MTUMISHI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Igunga, Tabora, Michael Joseph amedaiwa kuandika barua ya kuacha kazi ndani ya saa 24 na kutoroka kwenye kituo chake cha kazi.
Hatua hiyo imeelezwa inatokana na kudaiwa kutapeli fedha baadhi ya wananchi kwa kuwaahidi viwanja vya makazi na kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya watuhumiwa wenye kesi Takukuru.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, baadhi ya wananchi waliodai kutapeliwa fedha zaidi ya Sh milioni 8 wamedai wametapeliwa na mtumishi huyo akishirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya ardhi kutengeneza hati bandia.
Aidha, wamedai mtumishi huyo pia amekuwa akitoa siri za ofisi pindi wananchi wanapopeleka malalamiko yao na kuomba mamlaka husika kuhakikisha mtumishi huyo anakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Gazeti hili lilijaribu kumtafuta mtuhumiwa huyo aweze kutolea ufafanuzi tuhuma zinazomkabili, lakini hakupatikana katika kituo cha kazi wala kwa simu yake ya mkononi ilioonesha kuzimwa muda wote alipotafutwa.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Fidelis Kaluugula, amethibitisha kuwapo kwa taarifa za wananchi hao kudaiwa kutapeliwa na mtumishi huyo na kwamba anatafutwa ili ahojiwe.
“Ni kweli huyu Michael Joseph tumepokea barua yake ya kuacha kazi ndani ya saa 24 na tayari alitoroka kuhojiwa na kutokana na tuhuma na malalamiko dhidi yake yaliyoripotiwa katika kituo chake cha kazi," alisema.
Alitoa mwito kwa watumishi kuzingatia miiko ya utumishi ikiwa ni pamoja na kutojiingiza katika vitendo vya tamaa kwani vinaweza kuwaondolea uaminifu kwenye jamii na kuwaharibia malengo.