test

Jumamosi, 10 Septemba 2016

‘Kama huna wivu na mpenzi wako una matatizo’


KARIBU ndugu msomaji katika safu hii ya mahusiano ambayo hukupa fursa ya kufahamu na kujadiliana mambo mbalimbali ya mahusiano ya kimapenzi.
Awali ya yote, nitoe shukrani zangu za dhati kwa wote ambao wamekuwa wakipiga simu au kutuma sms kupongeza au kuchangia juu ya mada mbalimbali katika safu hii.

Baada ya salamu hizo, tuone maoni ya wasomaji wangu juu ya mada ya Jumanne iliyopita iliyosomeka; ‘Wivu ni kipimo cha mapenzi?’
Wivu ni ishara kubwa sana ya kugundua kuwa mpenzi wako anakupenda kwa dhati. Sidhani kama kuna mtu asiye na wivu, ila tunatofautiana, wapo watu wanaouonyesha dhahiri na wengine huuficha, lakini wanaumia kwa ndani. Mimi ninao ila huwa ni ngumu kuuonyesha na hata nikiuonyesha ni mara chache na anaweza asijue namwonea wivu. Benedict Simba.
Wivu si kipimo cha mapenzi ila kujiheshimu ndio kipimo cha mapenzi. Brayson kutoka Tanga.
Mapenzi bila wivu si mapenzi hayo. Ramadhan Mkindi wa Arusha.
Wivu ukizidi sana matokeo yake ni ugomvi. Seleman Juma wa Buja, Dar es Salaam.
Wivu unaweza kuwa ni moja kati ya njia za kulinda penzi. Omary Hassan wa Tanga. Wivu ni chachu ya mahaba, haiwezekani wawili wapendanao muishi bila ya kuoneana wivu. Ukimuona mpenzi wako hana wivu na wewe, si bure ana matatizo au hana penzi la dhati. Wivu usipite kiwango. Seif Madongo ‘Mr Love’ wa Yombo Vituka, Dar es Salaam.
Wivu ni moja ya ishara ya mapenzi ya dhati, lakini usizidi kiasi, kama hakuna wivu, basi hakuna mapenzi. Ila usizidi kumnyima mwenzako uhuru. Penueli Bankuwiha wa Kivule, Dar es Salaam.
Kutokana na hali ya mahusiano ilivyo kwa sasa, thamani ya mapenzi imeisha ladha, kwa kweli wivu ni muhimu kwenye mahusiano, ni ishara ya upendo kwa mwenza wako. Ninja Sokito wa Mabibo, Dar es Salaam.
Wivu ni kero sana katika maisha, kwani unaweza kumuaga mpenzi wako unakwenda mahali fulani kikazi, ukichelewa kurudi utakutana na simu nyingi za lawama au sms.
Wivu ndio mapenzi ila uchungwe usizidi si vizuri kutokuwa na wivu na mpenzi wako au mkeo, ukawa unaona kila anachofanya ni sawa, Dayana King wa Mbezi Mwisho, Dar es Salaam.
Wivu ni jambo jema sana katika mapenzi, ukiona mpenzi wako hakuonei wivu, jua hana mapenzi ya dhati na wewe, niwashauri watanzania wenzangu kuwa, wivu ndio msingi imara katika mapenzi. Jumanne Ally wa Igogo, Mwanza.
Wivu ni mzuri katika mahusiano ila ukizidi unakuwa siyo mzuri kwa sababu unapunguza furaha ya mapenzi. Allan Mhina wa Handeni, Tanga.
Kwenye uhusiano wa kimapenzi bila kuwa na wivu hayo siyo mapenzi, lazima wapendanao wawe na wivu.  Jamal Ibrahim wa Dar es Salaam.
Wivu ni jambo la kawaida tu kwa mpenzi wako, lakini ukizidi ujue anayofanya yeye anahisi na wewe unafanya kama hivyo. Rehema Amos Maganga ‘Mama Shirazy’ wa Kimara Korogwe, Dar es Salaam.
Mtu mwenye wivu ndio mzuri, maana anatambua umuhimu wa mapenzi ndani ya watu wawili mnaopendana, pia mtu huyu mwenye wivu anaonyesha ni jinsi gani anavyokupenda si yule ambaye hamjali mtu wake. Bernard Kilala.
Wivu ni kiungo muhimu sana katika mapenzi, kama hakipo hata upendo haupo, endapo mmoja wa wapenzi atadharau huduma ya kiungo cha wivu katika mapenzi, jua hajui hata maana ya mapenzi, hata neno lenyewe penzi ajifunze. Abely Gaba.
Wivu kila mtu anao ila usizidi sana mpaka mpenzi wako akajua, akishajua atakutesa sana, la sivyo utaumia moyo wako kila siku. Jonasi Mkude wa Tanga.
Wivu ni kitu muhimu kabisa katika mapenzi, kama huhisi wivu kwa umpendaye, jua hakuna mapenzi hapo ni kupotezeana muda tu, hata katika imani ya dini yetu ya kiislam, wivu umeruhusiwa ila usiwe wa kipumbavu, mtu asiye na wivu hatoingia katika pepo, kama wanyama wanaoneana wivu, iweje sisi binadam!  Ahmad Samatta.
Wivu unaweza kuchukuliwa katika sehemu tofauti, kwanza unahisi na mwenzako ni kicheche kama ulivyo wewe. Pili, ni kuhisi kuwa mwenza wako hana upendo wa dhati kama ulivyo nao wewe, ila ninavyoona anayeonyesha wivu kwa mwenzake huyo ndiye mwenye mapenzi bora na hatakubali kumwona anapotea. Shinaldo Shija.
Kama kweli unampenda mpenzi, mume au mke wako, huwezi kukaa kwa muda mrefu bila kujua sehemu alipo na anachofanya. Usipokuwa na wivu kwa mtu ambaye unampenda kwa dhati, ni dhahiri kuwa humpendi kwa asilimia 100. Juma Ally Kazoba wa Mwanza.
Mtu huwa anapenda sana ndio maana anakuwa na wivu. Mimi nina mpenzi wangu, nina muda mrefu naye miaka mitatu, kwa kweli huyu nilimpenda na bado nampenda, lakini tabia zake mimi zimenishinda, anapenda sana hela (fedha), mwanzo alikuwa akitaka kitu namwambia subiri, anasubiri ila kwa sasa akitaka kitu ni hapo hapo. Nimemfanyia mambo mengi mazuri ambayo hayana idadi, simuelewi kama mwanzo, ni mgumu kuelewa kitu ambacho kimenifanya nifikirie amepata mwanaume mwingine. Raymond wa Mkuranga.
Wivu ni hisia fulani juu ya mpenzi ama mwenza wako. Na hisia zinaweza kuwa ni sahihi ama laa, ila kwa yule umpendaye ni lazima kila wakati umfikirie, hivyo, kuwa na wivu na mwenza wako ni jambo bora na la msingi katika mahusiano ya kimapenzi. Mie nikirudi nyumbani mke wangu lazima apitie kunisachi kila mahali ndipo aniruhusu kuoga na nikiwa nje na nyumbani simu kila mara mpaka ‘nam-divert busy’ kwa anavyonisumbua. Zutto wa Segera, Tanga.
Kwa kweli wivu ni ishara ya mapenzi ya dhati kabisa na kama mpenzi wako hakufatilii ujue hakupendi kabisa. Wivu ndio ishara kubwa ya mapenzi. Michael Joseph ‘Mwilo’ wa Handeni, Tanga.
Mapenzi si mate kila mtu ayapate, ninasema hivyo kwa sababu wivu ni ishara tosha ya kujua jinsi gani unampenda mwenzi wako, kwa asiyejua thamani ya mapenzi hawezi kumuonea wivu mwenzake. Wamwisho Kufa, Nevada Salon, Buguruni Sheli, Dar es Salaam.
Wivu ndio kila kitu katika mapenzi ya mtu na mtu, usipokuwa na wivu hakika haumpendi mwenza wako. Sildo Nassary wa Visiga, Kibaha.
Nasapoti kuwa wivu ni kipimo cha mapenzi kwa sababu upendo unatoka moyoni, hauwezi kuvumilia kuona mwenzako anakusaliti kama unampenda kwa dhati, lazima roho yako iume, labda kama hujampenda na kuridhika naye. Leonald Joseph Sakala wa Mtaa wa Bugarika A, Nyamagana, Mwanza.
Wivu ni sehemu tu ya kuonyesha upendo kwa mwenzi wako, lakini nadhani hofu ya Mungu na uaminifu ni silaha kubwa katika kuonyesha mapenzi kwa umpendaye. Dart Mhando wa Mbezi, Dar es Salaam.
Mpenzi wako akikuonea wivu jua ana mapenzi ya dhati kwako ndio maana anakuwa na wivu na wewe. Zai wa Dar es Salaam.
Kwa kweli bora niwe limbukeni wa mapenzi, lakini mapenzi bila wivu ni sawa na bure, kama hauna wivu na mpenzi wako, kama upo naye ni kwa ajili ya kitu fulani, lakini si kwa upendo, wivu unaleta uaminifu kwenye mahusiano. Sefu Komba wa Temeke, Dar es Salaam.
Kwa kweli wivu ni upendo maana kama hujamuonea wivu mpenzi wako, basi itakuwa humpendi na ndio maana sisi waislamu tunasema wivu ni sunnah kwa maana hata Mtume wetu Muhammad (S.A.W), aliwaonea wivu wake zake, hususan Bi Khadija. Kidume Ndago wa Mwananyamala Mchangani, Dar es Salaam.
Wivu ni sunna na kama hauna wivu kwa mwenza wako basi hata mapenzi ya kweli hauna kwake. Wivu ndio ishara ya mapenzi ya pande zote mbili. Protini wa Mijelele Masasi.
Wivu katika mahusiano ni alama ya upendo kwa sababu mmoja kati yenu akionyesha wivu anakukinga na hatari ambayo ingeepukika. Kama mwenza wangu akionyesha wivu, najua ananipenda na ananilinda na vishawishi. Bupe Xavery wa Njombe.
Ndugu msomaji, kwa leo tuishie hapo, tukutane Jumanne ya wiki ijayo ambapo nitawaletea mada nyingine motomoto. Kama una maoni juu ya safu hii, tuma kupitia namba ya simu 0713 556022 au anuani pepe, michietz@yahoo.com.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx