Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa
Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu tarehe 28 Novemba, 2016
wamekubaliana kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuboresha utendaji
kazi wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA ili miradi hiyo
miwili ilete manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi Tanzania na Zambia.
Marais
hao wametangaza kuchukua hatua hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi baada viongozi hao
kufanya mazungumzo rasmi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 3 ya Rais
Lungu iliyoanza jana hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli.
Katika
mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio,
tevisheni na mitandao ya kijamii Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa
kwake na kuzorota kwa utendaji kazi wa reli ya TAZARA ambao umeshuka
kutoka usafirishaji wa tani 5,000,000 za mizigo mwaka 1976 hadi kufikia
usafirishaji wa tani 128,000 kwa mwaka hivi sasa, huku utendaji kazi wa
bomba la mafuta la TAZAMA nao ukiporomoka kutoka uwezo wake wa
kusafirisha tani 1,100,000 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa mwaka
hivi sasa.
Marais
hao wamekubaliana kuwakutanisha wanasheria wakuu wa Serikali za nchi
zote mbili haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya marekebisho ya
kisheria kwa maeneo yote yaliyoonesha kuwa kikwazo na pia kupanga upya
menejimenti za TAZARA na TAZAMA ili ziweze kuendesha vyombo hivyo
kibiashara na kwa manufaa yaliyokusudiwa wakati vilipoanzishwa na
Waasisi wa mataifa haya mawili yaani Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere wa Tanzania na Mhe. Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia.
“Tumekubaliana
ni lazima tubadilike na tubadilike kwa haraka, vikwazo vinavyotokana na
sheria viondolewe na manejimenti ya TAZARA ipangwe upya, na mimi nataka
kusema kwa uwazi, ukiwauliza TAZARA watakwambia tatizo ni mtaji lakini
ukweli ni kwamba tatizo ni menejimenti, ingekuwa tatizo ni mtaji, ule
uliokuwepo mwaka 1976 umekwenda wapi? maana sasa hivi TAZARA ina vichwa
14 tu vya kuendeshea treni na ina upungufu mkubwa wa mabehewa” amesema
Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Rais Lungu amesisitiza kuwa katika kuimarisha TAZARA
wamekubaliana kuweka pembeni siasa na kuirejesha TAZARA katika hali yake
ya kibiashara kwa kuhakikisha inafanya kazi ya kupunguza gharama za
usafirishaji wa mizigo iendayo kusini mwa Tanzania na nchini Zambia.
Mhe.
Lungu ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA,
Zambia inatarajia kunufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kiasi kikubwa
nchini Tanzania na pia inajipanga kutumia vizuri fursa ya kufunguka kwa
ukanda wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Corridor) na mpango wa ujenzi wa
reli ya kati ambapo ukanda wa Kaskazini mwa Zambia una mawasiliano ya
karibu na bonde la ziwa Tanganyika.
“Mhe.
Rais Magufuli una muda wa kutosha katika uongozi wako na mimi nina muda
wa kutosha pia, kwa hiyo kwa pamoja tunaweza kuimarisha maeneo yote ya
kuinua biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili ikiwemo kuimarisha
TAZARA na TAZAMA kwa manufaa ya wananchi wetu” amesisitiza Rais Lungu.
Kuhusu
hali ya biashara kati ya Tanzania na Zambia, Rais Magufuli amesema
Zambia ni nchi inayoongoza kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya
Dar es Salaam ambapo katika mwaka 2015 mizigo yenye uzito wa tani
Milioni 1.9 ilipitishwa na kwamba kumekuwa na ongezeko la biashara kati
ya Zambia na Tanzania kutoka Shilingi Bilioni 89.2 mwaka 2010 hadi
kufikia Shilingi Bilioni 152.2 mwaka 2015.
Dkt.
Magufuli amemhakikishia Rais Lungu kuwa Tanzania inaendelea kuboresha
mazingira ya kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi
bandari ya Dar es Salaam, kupunguza vizuizi vya barabarani kutoka 8 hadi
4, kushughulikia tatizo la vizuizi vya polisi na kujenga Kituo cha
Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post)
“Tunataka
mambo haya yote yaende haraka, wataalamu wetu ni lazima waharakishe
kurekebisha vikwazo vyote vilivyokuwa vinatuchelewa, tufanye kazi pamoja
kwa manufaa ya wananchi” amesisitiza Rais Magufuli.
Jioni
ya leo Rais Edgar Chagwa Lungu anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa
aliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar
es Salaam na kesho Rais Lungu anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku 3
hapa nchini.