Kwa
mara ya kwanza mshitakiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha
na kujeruhi, Salum Njwete maarufu Scorpion, amekutana na mlalamikaji
katika kesi hiyo, Said Mrisho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
iliposikilizwa jana.
Mrisho,
ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama
hiyo kuwa alichomwa visu tumboni na mgongoni kabla ya kutobolewa macho.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora
Haule, Mrisho alidai kuwa wakati tukio hilo linaendelea, alimkariri
mshitakiwa kwa kumuangalia usoni.
Akielezea
tukio lilivyotokea, alidai Septemba 6, mwaka huu saa nne usiku alikuwa
kazini kwake Tabata Segerea kwa kazi yake ya kinyozi na baada ya kufunga
ofisi, alikwenda kituoni kusubiri usafiri wa kwenda nyumbani kwake
Makuburi, karibu na Ubungo.
Alidai
wakati anasubiri usafiri, ilipita bajaji na kumuuliza anakokwenda,
ambapo alimwambia kwamba anakwenda Ubungo na mwenye bajaji alidai
anakwenda Buguruni, ila anaweza kumsogeza hadi Tabata Relini ili
akapande magari ya Ubungo.
‘’Wakati
nishapanda bajaji na tumeelewana anifikishe Tabata Relini ghafla dereva
huyo aliniomba apite njia ambayo ni fupi kutokezea Buguruni, ambapo
hapo ndiko nitakapochukulia magari ya Ubungo kwani naishi Makuburi,”
alidai Mrisho.
Alidai baada ya kufikishwa Buguruni Kwa Mnyamani, aliona wauza kuku na kusogea kwa ajili ya kununua ili kupeleka nyumbani kwake.
‘’Kulikuwa
kuna wafanyabiashara wengi wa kuku eneo la Buguruni kituo kinaitwa Kwa
Mnyamani kama saa 4:40 usiku ambapo nilinunua kuku mmoja kwa Sh 6, 000,”
alidai.
Akiendelea
kutoa ushahidi, Mrisho alidai wakati anaendelea na manunuzi na kuongea
na muuzaji, aliona mtu amesimama upande wake wa kulia na alianza
kumuita.
‘’
Aliniambia ‘broo’ nina shida. Nami nilimgeukia na kumuuliza una shida
gani kama una shida sema nakusikiliza kama naweza kukusaidia nikusaidie,
lakini mtu huyo hakujibu ambapo niliendelea na manunuzi,’’alidai.
Shahidi
alidai wakati anaendelea na manunuzi alishikwa na hofu, kwani mkono
wake alikuwa amevaa cheni ya silva na mfuko wa suruali, ulikuwa na fedha
iliyokuwa inaonesha kutuna.
‘’Ghafla
nilishtukia ninachomwa visu mkononi na bega la kushoto ambapo
nilipogeuka niliendelea kuchomwa na nikaanza kupiga kelele ya mwizi
lakini sikupata msaada, kwani nilishangazwa kuona watu wananiona lakini
hawanipi msaada,’’alidai na kuongeza:
‘’Yule
mtu alijibu hakuna mtu wa kumsaidia ambapo aliendelea kumchoma visu
vinne tumboni na kuanguka chini wakati huo kuna watu walikuwa wanamwita
Scorpion, kwamba tayari umeshaua huku akiendelea kunikagua
mfukoni,’’alidai.
Alidai
wakati anaendelea kukaguliwa, mshitakiwa alimkanyaga mkono wake na
kumkata cheni ambayo alikuwa amevaa mkononi na shingoni. Pia, alidai
kuwa alivyodondoka chini alidondoka chali kwa hiyo alikuwa na nafasi ya
kumkariri vizuri jinsi alivyo, kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa taa.
Aliiambia
mahakama kuwa, mshitakiwa aliendelea kumkagua mfukoni na kuchukua fedha
zote na kwamba alisikia sauti kuwa, “Salum mwache huyo keshakufa sasa
ukimchukulia na simu ndugu zake watajulishwaje?” Shahidi alidai baadaye
alivuliwa fulana na kumfunga mkononi kisha akamburuza kumpeleka
barabarani huku akiwaambia wenye magari wamgonge.
“Muda
huo nilikuwa sijatobolewa macho ambapo niliwekwa barabarani ili
nigongwe na gari, lakini yalikuwa yananipita nilikaa barabarani kama
nusu saa wakati huo yeye kasimama pembeni. “Baada ya muda alinivuta
pembeni na kunipiga kisu cha jicho la kushoto ambapo nilipoteza fahamu
kwa muda na baadaye nilisikia mtu anadai yeye ni raia mwema anataka
kunisaidia ambapo nilimpa simu na kuanza kuwasiliana na ndugu
zangu,’’alidai.
Shahidi
huyo alidai baada ya muda alisikia gari la polisi limefika na kumchukua
hadi kituoni kwa ajili ya kupewa Fomu Namba Tatu(PF3) kwa ajili ya
matibabu.
Aidha,
alidai kwa kuwa alikuwa anasikia maumivu, alichukuliwa maelezo akiwa
ndani ya gari ambapo baadaye alifikishwa Hospitali ya Amana na kupewa
huduma ya kwanza.
Shahidi
huyo alidai alipofika Amana, alikutana na ndugu zake na baada ya muda
alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alipewa kitabu cha
kusaini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji tumboni.
Pia
alidai baada ya muda, daktari wa macho alimfanyia uchunguzi na kueleza
kuwa macho yametobolewa, ambapo alikaa hospitali kwa siku sita.
Kabla
ya kuanza kutoa ushahidi huo, mshitakiwa ambaye alipandishwa kizimbani
saa 3.35 asubuhi, aliomba mahakama isianze kusikiliza shauri hilo hadi
wakili wake wa utetezi afike.
Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo, ambapo baada ya dakika 15 kupita wakili alifika na kuanza na usikilizwaji.
Kwa
mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu wa karate,
alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni Sheli
wilayani Ilala.
Ilidaiwa
mshitakiwa aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Sh 60,000,
kibangili cha mkononi na Sh 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani
ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.
Ilidaiwa
kabla ya wizi huo, alimchoma na kisu tumboni mgongoni na machoni. Kesi
hiyo itaendelea na ushahidi Desemba 28, mwaka huu na mshitakiwa
alirudishwa rumande.