Jeshi
la Polisi nchini, katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao
unaimarika, limeendelea na operesheni za kukamata wahalifu wa makosa
mbalimbali yakiwemo makosa ya usalama barabarani katika mikoa yote ili
kudhibiti vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Katika
operesheni hizo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha na katika
baadhi ya mikoa, wananchi wameweza kusalimisha silaha kwa hiari katika
vituo vya Polisi.
Operesheni
hizi ni endelevu, na ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kudhibiti
uhalifu na wahalifu hususani katika kipindi hiki tunapoelekea mwisho wa
mwaka, wananchi wanatakiwa kuwa makini na kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu haraka kwa kutumia namba za bure 111 na 112 pindi wanapowatilia
shaka watu wasiowajua katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze
kuchukuliwa.
Kwa
wamiliki wa maduka makubwa, hoteli na maduka ya kufanyia miamala ya
fedha kwa njia ya simu waangalie namna ya kuweka vifaa maalumu vyenye
uwezo wa kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka ama kufuata
huduma katika maeneo yao ya biashara.
Pia,
wananchi katika makazi yao waimarishe ulinzi kwa kutumia mpango wa
ulinzi jirani kwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kubadilishana
taarifa za hali ya usalama ili kuhakikisha mitaa yao inakuwa salama
wakati wote.
Aidha,
Jeshi la Polisi nchini linawataka madereva wa vyombo vya moto kuheshimu
na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuokoa
maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Jeshi
la polisi nchini, litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
sheria, bila woga ama upendeleo katika kuhakikisha usalama wa raia na
mali zao unaimarika.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba - Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.