Bodi hiyo imeruhusiwa kufungua kesi hiyo ndani ya siku 14, huku ikieleza kuwa imejipanga kuwasilisha kesi hiyo chini ya hati ya dharula ndani ya siku 7.
CUF imekuwa ikimshutumu Jaji Mutungi kwa kuingilia mambo ya ndani ya chama hicho kinyume na sheria, ikiwemo kutoa waraka wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba, aliyefukuzwa na chama hicho kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.
Jaji Ama Isario Munisi, ametoa uamuzi wa kukubaliana na maombi ya CUF na kusema mahakama hiyo imejiridhisha kwamba maombi hayo yalikuwa na hati ya kiapo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa.
Katika shauri hilo upande wa CUF unawakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na Juma Nassoro ambaye baada ya uamuzi wa Jaji Munisy, amewaeleza wanahabari kuwa watahakikisha ndani ya siku 7 wanafungua kesi hiyo chini ya hati ya dharula ili ianze kusikilizwa kwa haraka.
Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, amesema, wanatoa onyo kwa Jaji Mutungi kujihusisha na harakati za chama hicho kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa inavyosema.
“Tumesikitishwa na barua ya Jaji Mutungi kwenda benki mbalimbali ikiwemo NMB tawi la Ilala kwa ajili ya kufungua akaunti nyingine ya chama huku akifahamu kikatiba hairuhusiwi.
Chama kimebaini kwamba kuna njama za kuandaa nyaraka batili zinazofanywa na Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya kufungua akaunti nyingine baada ya kukataliwa na NMB,” amesema.
Abdallah Katau, Mwenyekiti ya Bodi ya CUF amesema, “Bodi hii inawajibika kwa wanachama wake na hakuna sehemu nyingine yoyote. Hakuna bodi mbili kama baadhi ya watu wanavyodai.”
Katau amesema msajili hawezi kukisumbua chama cha CUF kwani chama hicho kipo imara na kimeenda mahakamani ili haki itendeke.