KAMPUNI za Selcom na Puma Energy za Dar es Salaam, zinatarajiwa kutuzwa leo na Rais Dk. John Magufuli kwa kudhamini Wiki ya Nenda kwa Usalama kwa mwaka huu inayoadhimishwa mkoani Geita.
Wiki ya Nenda kwa Usalama mwaka huu inazinduliwa kitaifa mkoani Geita ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Magufuli.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohamed Mpinga, alisema wiki iliyopita kwamba Wiki ya Usalama Barabarani itaanza leo Septemba 26 hadi Oktoba 1, 2016.
Selcom na Puma Energy mwaka huu zimejitokeza kudhamini Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa kutoa vifaa mbalimbali zikiwamo stika.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mikakati wa Selcom, Benjamin Mpamo, alisema wanatambua wajibu wao kwa jamii hasa ikiwemo kulinda usalama wa raia na maisha yao pindi wanapokuwa barabarani.
“Selcom inatambua kwamba ajali za barabarani zinapoteza uhai. Kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kutoa fursa sawa kwa kampuni za ndani za Tanzania ili yaweze kuonyesha weledi wake, Selcom imeamua kuunga mkono juhudi hizi kwa kurudisha sehemu ya faida ndogo inayopatikana kwa Watanzania kwa njia hii.
“Tutashirikiana na Polisi kuandaa mipango mbalimbali ili kutoa elimu kwa kuwa ajali za barabarani zinaepukika pindi jamii inapopata elimu ya kutosha,” alisema.
Selcom ni kampuni ya kwanza nchini iliyojitokeza kudhamini wiki ya Nenda kwa Usalama.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mpinga alisema Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limeelekeza wamiliki wa magari ya usafirishaji mizigo yanayokwenda mikoani na nje ya nchi kuajiri madereva zaidi ya mmoja katika magari hayo, ili kuepusha ajali zinazotokana na uchovu wa madereva na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari.