Fatma Karume, mtoto wa rais wa zamani wa Zanzibar, ameshangazwa na
kitendo cha Profesa Ibrahim Lipumba kutaka kurudi kwenye nafasi yake ya
awali ya uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wakati alijiuzulu
mwenyewe.
Fatma, mtoto wa Amani Abeid Karume ambaye ni rais wa sita wa Zanzibar,
alisema hayo alipoulizwa kuhusu hali iliyoukumba uongozi kwenye chama
hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar baada ya tamko la Msajili wa
Vyama vya Siasa kuwa, anamtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali
wa CUF.
Msajili huyo, Jaji Francis Mutungi alitoa uamuzi huo baada ya kuziita
pande zinazosigana kwenye mgogoro, kusikiliza hoja zao baadaye kutoa
maoni na msimamo wa ofisi yake kuwa Profesa Lipumba alifuta uamuzi wake
kwa maandishi kabla ya mkutano mkuu wa CUF haujajadili barua yake ya
kujiuzulu, hivyo anaendelea kuwa mwenyekiti halali.
“Profesa Lipumba alijiuzulu mwenyewe. Aliandika barua akaipeleka kwa
katibu mkuu, kisha akautangazia umma na dunia nzima ikafahamu kwamba
siyo tena mwenyekiti wa CUF,” alisema.
