Kwa niaba ya Wabunge wote wa CUF napenda kuwajulisha wanachama wa CUF walioko Dar Es Salaam kwamba tumeahirisha mapokezi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la CUF, Kamati ya Uongozi ya chama na Katibu Mkuu tuliyopanga kuyafanya kesho Ijumaa saa 2.00 asubuhi kwenye Ofisi Kuu ya CUF Buguruni.
Tumefanya uamuzi huu baada ya kujiridhisha kuwa hali ya usalama wa wanachama watakaohudhuria na viongozi watakaopokelewa siyo nzuri.
Tunazo taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya Ofisi huku yakilindwa na vyombo vya dola tangu Ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.
Wakati tunaahirisha mapokezi ya kesho tunajipa muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba wanachama wote walioko DAR, MIKOANI na ZANZIBAR wawe watulivu kwani chama na viongozi makini hawawezi kuwa tayari kuona maisha na usalama wa wanachana na viongozi vinahatarishwa kwa kuigeuza Ofisi Kuu kuwa uwanja wa mapambano (battle ground).
Imetolewa na
RIZIKI SHAHARI (MB),
KIONGOZI WA WABUNGE,
THE CIVIC UNITED FRONT,
28 Septemba 2016.