MKOA
wa Dodoma wakishirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA)
wametekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuandaa na
kuwasilisha mapendekezo ya awali ya namna serikali itakavyohamia Dodoma.
Aidha, imeelezwa kuwa kuanzia sasa Waziri Mkuu ataweka hadharani maelekezo ya wizara na watumishi kuhamia Dodoma.
Hayo yamebainishwa katika mahojiano yaliyofanyika jana na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge.
Mwishoni
mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa
serikali, taasisi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Dodoma alielezea
azma ya serikali kuhamia Dodoma na kutoa siku 14 kwa Mkoa na CDA,
kuwasilisha mapendekezo ya awali kwa namna serikali itakavyohamia
Dodoma.
Akitoa
siku hizo kwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake,
hususani CDA kuandaa na kutoa mpango kazi wake, Majaliwa alisema,
“Ndani ya siku 14 nipate proposal (mapendekezo) ya kwanza namna
mtakavyotekeleza, naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu
kitakachowajumuisha makundi yote. Baada ya siku 14 nipate mpango wenu.”
Madenge
alisema kwamba Mkuu wa Mkoa huo, Jordan Rugimbana yuko Dar es Salaam
alitarajiwa kuwasilisha mpango kazi huo kwa Waziri Mkuu na kwamba muda
wowote Waziri Mkuu atatangaza utaratibu wa kuhamia Dodoma.
“Tumeandaa mpango kazi kulingana na maelekezo ya waziri mkuu na mkuu wa mkoa amekwenda kukabidhi mpango huo,” alisema Katibu Tawala Dodoma.
Akizungumzia
taarifa za baadhi ya wizara kuanza kuhamia huko, Katibu tawala huyo
alisema kwamba kama mkoa hawana taarifa za wizara na watumishi kuanza
kuhamia Dodoma.
“Tunasubiri maelekezo ya waziri mkuu, baada ya mpango kazi kukamilika utawekwa hadharani mambo yote ya serikali kuhamia Dodoma,” alisema Madenge.
Akifafanua
zaidi, alisema anachojua yeye mpango unakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu
na na wizara zitajipanga kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu
Majaliwa.
Mkoa
wa Dodoma umekuwa katika hekaheka za kutekeleza maagizo ya serikali ya
kuhamia Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma muhimu kama
upatikanaji wa viwanja zinakwenda kwa taratibu zinazotakiwa.
Ili
kuondoa mhemko na udalali wa viwanja unaoweza kupandisha bei na pia
kuzuia vurugu, mkuu wa mkoa amepiga marufuku uuzaji wa viwanja ndani ya
mji wa Dodoma. Sababu kubwa ya kupiga marufuku kunatokana na kundi la
madalali kutoka mikoa mbalimbali kuvamia mji.
Kupokewa
kwa mpango kazi huo ni moja ya hatua za kukamilisha uhamiaji wa
serikali Dodoma, ambapo hatua nyingine ni kwa serikali kuwasilisha
bungeni muswada wa kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili
uthibitishwe kisheria.
Muswada huo utawasilishwa katika Bunge linaloanza Septemba 6, mwaka huu.
Waziri
Mkuu Majaliwa alisema muswada huo wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma,
utapelekwa bungeni ili azma ya Rais John Magufuli na serikali yake uwe
na nguvu kisheria, baada ya Rais Magufuli kutangaza hivi karibuni kuwa
ndani ya miaka minne na ushee iliyobaki ya kumaliza muhula wake wa
kwanza wa urais, Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa imehamia katika mji
wa Dodoma, ambao mwaka 1973 ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania.