Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo jana alisema: “Siwezi
kusema Rais amekataa kuonana nasi, hapana. Labda ni kwa lile tulilokuwa
tuende kumuona nalo (Ukuta) lakini kwa mazungumzo mengine milango ya
Rais iko wazi,” alisema.
Wazo
la viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kutaka kuonana na Rais
lilibuniwa Agosti ili kuzuia maafa ambayo yangejitokeza baada ya Chadema
kutangaza kufanya maandamano waliyoyapa jina la Ukuta, Septemba Mosi.
Hata
hivyo, Dk Shoo alielekeza atafutwe Katibu wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Mchungaji Dk Leonard Mtaita kwa maelezo zaidi akisema ni
mmoja wa wanaoratibu suala hilo.
Dk
Mtaita alipotafutwa kwa mara ya kwanza Septemba azungumzie kama barua
waliyopeleka kwa Rais imejibiwa alisema tetemeko la ardhi lililotokea
mkoani Kagera na kusababisha maafa makubwa litachelewesha mpango wao wa
kukutana na Rais.
Hata
hivyo alipotafutwa tena jana, Dk Mtaita aliomba atafutwe mwenyekiti
mwenza wa kikao kilichoibuka na wazo hilo ambaye ni Sheikh wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim.
“Tumewaachia
wenzetu walioko Dar es Salaam, Sheikh Salim ndiye mwenyekiti mwenza na
yeye yuko Dar na ndiye alijitolea kufanya mawasiliano na Mheshimiwa
Rais,” alisema Dk Mtaita.
Sheikh Salim alipotafutwa ili aeleze alipofikia kufanikisha kuonana na Rais alijibu kwa kifupi tu: “Sisi tuko katika kusubiri. Barua tulishatuma kwa Mheshimiwa Rais. Tunasubiri tu”.
Msemaji
wa Serikali, Hassan Abass alipoulizwa alitaka atafutwe Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa kuwa ndiye msemaji wa
Rais.
“Mtafute Msigwa maana yeye yupo karibu na Mheshimiwa (Rais Magufuli) na anajua ratiba zote,” alieleza.
Alipotafutwa,
Msigwa aliwataka viongozi hao kuendelea kusubiri kwa kuwa kila kitu
kina utaratibu wake na pia inategemea ratiba ya Rais.
“Kama wameandika, wasubiri watajibiwa,” alisema Msigwa.
Viongozi
wa Chadema wanaposoma Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa wanaona wana
haki ya kufanya mikutano ya ndani na hadhara na maandamano mradi tu
Jeshi la Polisi litaarifiwe siku na mahali pa shughuli hiyo.
Rais
Magufuli alipiga marufuku siasa za ushindani hadi mwaka 2020 jambo
ambalo Chadema waliamua kujitokeza kupinga kwa maandamano.
Mbali ya Rais Magufuli, Jeshi la Polisi lilitangaza kuwa ni marufuku kufanya mikutano na maandamano.
Hali
hiyo iliyotishia kuwepo makabiliano yenye maafa ndiyo iliyowaibua
viongozi wa dini ambao walichukua hatua kwanza kuwasihi viongozi wa
Chadema na pili kuwataka wasubiri mrejesho.