Chadema
imetangaza kuwa Januari itaanza kutumia kadi mpya za uanachama za
kielektroniki, zitakazoiwezesha kukusanya Sh13.9 bilioni kwa mwaka na
kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.
Mkakati
huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe wakati
wa mkutano wa ndani uliofanyika mkoani Morogoro. Tofauti na Mbowe,
viongozi wengine wa chama hicho walioko mikaoni ni Edward Lowassa
aliyeko Dodoma na Frederick Sumaye ambaye yupo Singida.
Mbowe
alisema mfumo huo utasaidia pia kudhibiti baadhi ya viongozi wasio
waaminifu, wanaotumia mwanya wa kuuza kadi na kushindwa kuwasilisha
fedha kwenye hazina ya chama.
Alisema
kwa mfumo huo mpya, kama Chadema itakuwa na wastani wa wanachama
100,000 katika wilaya moja na kila mmoja kulipa ada ya Sh1,000 kwa
mwaka, maana yake itaingiza Sh100 milioni.
Kwa
hoja hiyo ya Mbowe, ikiwa chama hicho kitakuwa na wastani wa wanachama
100,000 katika kila wilaya za Tanzania Bara ambazo ni 139, Chadema
itakuwa na uwezo wa kukusanya Sh13.9 bilioni kila mwaka.
Vyama
vya siasa vinapata ruzuku kwa mujibu wa sheria na ripoti ya ukaguzi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha kuwa
jumla ya Sh67.7 bilioni zililipwa na Serikali kwa vyama vya siasa katika
mwaka kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka wa fedha 2009/2010 mpaka
2012/2013. Fedha ambazo kwa mujibu wa CAG zilikuwa hazijakaguliwa
kisheria.
Ikilinganishwa na mkakati mpya wa Chadema, fedha hizo ni ndogo katika kuhudumia shughuli za chama nchi nzima.
Mbowe
alisema Chadema imeamua kuhakiki wanachama wake ili ifikapo Januari iwe
tayari imemaliza kazi hiyo na kuingia rasmi katika mfumo mpya,
utakaokisaidia kuondokana na dhana ya utegemezi wa ruzuku kutoka
serikalini.
Alisema
ili chama kipige hatua na kuondokana na utegemezi wa ruzuku serikalini,
wamekusudia kuingia katika mfumo wa kupata mapato kutoka ndani ya
wanachama kupitia ulipaji wa ada.
Mbowe
alizungumza na wanachama hao kutoka ngazi za vitongoji, vijiji, kata na
wilaya waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wenye lengo la kuwakumbusha
mambo mbalimbali ya kuimarisha chama hicho baada ya Serikali ya Rais
Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara.
“Katika
kipindi cha miaka miwili ijayo, Chadema itakuwa tayari imefanya
utambuzi wa wanachama wake kwa kuwatambua katika kila mtaa, kitongoji,
kijiji, kata na jimbo kupitia mfumo mpya wa kadi za eleketroniki ifikapo
Januari 2017,” alisema Mbowe.
Alisema
katika baadhi ya maeneo ya mikoa hapa nchini, kadi za uanachama za
Chadema ni lulu na zimekuwa zikiuzwa hadi Sh5,000 badala ya 500.
Alieleza
kuwa mapato ya chama lazima yatokane na ada za wanachama na siyo ruzuku
ya Serikali, kwa kuwa utegemezi wa ruzuku ni hatari kwa uhai wake.
“Hii ruzuku inayotolewa na Serikali inatolewa kwa sababu ya CCM na CCM bila ruzuku hakiwezi kujiendesha,” alidai.
Mbowe
alisema kila jimbo linapata fedha za ruzuku kulingana na idadi ya kura
ilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, akitolea mfano
Jimbo la Mlimba kuwa Mbunge Suzan Kiwanga alishinda kwa kura 40,000
wakati urais Chadema ilipata kura 38,000 huku katika udiwani wakipata
kata tisa kati 16.
“Kutokana
na ruzuku, Mlimba itapata Sh163,688 kila mwezi. Unaweza kuona fedha za
ruzuku kutoka ndani ya chama ni ndogo sana ambapo Mkoa wa Morogoro
unapokea kiasi cha Sh2.2 milioni kila mwezi.
“Kufikia
mwaka 2017 kupitia programu ya Chadema msingi, tumekusudia kukijikita
zaidi kusaka wanachama kutoka ngazi ya mitaa, vitongoji na balozi na
tutaanza uchaguzi ndani ya chama.
“Tumebaini
kuwa baadhi ya maeneo Chadema tumeshindwa kupata wenyeviti wa Serikali
ya vitongoji na vijiji, kukosa madiwani na wabunge kutokana na kukosa
misingi imara wa wanachama,” alisema Mbowe.