WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameliegiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya
Wilaya ya Kibaha lifanye maamuzi ya kupima ardhi haraka na kutenga
maeneo kwa ajili makazi na viwanda ili kujiandaa na uwekezaji mkubwa.
Ametoa
agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Novemba 19, 2016) wakati akizungumza
na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani mara
baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta
cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani
Pwani.
“Jiji
la Dar es Salaam limejaa, na Kibaha mjini pia hawana ardhi ya kutosha
kwa kimbilio pekee hivi sasa ni Kibaha Vijijini. Baraza la Madiwani
fanyeni maamuzi, pimeni ardhi na mtenge maeneo ya makazi, viwanda na
taasisi za elimu ili mkipata wawekezaji iwe rahisi kuwapa maeneo,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi kwa taasisi
nyingi na halmashauri nyingi nchini kwani zilikuwa zinashindwa kumudu
bei ya kununua magari ya zimamoto.
“Baadhi
ya Halmashauri nyingi zilikuwa zinanunua gari moja kwa sh. milioni 500
na hiki ni kiasi kikubwa mno kwa hiyo kiwanda hiki kitakuwa mkombozi kwa
taasisi nyingi na halmashauri zetu,” alisema.
Alisema maeneo mengi nchini yanahitaji magari ya zimamoto lakini yalikuwa yanashndwa kumudu bei za magari hayo.
Aliyataja
maeneo hayo kuwa ni viwanja vya ndege, bandari, taasisi zilizo chini ya
TAMISEMI kama vile shule za sekondari za bweni, Majiji, miji mikuu,
Manispaa na Halmashauri za Wilaya.
Alisema
ameguswa kukuta kiwanda hicho pia kina uwezo wa kutengeneza matreka na
zana za kilimo (farm implements) kwani asilimia kubwa ya Watanzania ni
wakulima na wanategemea jembe la mkono.
“Kupitia kiwanda hiki, matrekta mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu.”
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini
alimweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho
imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenhye hatua ya kufunga mitambo.
Hata hivyo, alisema wanaisubiri iwasili kutoka India.
Alisema
kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000 kwa
mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha
magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya
nchi.
“Tukiweza
kuzalisha vipuri hapa nchini kwa asilimia 60, umiliki wa magari haya na
matrekta utakuwa ni wa Tanzania na siyo wa kampuni za nje tena. Pia
tutakuwa tumefaulu kuhamisha teknolojia kwa vijana wetu,” alisema.
Alisema hadi sasa vijana 60 wamekwishapatiwa mafunzo na wako tayari kuanza kazi mara uzalishaji utakapoanza Machi, 2017.
Kuhusu
teknolojia ya utengenezaji wa magari ya zimamoto, Eng. Mangazini
alisema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika cha kwanza
kikiwa huko Bassa, Afrika Kusini.
Mapema,
akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, mwakilishi wa Equator SUMA JKT
Ltd. Kapteni Farijala Mkojera alisema kiwanda hicho kinamilikiwa kwa
pamoja na kampuni ya Equator Automech Ltd ambao wana hisa asimilia 70 na
SUMA JKT inamiliki asilimia 30 ya hisa za kiwanda hicho.
Akizungumzia
ujenzi wa kiwanda hicho, alisema hadi sasa wamekwishatumia sh. bilioni
1.5 na kwamba hadi ujenzi utakapokamilika, wanatajia kuwa wametumia sh.
bilioni mbili. “Ujenzi ukikamilika, tunatarajia kuajiri wafanyakazi 200 katika fani mbalimbali,” alisema.
Alisema
wakianza uzalishaji, mbali ya magari ya zimamoto na matrekta, wataweza
pia kuunganisha mabasi na zana za kilimo kama vile combine harvesters.
“Tutakuwa
tumefanikiwa kuhamisha teknolojia kutoka Russia (magari za zimamoto) na
India na Poland (matrekta). Tuna uhakika wa soko hapa nchini katika
Jumuiaya za EAC na SADC,” alisema.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma mchana huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU