Mwanamke
mkazi wa Unga-Limited jijini Arusha , Lightness Kivuyo ameripotiwa kufa
wakati akifanyiwa maombi nyumbani kwa mchungaji aliyejulikana kama
‘Nabii Rajabu’ eneo la Kwa-Mrombo pia jijini hapa.
Kwa
mujibu wa dada wa marehemu, Juliana Kivuyo, Lightness alikuwa
amesindikizwa nyumbani kwa nabii huyo nyakati za usiku na mumewe
aliyemtambulisha kama Shafii Mohammed na kwamba wakati akifanyiwa ibada
ya maombi, alianguka na kufariki miguuni mwa ‘Mtume,’ huyo.
“Baadaye shemeji alikuja nyumbani akihema, huku anadai kuwa dada alikuwa kwenye hali mbaya kule kwenye maombi,” alisema
Juliana na kuongeza kuwa alitoka mbio kwenda Kwa-Mrombo nyumbani kwa
Nabii Rajab na kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi, akiwa bila nguo
isipokuwa tu khanga alizofunikwa nazo.
Nabii huyo pia anadaiwa kumnyoa nywele zote pamoja na nyusi za macho wakati akimfanyia ‘huduma,’ hiyo.
Polisi
jijini hapa wamethibitisha tukio hilo wakiongeza kuwa tayari watu
wawili wamekamatwa kutokana na kifo hicho cha ‘maombi tatanishi.’
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo ameongeza kuwa atatoa taarifa kamili mara baada ya kikao chake na Mkuu wa Mkoa.
Mganga
Mkuu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Jacqueline Uriwo
amekiri kupokea mwili wa marehemu, lakini akasema, “Kwanza
walijaribu kutudanganya kuwa huyo mama alikuwa hai na kwamba aliletwa
kwa ajili ya matibabu, lakini tukagundua kuwa walichokileta ni mwili
mfu, hivyo tukampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti!.”
Mkurugenzi
wa Huduma ya Mazishi katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Francis Coster
alisema mwili ulipelekwa hapo na mume wa marehemu ambaye alisisitiza
kuwa mkewe hajafa, bali kazimia tu na kwamba mara nyingi huzimia kwa saa
nyingi.
Dk
Coster aliongeza kuwa ilibidi na wao wasiweke mwili kwenye jokofu na
kuulaza kwenye machela kwa saa sita na ndipo wakaamua kuuweka kwenye
droo za maiti, kwani ilikuwa wazi sasa kwamba asingeamka tena asilani.
Waganga
hospitalini hapo wamekiri kuwa mwili wa marehemu uliletwa hospitalini
hapo ukiwa umenyolewa upara, lakini ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe
hususan maeneo ya mikono na kifua.
Baba
mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo ambaye ndiye mlezi wa Lightness,
alisema mume wa marehemu alimtaarifu juu ya kifo hicho na kuongeza; “Lakini
baadaye nikaletewa taarifa nyingine kuwa Lightness kumbe alikufa wakati
akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa mtu anayeitwa ‘Nabii
Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao walikuja kumkamata
mumewe pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri.”