test

Ijumaa, 18 Novemba 2016

Wakuu 7 wa Mikoa Hatarini Kutumbuliwa kwa Kushindwa Kutekeleza Agizo la Rais Magufuli


Wakuu wa mikoa saba wako hatarini kutumbuliwa kutokana na kushindwa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kumaliza tatizo la madawati katika mikoa yao. 
Akizungumza jana alipokuwa akipokea madawati 3,500 yenye thamani ya milioni  300  kutoka benki ya NMB, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene alisema mikoa ya wakuu hao saba inaoongoza kwa upungufu wa madawati. 
Aliwataja kuwa ni wa Geita, Mwanza, Kigoma, Mara, Rukwa, Simiyu na Dodoma. 

Simbachawene alisema kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi hiyo ametoa siku 43 na wasipotekeleza watakuwa wameshindwa kwenda na kasi ya Dk Magufuli. 
Wakuu wa mikoa hiyo ni John Mongella (Mwanza), Brigedia Jenerali Emanuel Maganga (Kigoma), Dk Charles Mlingwa (Mara), Zelothe Steven (Rukwa), Anthony Mataka (Simiyu), Jordan Rugimbana (Dodoma) na Ezekiel Kyunga (Geita).

“Hii mikoa ambayo haijatekeleza agizo la Rais John Magufuli kumaliza tatizo la madawati,ninawaomba hadi kufikia Januari 2017 wawe wameshatekeleza, wasipofanya hivyo watakuwa wameshindwa kasi yetu,” alisema Simbachawene.
Alisema Mkoa wa Geita unaongoza kwa upungufu wa madawati 68,306 ya shule ya msingi na 15,669 ya sekondari, Mwanza kuna upungufu wa madawati 41,438 ya shule za msingi, Kigoma 31,171 ya shule za msingi na Mara kuna upungufu wa madawati 15,843 shule za msingi na 1,135 shule za sekondari. 
Rukwa ina upungufu wa madawati 9,634 ya shule za msingi na 1,340 shule za sekondari, Simiyu ina upungufu 10,209 shule za msingi na 647 ya shule za sekondari na Dodoma ina upungufu 10,592 shule za msingi na 4,281 shule za sekondari. 
Simbachawene aliitaja mikoa iliyomaliza tatizo la madawati kuwa ni Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Manyara, Njombe, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.

“Mikoa ambayo sijaitaja wamebakiza kidogo utekelezaji wa madawati, naamini watakamilisha hivyo naishukuru Benki ya NMB kwa kutuunga mkono kuchangia madawati,” alisema Simbachawene. 

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema walitenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kununulia madawati. 
Alisema mwaka huu wamenunua madawati 10,000 yenye thamani ya Sh900 milioni. 

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx