Jijini Mwanza Rais Magufuli alipokelewa
na maelfu ya wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake tangu
alipoingia kupitia kivuko cha Busisi - Kigongo na baadaye kupita
Usagara, Buhongwa, Mkolani, Nyegezi, Mkuyuni na Igogo ambako pamoja na
kuwahakikishia kuwa Serikali yake imejipanga kukabiliana na kero
mbalimbali za wananchi na kuwaletea maendeleo, amesitisha agizo la Jiji
la Mwanza la kuwataka wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la
Machinga kutofanya biashara zao katikati ya Jiji ifikapo tarehe 20
Agosti, 2016.
Pamoja
na kusitisha agizo hilo, Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Jiji la
Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutafuta na kuandaa maeneo
ambayo wafanyabiashara hao watayatumia kwa ajili ya kufanyia biashara
zao.
"Na
mtakapowatafutia maeneo ya biashara wapelekeni sehemu ambazo ni nzuri,
msiwapeleke sehemu ambazo hazina biashara, hawa wamachinga wanaendesha
maisha yao kwa kutumia biashara hizi" Amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mwanza kuwa Serikali imeanza
kufanya usanifu na upembuzi yakinifu ikiwa ni maandalizi ya kuanza
ujenzi wa daraja kubwa litakalounganisha eneo la Busisi Wilayani
Sengerema na Kigongo Wilayani Misungwi ili kuondoa adha ya wananchi
kuvuka eneo hilo kwa kutegemea vivuko, na pia itahakikisha inanunua meli
moja katika ziwa viktoria kama ilivyoahidi.
Kabla ya kuingia Jijini Mwanza Rais Magufuli alihutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Sengerema na pia alizungumza na wananchi wa Sima Wilayani Sengerema na Kasamwa Wilayani Geita ambako aliwahakikishia
kuwa Serikali yake itaongeza msukumo katika kutatua tatizo la uhaba wa
maji katika maeneo hayo kwa kusambaza maji ya kutoka ziwa Viktoria huku
akiwataka viongozi halmashauri husika kutumia rasilimali za halmashauri
kutatua tatizo hilo la maji katika maeneo ambayo hayatapitiwa na mradi
mkubwa wa maji ya kutoka ziwa Viktoria.
Katika
hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa ya
Mwanza na Geita kutafakari sababu zilizosababisha kufa kwa Chama Kikuu
cha Ushirika cha NYANZA na viwanda vya kuchambua pamba (Ginneries) ili
kupanga namna ya kuvifufua.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo
alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasamwa kilichopo
Wilayani Geita na ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kuunga mkono
juhudi za wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao
yao ikiwemo zao la pamba.
Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya siku mbili leo tarehe
11 Agosti, 2016 kwa kuweka jiwe la msingi katika Daraja la watembea kwa
miguu na kuzungumza na wananchi wa Mwanza katika Uwanja wa Furahisha.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
10 Agosti, 2016