“MAKAO makuu ya kitaifa ya nchi ni kitu cha kudumu. Ikiwa tunakata shauri makao makuu yabakie hapa hapa Dar es Salaam au yahamishiwe Dodoma tutakuwa tunatoa uamuzi wa kudumu, kwa hiyo zile sababu ambazo ndiyo msingi wa uamuzi wetu zinabidi ziwe sababu za kudumu.
Tusizitumie sababu zisizokuwa za kudumu kufanya maamuzi ya kudumu. “Kwa muda wa miaka 20 au 50 na hata miaka 100 kutoka sasa, mji wa Dodoma bado utakuwa katikati ya nchi na Dar es Salaam vile vile kubakia mpakani mwa nchi. Kutokana na sababu hizo, Kamati Kuu ya Tanu (Tanganyika African National Union) imezingatia sababu za kudumu na kukata shauri la kudumu, imekataa kabisa kutumia sababu hafifu kushauri suala la kudumu.”
Hiyo ni sehemu ya hotuba aliyoitoa Mwalimu Nyerere mwaka 1973 kwa njia ya redio baada chama tawala wakati huo cha Tanu, kuamua kuhamishia makao makuu ya serikali (na hata ya chama chenyewe) mjini Dodoma. Katika hotuba yake hiyo, Mwalimu alisema gharama za kujenga makao makuu ya kitaifa ni kitu cha muda mfupi na pia akasema Kamati Kuu ya Tanu imeamua kwamba makao makuu ya taifa yatajengwa Dodoma katika miaka 10 ijayo.
Mwalimu pia alitangaza kwamba serikali inachukua hatua za haraka kutekeleza uamuzi huo. Je, ni kwa nini kwa miaka 43, serikali ya Mwalimu Nyerere na zilizofuata baadaye zilishindwa kuhamia Dodoma? Timu kutoka magazeti ya Serikali, HabariLeo na Daily News, hivi karibuni ilimtembelea Mzee Pius Msekwa nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam ambapo ilifanya naye mazungumzo kuhusu alivyomfahamu Mwalimu Nyerere ambaye nchi yetu inajiandaa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu afariki dunia.
Moja ya swali ambalo timu hiyo ilimuuliza na yeye kulijibu kwa mapana lilikuwa ni nini hasa kilikwamisha nchi kuhamia Dodoma na hasa kwa kuzingatia kwamba hatua hiyo Mwalimu alitaka iwe imekamilika ndani ya miaka 10 (kuanzia mwaka 1973). Akijibu swali hilo, Mzee Msekwa ambaye ni mcheshi na mwenye kumbukumbu nyingi, anaanza kwa kusema kwamba umuhimu wa nchi kuhamia Dodoma bado uko pale pale kama ilivyokuwa mwaka 1973 wakati azimio hilo linapitishwa.
Mkongwe huyu wa siasa na uongozi ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) anasema: “Unapotawala nchi ukiwa katikati ni tofauti na unapokuwa pembeni… Kitu ambacho labda kimebadilika sasa hivi ni suala la ulinzi na usalama. “Wakati ule, katika kuelezea sababu za kuhamia Dodoma, kuna mmoja alijenga hoja kwamba sababu nyingine ya umuhimu wa kuhamia Dodoma ni ulinzi. Alisema kwa Dar es Salaam adui anaweza kuja kupitia bahari na kujificha lakini Dodoma mpaka asafiri kilometa 300 hadi kufika Dadoma atakuwa ameshaonekana. Lakini siku hizi hilo halina nguvu kwa sababu mtu anaweza kukupiga Dodoma akiwa Dubai,” anasema Msekwa.
Anasema alikuwepo kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Tanu kilichofanya uamuzi huo wa kuhamia Dodoma na kwa bahati nzuri anajua takribani mambo yote yaliyofuata baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo na hasa kwa vile aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa CDA. “Sababu iliyotukwamisha kuhamia Dodoma kwa kipindi chote hicho ni moja tu. Nayo ni uwezo wa kifedha wa serikali wa kuhamisha makao makuu ya serikari kutoka Da r es Salaam kwenda Dodoma,” anasema.
Akifafanua kwanini uwezo wa kifedha ulikuwa ni muhimu wakati ule, Msekwa anasema kwamba hapakuwa na mtu au chombo kingine cha kutekeleza hilo zaidi ya serikali yenyewe. “Wakati huo hapakuwa na sekta binafsi kama ilivyo sasa. Na mkumbuke wakati huo ilikuwa ni miaka michache baada ya kupitishwa kwa Azimio la Arusha. Mambo yote yakawa yanaendeshwa na serikali peke yake, hakuna sekta binafsi wala hakuna chombo kingine kinachoweza kuwekeza Dodoma. Ni serikali peke yake,” anasisitiza.
Anasema licha ya majukumu yake mengi, serikali, baada ya kupitisha uamuzi huo, ilianza kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo. Anasema hatua hiyo ilikwenda sanjari na kuanzishwa kwa mikakati muhimu ikiwa ni pamoja na kuundwa wizara maalumu kwa ajili ya ustawishaji makao makuu pamoja na kuunda Mamlaka ya Kustawisha Mji wa Dodoma (CDA). Anafafanua kwamba fedha zilizotolewa kwa wizara na mamlaka hiyo zilitumika kwa ajili ya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, mfumo wa majitaka na majisafi na kupanda miti.
“Moja ya kazi kubwa ilikuwa ni kupanda miti kwa sababu wakati ule Dodoma kulikuwa na ugonjwa wa macho (vikope). Kulikuwa na upepo mkali na vumbi, hivyo kusababisha ugonjwa wa macho. Watu wengi, wakazi wa Dodoma walikuwa wanaugua ugonjwa huo wa macho. “Dodoma wakati huo ilikuwa ndogo sana. Mwaka 1973 ilikuwa na watu kama 40,000 hadi 45,000 tu hivi. Na ilikuwa kama jangwa hivi, hivyo ilibidi serikali ianze upya kupatengeneza ikiwa ni pamoja na kupanda miti. Hiyo kazi ya kupanda miti ndio ilikuwa kubwa,” anasema.
Mzee Msekwa anasema hatua za kupatayarisha Dodoma ili kupokea ujio wa makao makuu ya nchi zilikuwa zinakwenda vyema lakini zikakwamishwa na majanga matatu makubwa yaliyoikumba nchi na hivyo kusababisha kuwa na tatizo la fedha. Anasema miaka mitatu tangu kufanyika kwa uamuzi huo, ulipofika mwaka wa nne, yaani mwaka 1977, janga la kwanza likaikumba nchi ambalo lilikuwa ni kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Anasema hatua hiyo iliifanya Tanzania kuanza kujipanga kivyake hasa katika huduma zilizokuwa zinatolewa na jumuiya hiyo. “Hii ni kwa sababu huduma zilizokuwa zinatokea na Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikuwa haziingii kwenye bajeti ya serikali, yaani mambo kama usafirishaji kwa njia ya reli, kwa njia ndege na masuala ya posta na simu… Yaani mambo yote ya mawasiliano na uchukuzi wala hatukuwa na wizara hiyo kwa sababu yalikuwa yanashughulikuwa na jumuiya. “Kwa hiyo jumuiya ilipovunjika, kipaumbele cha bajeti ya serikali kikawa ni kuhudumia mambo hayo kuliko kuhamia Dodoma,” anasema.
Anasema kabla hilo halijakaa vyema, mwaka 1979, nchi ikajikuta katika janga lingine na safari hii likiwa ni vita ya kumuondoa Idi Amin Dada wa Uganda aliyevamia sehemu ya Tanzania. “Hapo ikabidi fedha nyingi za serikali zitumike katika kuhudumia vita hiyo,” anasema na kuongeza kwamba, kama alivyosema Mwalimu Nyerere, uvamizi huo ilikuwa ni sawa na nyoka aliyekuingilia ndani ya nyumba na kujificha chini ya uvungu, watoto hawawezi kulala hadi uhakikishe umemuondoa nyoka huyo.
Anasema hata kabla ya vita ya Uganda, nchi ilikumbwa na janga la tatu ambalo lilikuwa ni kupanda maradufu kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia. “Na haya yote yalitokea katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, mwaka 1977, 1978 na mwaka 1979. Bei za mafuta zilipanda sana na mnajua umuhimu wa mafuta katika uchumi wa nchi,” anasema. Anasema baada ya mambo hayo kuikumba nchi, bajeti ya kuhamia Dodoma ikawa kama imefutwa kabisa, isipokuwa kwa mambo madogomadogo kama vile ya kulipa mishahara.
Mzee Msekwa anasema athari za majanga hayo hazikuisha ndani ya mwaka mmoja bali ziliendelea kuiathiri nchi kwa kipindi kirefu. Anasema akiwa Mwenyekiti wa CDA, kuna wakati Mwalimu Nyerere alimwita na kumwambia ajaribu kuhamisha wizara moja ili kuonesha mfano kwamba wazo hilo la kuhamia Dodoma linawezekana. Anasema wizara waliyoona ni bora kuanza nayo ni Wizara ya Madini.
Anasema alizungumza na waziri mhusika lakini alipompa mahitaji ya kuhamia Dodoma, wakati huo bado ni serikali pekee ikitegemewa kufanya kila kitu ikaonekana haiwezekani. “Nilimwonesha Mwalimu matokeo, akasema ni kweli uwezo huo hatuna lakini akanitaka nijaribu kutafuta wizara ndogo zaidi kwa sababu Wizara ya Madini na Nishati ilionekana ni kubwa sana,” anasema.
Anasema wizara waliyodhani ni ndogo ilikuwa ya Mambo ya Nje, kwa maana kwamba watumishi wake wanaoishi Dar es Salaam ni wachache kwa vile wengi wanaishi kwenye balozi mbalimbali nje ya nchi. Lakini anasema waziri husika alipompa orodha ya mahitaji ili wizara yake iweze kuhamia Dodoma bado ikaonekana mzigo huo kubebwa na serikali pekee ulikuwa bado mkubwa.
“Tena waziri akaniambia nyie mnafikiria wizara pekee lakini hili ni pamoja na mabalozi walioko hapa nchini,” anasema na kuongeza kwamba aliporudisha ripoti kwa Mwalimu, akashauri wasubiri kwanza wakati nchi ikizidi kujijengea uwezo. Maneno ya Msekwa yanalingana na aliyoyasema Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, wakati akihutubia wananchi, Novemba 29, 2001. Pamoja na mambo mengine, alitoa sababu kadhaa zilizopandisha deni la taifa (unaweza kuipata hotuba hiyo katikawww.egov.ho.tz).
Rais Mkapa alisema: “Sababu ya pili ya mlundikano wa madeni ni athari kubwa zilizotupata kutokana na matukio ya kitaifa na mengine nje ya taifa letu. Hayo ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta katika miaka ya 70, ukame, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, vita dhidi ya Nduli Idi Amin, na kushuka kwa bei ya mazao yetu makuu kwenye soko la dunia.”
Mkapa akaendelea kusema: Kwa upande mmoja matukio hayo yalipunguza sana ukuaji wa uchumi wetu, na hivyo uwezo wa kulipa madeni ya zamani, lakini pia, kwa upande mwingine, yalitulazimisha tukope zaidi ili kuendeleza mipango yetu ya maendeleo. Hata pale ambapo fedha za kulipia baadhi ya madeni ya nje zilikuwepo, uhaba wa fedha za kigeni ulitufanya tushindwe kulipa deni la nje kwa fedha za kigeni.
Hivyo deni liliendelea kukua, bila uchumi kukua kwa kasi ya kuwezesha kulipa.” Je, kwa mtazamo wa Mzee Msekwa, sasa inawezekana kuhamia Dodoma kama Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ilivyopania? Akijibu swali hilo, Mzee Msekwa anasema kwamba kwa sasa inawezekana kwa sababu yale yaliyokwamisha erikali ya Mwalimu Nyerere na zilizokuja baadaye hayapo.
Kikubwa anasema kwa sasa serikali haifanyi mambo yenyewe bali mambo mengi inafanya kwa kusaidiana na wawekezaji kutoka sekta binafsi. “Sasa tuna sekta binafsi. Hii inaweza kuwekeza Dodoma na kurahisisha sana hatua ya kuhamia Dodoma. Kwa mfano, mfanyabiashara mmoja tu, Mustafa Sabodo, ametangaza kwamba atawekeza Dodoma Sh trilioni 10 kama njia ya kuunga mkono hatua ya Rais Magufuli kuhamia Dodoma.
“Tunapozungumzia… huko kuwekeza ni pamoja na kujenga majengo ambayo yanaweza kukodiwa na wizara na idara za serikali. Hata hapa Dar es Salaam kuna wizara takribani 11 hazipo katika majengo ya serikali,” anasema na kuongeza kwamba anaamini sekta binafsi itasaidia sana suala zima la kuhamia Dodoma. Anasema hata watumishi wengi wa serikali jijini Dar es Salaam hawaishi katika nyumba za serikali bali wanapanga kwenye sekta binafsi na hivyo sekta hiyo itawawezesha kuishi Dodoma kwa kuwapangisha.
“Kwa hiyo nasema, sababu za kuhamia Dodoma bado zipo, nia ya kuhamia Dodoma bado ipo na ameionesha Rais Magufuli, na uwezo wa kuhamia Dodoma sasa upo. Napenda nitumie maneno hayo kama alivyoyatumia Mwalimu Nyerere tulipodhamiria kumuondoa Idi Amin katika ardhi yetu,” anasema.
Mbali na uwepo wa sekta binafsi kama mbia muhimu katika kutekeleza suala la kuhamia Dodoma, Mzee Msekwa pia anasema juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kubana matumizi na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali anaamini uwezekano wa kuhamia Dodoma upo. “Sasa hivi walipa kodi wako wengi zaidi (ikiwemo sekta binafsi). Zamani walipa kodi wa uhakika walikuwa wafanyakazi wa serikali pekee kwa sababu wanakatwa kodi moja kwa moja lakini wengine wengi walikuwa wanakwepa.
“Kwa hiyo utaona uwezo wa serikali sasa ni mkubwa zaidi, uwezo wa sekta binafsi nao ni mkubwa ambao haukuwepo wakati ule na utayari wa sekta binafsi wa kuunga mkono jambo hili umejionesha. Yote haya yanaashiria kwamba Rais wa sasa atafanikiwa kutupeleka Dodoma,” anasema Mzee Msekwa.
Pius Msekwa ni nani hasa, yuko wapi na anafanya nini? Ni magumu gani aliyoyapata wakati akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano? Na ni kipi hasa kilichoibua sakata la G 55 ambapo wabunge walitaka kuunda Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano?
Fuatilia ndani ya HabariLeo pekee katika matoleo yajayo ili kupata majibu ya maswali hayo.