule kwenye mabano kuwa ni Emmanuel
Nkwabi (Mhama) aliyelipa Sh 56,000 Sita Kasangi (Mwakuzuka) aliyelipa Sh
132,000, Iman Gongo (Nyamigege) amelipa Sh 155,000, Fabian Mchiwa
(Mwanyaguli) Sh 21,000 na Omari Masani (Ngaya) Sh 86,000.
Aliwataja wengine kuwa
ni Vedastus Masonga (Buganzo) Sh 215,5000, Bernard Patroba (Nyamididi)
Sh 142,000, Abbas Kirua (Gulla) aliyelipa Sh 26,000, Elisafi Mshana
(Shishinulu) Sh 456,500, George Mabambi (Mbizi) Sh 68,000 na Hussen Said
(Bukwangu) Sh 56,000.
Wengine ni Anthonia
Peter (Chella) Sh 168,000, Godfrey Niwagira (Buyange) Sh 99,000, Aron
Sizya (Kashishi) Sh 198,400 pamoja na Jovinus Katemi (Nyakadoni)
aliyelipa Sh 99,000.
Kwa upande wake, Ofisa
Elimu Msingi wa Halmashauri ya Msalala, Vivian Masangya, alisema walimu
wakuu wa shule za msingi katika halmashauri yake wanatakiwa kuhakikisha
kila mwezi wanatoa taarifa za wanafunzi.
Aidha, aliwataka wawe makini katika kutoa takwimu mbalimbali za wanafunzi.
Masangya aliongeza kuwa
sasa Serikali inataka kuona watumishi wake wakiwemo walimu wanafanya
kazi kwa kufuata miongozo pamoja na weledi na kuongeza kuwa kwa sasa
serikali hapendi kuona fedha zake zinapotea kirahisi kama ilivyokuwa kwa
walivyofanya walimu hao.
IMEANDIKWA NA RAYMOND MIHAYO,-habarileo KAHAMA