test

Jumanne, 22 Novemba 2016

BILIONEA MENGI MMILIKI WA IPP AFUNGUKA HAYA KUHUSU UTAWALA WA MWAKA 1 WA RAIS MAGUFULI SOMA HAPA LIVE!!


“Kabla sijazungumzia au kutoa tathmini ya mwaka mmoja wa utawala wa Rais John Pombe Joseph Magufuli, ningependa kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa kiongozi kama huyu ili atuongoze Watanzania. Nachukua fursa hii kumuombea maisha marefu na afya njema.


“Mimi ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania yaani Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ambayo iliasisiwa Novemba 4, 1998. Mpaka hivi sasa Taasisi hii ina wanachama wapatao milioni 5, wanaotoka katika asasi 173, na mashirika yapatayo108.

Tathmini ya mwaka mmoja wa Dk. Magufuli
“Kwa ujumla mwaka wa kwanza wa Uongozi wa Mh. Rais Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano umekuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa. Mifano ya mafanikio haya makubwa iko mingi, lakini miongoni mwa ile inayonigusa zaidi ni suala la usimamizi wa nidhamu, uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma na sekta za umma kwa ujumla.

“Pia tumeshuhudia uwapo wa serikali inayowajibika ipasavyo katika kusimamia wajibu wake kwa kuwatumikia wananchi hususan wananchi wa kawaida. Serikali imetoa matumaini makubwa katika kipindi hicho kwa kuonyesha kwamba ipo kwa ajili ya Watanzania wote na siyo kundi fulani la watu wachache wenye maslahi binafsi.

“Ni ukweli ulio dhahiri kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja Mh. Rais Magufuli ameweza kurudisha nidhamu, uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma na pia kuwakumbusha watumishi wa umma kwamba wao sio watawala, bali ni watumishi wa wananchi.

“Sisi wafanyabiashara ambao kazi zetu zinategemea watumishi wa umma kupata vibali na kulipa tozo mbalimbali, tumeshuhudia ufanisi na mabadiliko chanya ya mawasiliano baina yetu na wenzetu wa kutoka sekta za umma. Kwa mfano kasi ya kufanya uamuzi na kuchukua hatua stahiki kwa wakati imeongezeka na kuipa serikali taswira chanya mbele ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Tumeshuhudia urasimu ukipungua kwa kasi sana serikalini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na hali hii itaendelea kuvutia uwekezaji ambao unahitaji maamuzi sahihi na haraka pamoja ikiwa na utekelezaji. “Huko nyuma ilifika wakati watu wakadhani serikali iko likizo au haipo kabisa, hali iliyosababisha shughuli za serikali kuendeshwa kiholela.

Lakini sasa katika kipindi cha mwaka mmoja chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Magufuli tumeweza kusikia na kuhisi uwepo wa serikali tena iliyo makini na madhubuti katika kuhakikisha inawatumikia Watanzania wote kwa uadilifu mkubwa na kuwawajibisha wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.

“Tofauti na awamu zilizopita, ambapo watumishi walikuwa wakikiuka miiko ya utumishi wa umma, lakini hawachukuliwi hatua za dhati, awamu hii tumeshuhudia hatua zikichukuliwa mara moja chini ya kauli mbiu ya ‘utumbuaji majipu.

‘’ Huko nyuma kulikuwa na kuundwa kwa tume kila mara eti kuchunguza waliokiuka au wanaotuhumiwa maadili, na ripoti za uchunguzi zilipokamilika, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa. Leo hii mtu akiharibu, hakuna cha kuunda tume, anatumbuliwa na uchukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Mafanikio yote haya yamepatikana katika mwaka mmoja tu wa serikali ya awamu ya tano. Na lazima tukubali kwamba huu ni mwanzo mzuri. “Kwa maoni yangu, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli imeonesha utashi mkubwa wa kisiasa katika harakati za kuboresha mazingira na fursa za biashara kwa sekta binafsi za wazalendo.

“Utashi huo umedhihirishwa pale Mh. Rais Magufuli alipokutana na wafanyabiashara mbalimbali tarehe 3 Desemba, 2015 muda mfupi baada ya kuapishwa na kuweka bayana msimamo wa serikali yake wa kushirikiana na wafanyabiashara’’.

“Sekta binafsi lazima ishiriki kikamilifu katika uanzishwaji na undelezaji wa viwanda nchini hasa viwanda vya kuifanya Tanzania iweze kusindika na kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani, kinyume na hali ilivyokuwa huko nyuma ambako tumekuwa tukiuza mali ghafi nje kwa muda mrefu.

“Mkazo mkubwa lazima uwe katika ujenzi wa viwanda vya kusindika bidhaa zinazotokana na kilimo na ufugaji na uongezaji thamani ya bidhaa zetu kwa kuzingatia kuwa kwa muda mrefu, nchi yetu imekuwa ikizalisha na kuuza nje bidhaa ghafi jambo ambalo limekuwa linakosesha nchi yetu mapato makubwa.

Upigaji vita rushwa nchini
“Rushwa imekuwa ni tatizo sugu hapa nchini, Afrika na kwingineko duniani. Imekuwa ni desturi kwa watawala kuahidi kwamba watapambana na kutokomeza rushwa na ufisadi wakati wakiwa kwenye kampeni za uchaguzi, lakini wakishaingia madarakani hakuna mafanikio yoyote ya maana katika kutokomeza janga hili.

“Lazima tutambue kwamba mapambano yoyote dhidi ya rushwa na ufisadi yanahitaji mambo mawili ya msingi:-

“La kwanza ni utashi wa kisiasa na jambo la pili, ni uongozi ambao unaongoza mapambano hayo kubadilika kifikra na kimtazamo kwa kutambua kwamba rushwa na ufisadi ni vitendo viovu vinavyoweza kutokomezwa na watu wenye dhamira ya ukweli.

“Mheshimiwa Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya ukweli kwa vitendo na ushupavu mkubwa kwamba yuko tayari kupambana na ulaji rushwa uliokithiri na kutamalaki nchini kwa miaka mingi. Kwa kipindi cha mwaka mmoja amefanya maamuzi magumu katika kukabiliana na rushwa na ufisadi nchini.

“Sote tutakumbuka nchi ilipofikia ambapo rushwa na ufisadi vilikithiri na kujijengea himaya na mtandao mpana ambao ulikuwa tishio kwa ustawi wa nchi yetu.

“Mwaka huu wa kwanza wa Rais Magufuli ni mwaka muhimu katika historia ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi, kwani umeweka misingi na hatua madhubuti inayolenga kutokomeza tatizo hili.

“Kauli zake zinazoambatana na vitendo vya kijasiri dhidi ya rushwa na ufisadi ni ushahidi tosha kwamba yeye na serikali yake hawana mzaha katika kutokomeza uovu huu. Mfano mzuri ni jinsi alivyoshughulikia watumishi wa umma ambao wamehusishwa na rushwa, au ufisadi ambapo tumeshuhudia kutenguliwa nyadhifa zao na kuwafikisha mbele ya sheria.

“Pia Mheshimiwa Rais ametekeleza ahadi yake ya wakati wa kampeni kwa kuanzisha Mahakama Maalumu ya kusikiliza na kuamua kesi za rushwa na ufisadi kwa haraka zaidi ili haki ipate kutendeka.

“Binafsi sikubaliani na maoni ya baadhi ya watu kwamba serikali ya awamu ya tano inawaminya wafanyabiashara. Tulicho kishuhudia ni serikali ya Awamu ya Tano kusimamia kikamilifu na kwa dhati ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Ni wazi kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli amevalia njuga suala la ulipaji kodi kwa kila mfanyabiashara na Watanzania kwa ujumla. Katika kusimamia hili, baadhi ya watu huenda wamefikia hatua ya kutafsiri hali hiyo kama ni kuminya wafanyabiashara.

“Kwa mfano, mtu ambaye biashara yake ilikuwa inategemea kutumia rushwa ili kutoa mizigo bandarini bila kulipa kodi lazima alalamike.

“Lakini mfanyabiashara aliyekuwa anaendesha biashara yake kihalali bila kutegemea rushwa, au kukwepa kodi hana sababu ya kulalamika, na wala hutamsikia akilalamika katika mazingira ya sasa ambayo yanatutaka wote tulipe kodi stahiki. Hakuna nchi iliyoendelea duniani ambayo watu wake wanakwepa au hawataki kulipa kodi.

“Aidha tumeshuhudia pia serikali ya Awamu ya Tano ikibana matumizi kwa kupunguza matumizi kama vile kudhibiti safari za ndani na nje ya nchi kwa watumishi wa umma na hata viongozi wakuu wa kisiasa.

“Mwisho kabisa, natoa wito wangu kwa Watanzania wenzangu kwamba, tumwamini Rais wetu, kwani ana nia njema ya kutupeleka mahali pazuri katika maendeleo ya nchi yetu. Hivyo hatuna budi kumpa nafasi atekeleze kwa uhuru yale aliyo ahidi kuwafanyia Watanzania wakati wa kampeni katika kipindi cha miaka mitano.

“Nawaomba Watanzania tumuombee ili aendelee kuongoza nchi kwa misingi ya haki na uadilifu mkubwa na pia tuwe waungwana, pale Mheshimiwa Rais anapotenda mema, tuyatambue na kumpongeza''.

“Kauli ya Rais ya “Hapa Kazi Tu” tuitafsiri kwa vitendo yaani tufanye kazi kweli kweli.”

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx