MABASI yanayosafirisha abiria wanaokwenda mikoani yaliyofungiwa na Serikali kwa kusababisha ajali yameanza kuruhusiwa kutoa huduma hiyo.
Mabasi hayo yameruhusiwa baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (SUMATRA) na Wamiliki wa Mabasi ya Abiria (TABOA) kufikia muafaka.
Makubaliano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita yalilenga kuleta suluhu kwa kuwataka TABOA kusimamisha mgomo wa mabasi uliopangwa kufanyika nchi nzima Agosti 22 mwaka huu.
Zaidi ya mabasi 60 ya kampuni tofauti yalifungiwa na Serikali baada ya kile kilichodaiwa na serikali kwamba yalisababisha ajali kwa uzembe wao.
Wamiliki wa mabasi hayo walikuwa wanahoji sababu ya SUMATRA kufungiwa leseni ya usafirishaji kwa kampuni badala ya kupewa adhabu basi moja lililopata ajali badala ya kufungiwa kampuni nzima.
Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu jana alisema wamekubaliana mabasi ambayo ni mazima yaliyofungiwa yaachiwe kutegemeana na utaratibu wa ukaguzi yaweze kuingia barabarani kutoa huduma ya usafirishaji.
“Tulikubaliana na serikali ndani ya siku saba iwe imeyafungulia mabasi yetu mazima kutegemeana na utaratibu wa ukaguzi yaendelee kutoa huduma kwa wananchi na tayari serikali imeanza kuyaachia baadhi ya mabasi hayo,
“Baadhi ya mabasi yaliyofungiwa ambayo yameachiwa kutoa huduma ni ya Mohammed Trans, Mbazi, Kisbo Safari, City Boy, KVC, Wibonera na Kandahari”, alisema Mrutu.
Alisema walikubaliana serikali iyakamate mabasi yote madogo nchini yanayofanya safari za usafirishaji abiria mikoani bila ya kuwa na leseni ya biashara hiyo.
Alisema mabasi hayo yamekuwa kero kubwa kwa kugombania abiria na yanapokuwa barabarani yanawachomekea madereva wa mabasi makubwa.
Pia aliomba idadi ya vituo vya polisi vya ukaguzi barabarani vipungue.