Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imegeuziwa kibao katika suala la Escrow, imefahamika.
Kampuni
hiyo imetakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 (Sh
bilioni 216.2 ) kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zikiwa fedha
za ziada ambazo ililipwa kabla ya hesabu kufanywa upya.
Hatua
hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa
Biashara uliotolewa Septemba 12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa
Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.
Mahakama
hiyo ilitoa uamuzi huo kutokana na kesi iliyofunguliwa na Benki ya
Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) dhidi ya Tanesco ikidai kulipwa
Dola za Marekani milioni 369.
Kwa
mujibu wa Wakili wa Tanesco, Richard Rweyongeza, amesema walichokuwa
wanabishania mahakamani si Tanesco kulipa bali walikuwa wanabishania
shirika hilo litalipa kiasi gani na linamlipa nani.
“Kabla
hatujaingia katika kutetea kesi hiyo, mwaka 2014 mahakama hiyo ilisema
inayo madaraka na ikaamuru Tanesco kuilipa SCB-HK.
“Sisi
tuliingia kutetea baada ya uamuzi huo, Mei, 2014 tukaomba hesabu
zifanyike upya kwa malekezo yaliyotolewa na mahakama hiyo kujua deni
halisi.
“Hesabu zilipofanyika kwa mtaji wa mwekezaji, walichukua mkopo wakahesabu kuwa ni mtaji, hatua hiyo ilikataliwa na mahakama.
“Kabla
ya hesabu kufanyika ndipo likaingia suala la akaunti ya Tegeta Escrow.
Fedha zilipochukuliwa katika akaunti hiyo, SCB-HK wakabadilika wakasema
hakuna haja ya kufanya hesabu upya kwa sababu Tanesco wamekubali viwango
hivyo ndiyo sababu waliwalipa IPTL.
“Tulibishania
hoja hiyo ya kulipa kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike
upya, mahakama ilikubali hesabu ifanyike kwa kutumia mkopo wa wana hisa.
“Baada
ya kuamuru hivyo, deni likashuka kutoka walichokuwa wakidai Dola za
Marekani milioni 369 hadi kuamuriwa kulipa Dola za Marekani milioni
148,”anasema Wakili Rweyongeza.
Alisema
IPTL walilipwa Dola za Marekani milioni 246 kwa kutumia viwango vya
zamani na kwamba uamuzi uliotolewa unaanza kutumika katika kipindi chote
ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa mpaka mwaka 2015.
“Kutokana
na hesabu hizo gharama ilikuwa chini, IPTL ililipwa zaidi hivyo
inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 kwa Tanesco,”alisema.
Rweyongeza
alisema walipendekeza SCB-HK wadai fedha zao kwa IPTL lakini mahakama
hiyo ilikataa na kuamuru Tanesco ndiyo walipe hivyo kwa mtazamo wa
kawaida IPTL inatakiwa kurejesha fedha kwa shirika hilo.
Katika
kuhitimisha, mahakama hiyo ilisema pande zote mbili zinazopingana
zilishinda katika maeneo muhimu waliyokuwa wakibishania lakini
zilipoteza katika hoja nyingine.
Baada
ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo mahakama iliamuru pande hizo mbili
kulipa gharama za usuluhishi na nyingine kwa viwango sawa.
Malipo
hayo na anayelipwa katika mabano ni Dola za Marekani 254,775.02
(Profesa MC Rae), Dola 171,278.36 (Profesa Douglas) na Dola 370,126.76
kwa ajili ya Profesa Stem.
Gharama
nyingine zilizokadiriwa moja kwa moja ni Dola za Marekani 157,336.26 na
gharama za utawala kwa mahakama hiyo Dola za Marekani 180,000 ambako
jumla ya gharama zote wanazotakiwa kulipa Tanesco na SCB-HK ni Dola za
Marekani 1,133,516.42.
Hata
hivyo Rweyongeza alisema pamoja na ushindi huo hawakuridhishwa na
uamuzi huo kwa sababu katika uamuzi wa kwanza, mahakama hiyo ilikataa
hesabu kupigwa kwa kutumia kiwango cha 22.31 lakini bado katika uamuzi
huu walitumia kiwango hicho kufanya hesabu hivyo walikosea kufanya
hivyo.
Hoja ya pili, alisema SCB-HK si mwekezaji hivyo hakustahili kupeleka kesi hiyo mahakamani na kwamba hapakuwa na hoja.
“Sababu
nyingine ya kutoridhishwa na uamuzi huo ni kwamba hatukupewa nafasi ya
kujibu hoja mpya zilizowasilishwa kuhusu Tanesco kwamba ilidanganya,
tulipaswa kujibu kwa maelezo ya mashahidi si mawakili.
“Tuliwasilisha
hoja kwa maandishi, zilipotokea hoja mpya tulitakiwa kuzijibu kwa
kuleta mashahidi, tunapinga pia uamuzi ulioitambua SCB-HK kuwa
ilistahili kisheria,”alisena Rweyongeza.
Suala
hilo limeibuka ikiwa imepita miaka mitatu tangu Serikali kupitia
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini
kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Dola za Marekani milioni 200 (zaidi ya
Sh bilioni 300) kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha
hizo zilitolewa na kwenda kwa mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power
Solutions Tanzania Limited (PAP), Harbindar Singh Sethi mwenye makazi
yake nchini na Afrika Kusini.
Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.
Chanzo cha Escrow
Mwanzoni
mwa miaka ya 1990 nchi ilikuwa na upungufu wa umeme kutokana na
upungufu wa maji kwenye mabwawa, ambapo 1994 serikali ilitoa kazi ya
uwekezaji kwa IPTL ilikuwa iliyokuwa ikimilikiwa na VIP ya Tanzania
iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia yenye asilimia 70.
Tanesco
na IPTL walisainiana mkataba wa miaka 20, hata hivyo uzalishaji
haukuanza mara moja kutokana na mgogoro ulioibuka baina yao (Tanesco na
IPTL) .
Mwaka
2002 IPTL ilianza kuzalisha umeme na mkataba ukaanza kuhesabiwa hapo,
lakini kutokana na mgogoro ikafunguliwa akaunti ya Escrow na mwaka 2004
Tanesco ilifungua shauri kupinga tozo la Capacity Charge
Uwiano
wa mtaji ni 70 kwa 30 na uamuzi haujabadilishwa na mahakama yoyote.
Mwaka 2004 Kampuni ya Mkono & CO advocates iliishauri Tanesco
iendelee kupinga Capacity Charge London.
Inaelezwa
kuwa Agosti 2005, benki ya SCB-HK ilinunua kwa bei ya punguzo ya dola
za Marekani 76.1 kutoka Benki ya Malaysia ya Danaharta baada ya
kushindwa kurejesha deni la muda mrefu kutoka IPTL.
Bei
halisi ya deni hilo ilikuwa ni dola milioni 101.7 kwa mujibu wa
ushahidi uliopo ambako IPTL ilikopa dola milioni 100 mwaka 1998 kutoka
kwa mbia wa benki ya Malaysia ili kujenga mtambo wa kufua umeme wa
megawati 100 wa Tegeta.
Kwa
mujibu wa makubaliano hayo, SCB-HK ilipewa kandarasi kadhaa ikiwamo
haki ya kulipwa deni la 1997, ambako mkataba wa utekelezaji na hatia ya
makubaliano ya dhamana iliyosainiwa kati ya IPTL na Serikali.
Fedha zilivyotolewa
Akaunti
ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuhifadhi
fedha za malipo ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye
mgogoro na Kampuni ya IPTL na suala hilo lilipelekwa mahakamani.
Kwa
mujibu wa masharti ya uendeshaji wa akaunti ya Escrow, fedha zilitakiwa
zitolewe baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo, lakini wakati
ilitaka pande hizo mbili zikutane na kukokotoa viwango vya tozo, fedha
hizo zilitolewa na kulipwa mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power
Solution (PAP) jambo lililosababisha kuibuka kashfa hiyo.
Ilivyotua bungeni
Aliyekuwa
wa kwanza kulifikisha bungeni suala hilo ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila, ambaye aliwalipua baadhi ya mawaziri wa Serikali
ya awamu ya nne kuhusika na mpango huo.
Hatua hiyo ilisababisha Spika wa Bunge la 10 kuagiza uchunguzi wa vyombo vya dola kuweza kuchimbua kwa undani wizi huo.
Baada
ya kukamilika ilikabidhiwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAP)
chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake Zitto Kabwe na Makamu wake, marehemu
Deo Filikunjombe.
Novemba
28 mwaka 2014, Bunge la 10 lilitoa maazimio manane kuhusu suala hilo
huku Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira wa (VIP), aliyekuwa Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme wa Umeme Tanzania
(TANESCO) walionekana kuhusika kwa namna moja au nyingine katika
kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya
Tegeta kwenda Pan African Power Solutions Ltd (PAP) na VIP.
Bunge
pia liliazimia mawaziri wa wakati huo wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa kati huo, Eliachim Maswi
na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri
mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Mawaziri
hao walipoteza nyadhifa zao huku Profesa Muhongo akijiuzulu na
Tibaijuka uteuzi wake ukifutwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Credit: Mtanzania