MADEREVA 10 waliokuwa wametekwa na kuokolewa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wamesema wataendelea na kazi ya udereva kwenda nje ya nchi, kwani kilichotokea ni ajali kazini kama ilivyo kazi nyingine.
Mmoja wa madereva hao waliorejea nchini juzi alasiri na kupokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Kumbuka Suleiman alisema kazi hiyo ndiyo waliyojifunza, hivyo hata wakiacha ipo siku wataajiriwa sehemu nyingine na kufanya kazi hiyo hiyo.
Madereva hao waliopata mateso makali ikiwa ni pamoja na kutembea kilometa 50 na sehemu nyingine kwa magoti wakiwa mateka wa waasi hao, walirejea nchini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda (RwandAir).
Alisema baada ya kuwasili walipewa likizo ya siku tano na mwajiri wao na kutakiwa kuripoti kazini Jumatatu ijayo ambapo watakwenda kufahamu maamuzi ya kiongozi wao kazini ikiwa waendelee na kazi au likizo.
Walipowasili nchini walilakiwa na vilio vya furaha kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki baada ya kutekwa siku ya Jumatano asubuhi ya Septemba 14 mwaka huu na kuokolewa na majeshi ya DRC Alhamisi jioni.
Baada ya kutekwa, walisema waliteswa usiku kucha, walikunywa maji machafu yaliyotuama kwenye madimbwi huku wakitembea katika mapori manene yaliyowafanya kushindwa kutembea kwa kusimama, bali kutumia magoti.
Madereva hao baada ya kukombolewa walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Maniema na kupatiwa dawa za maumivu baada ya wote kukutwa wakiwa wazima.
Kikundi cha waasi cha Maimai kiliwateka madereva hao 13 wakiwemo raia wa Kenya na kutaka kulipwa dola za Marekani 4,000 (Sh milioni 8.4) kwa kila mmoja ili kuwaachia huru. Utekaji huo ulifanyika katika eneo la Namoyo, Jimbo la Kivu Kusini juzi na malori manne yaliteketezwa kwa moto.
Kati ya malori yaliyotekwa, manane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania, Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na mfanyabiashara kutoka Kenya na yalikuwa yameshusha saruji.
Dewji alisema ataendelea kufanya biashara na nchi ya DRC na kamwe tukio hilo halitamfanya kuacha kufanya biashara, bali atakachofanya ni kuomba wanajeshi kuvusha magari hayo katika maeneo hatarishi.
Alishukuru Serikali ya Tanzania na DRC kwa kuwa naye bega kwa bega katika harakati za kuwaokoa madereva hao na kuwa kutokana na kuchomwa moto kwa magari yake manne amepata hasara ya Sh milioni 600.