Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamadi Massauni akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika mkutano watano wa Bunge la 11 linaloebdelea Mjini Dodoma Novemba 7, 2016.Jumla ya askari 152 wamefukuzwa kazi mwaka huu na Jeshi la Polisi kwa sababu ya kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni ya Jeshi hilo kama zilivyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Polisi (PGO) namba 103.
Idadi ya askari hao waliofukuzwa kazi imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Msabaha aliyehitaji kufahamu juu ya idadi ya askari waliochukuliwa hatua kwa sababu ya utovu wa nidhamu.
Mhandisi Masauni amesema kuwa kazi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama ni kulinda raia, mali zao pamoja na mipaka ya nchi lakini kuna baadhi ya askari hao wanakwenda kinyume na Sheria kwa kuwapiga wananchi na kuwasababishia ulemavu pamoja na vifo hivyo Jeshi hilo limewachukulia hatua za kinidhamu.
“Jeshi la Polisi hufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo lakini kuna baadhi ya askari wamekuwa wakikiuka maadili na mwenendo mwema wa Jeshi letu hivyo kuanzia Januari 2015 hadi Juni 2016 tuliwachukulia hatua za kinidhamu askari 200”, alisema Mhandisi Masauni.
Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa baada ya askari hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, walifanyiwa uchunguzi wa kina na jumla ya askari 152 kati ya 200 walikutwa na hatia hivyo hatua iliyofata ni kuwafukuza kazi.
Akizungumzia kuhusu mpango wa Serikali juu ya kujenga nyumba za askari Polisi, Mhandisi Masauni amesema kuwa wanatambua tatizo la makazi ya Askari Polisi katika maeneo mbalimbali nchini hususani kwenye mikoa mipya hivyo Serikali ina nia ya kutatua tatizo hilo kwa kuanza ujenzi wa nyumba kwa ajili ya askari hao.
“Serikali imedhamiria kupunguza tatizo la upu
ngufu wa makazi ya askari polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima ambao utaanza kutekelezwa baada ya taratibu za mkopo wa kuwezesha ujenzi huu kukamilika”, aliongeza Mhandisi Masauni.