WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni
722.7 kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo
Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa
Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya
600.
Amesema
sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015
hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016,
takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni
2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao
yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi
trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15
uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni
9.29,” ameongeza.
Waziri
Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote
wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa
mara moja na wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe
mahakamani na yeye apewe taarifa.
“Kumekuwepo
na changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa
wakati hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia
muda wa kustaafu. Suala hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa
waajiri wote nchini waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa
wakati,” amesisitiza.
Mbali
ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za
shirika hilo na wapangaji wote wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na
wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa wafikishwe mahakamani.
“Nimeambiwa
pia lipo tatizo la wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala
hili lilitolewa maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na wenye Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua
nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini
hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF
ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”
Akizungumzia
utendaji wa shirika hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika
hilo na Bodi ya Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji
wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa
ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika
mfuko wa NSSF.
“Nimefurahishwa
na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari
nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga
Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda
hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,”
amesema.
Mapema,
akielezea utendaji wa shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof.
Godius Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh.
80,000 hadi sh. 100,000 kwa mwezi.
Alisema
limeanza kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi
Dodoma ili kuendana na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado
unaendelea lakini tumeshabaini kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200
hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.
Kuhusu
uwekezaji kwenye ujenzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo
Kigamboni, Dar es Salaam, Prof. Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa
kwa sababu makusanyo ya tozo kwa watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna
uhakika kwamba fedha tulizowekeza zitarudi,” amesisitiza.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 45 za saruji ambazo ni sawa
na mifuko 900 yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa ajili ya waathirika
wa tetememo la ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada huo kutoka kwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe.
Akiwasilisha
msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani
Kagera na wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali
kukabiliana na maafa hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya
madawati 6,000 yenye thamani ya sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali.
Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa.