Na: Abushehe Nondo - MAELEZO
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonyani
amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi na kumlipa fidia ya shilingi
bilioni moja kutokana na kuandika habari ya kumchafua.
Akizungumza
na waandishi wa habari Ofisi kwake Waziri Ngonyani amesema kuwa Gazeti
hilo la tarehe 4 Agosti 2016 liliandika habari yenye kichwa cha Habari
“Waziri amchafua JPM” ikimuhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya
Kampuni ya Madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la
Taifa (Stamico).
“Nimewaandikia
notisi ya siku saba ikiwataka waombe radhi na kunilipa fidia, na
wasipofanya hivyo hatua stahiki kuwapeleka mahakamani akiwemo Mwandishi
Josephat Isango, Mwanahalishi Publisher na Mchapaji wa gazeti hilo”. Alisema Mhandisi Ngonyani.
Mhandisi
Ngonyani amesema kuwa habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia
nyaraka za kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa tarehe 24 Julai na
kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO wakati ukweli ni
kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili na siyo Kaimu kama
barua hiyo inavyosomeka.
Ameongeza
kuwa habari hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga
kura wake wa jimbo la Namtumbo ambao walijitoa katika kumsaidia wakati
wa kampeni na hali kadhalika zimemchafua Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa
kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama.
“Mheshimiwa
Rais Dkt. Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote
aliyechangia kuingia kwake ikulu ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo,
Iweje leo mtu tu anaibuka na kuandika habari za kugushi? ”. Aliongeza.
Aidha
Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari
nchini kuwa waangalifu pindi wanapoandika habari za kutunga kwa
kutotumia majina halisi kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni
za uandishi wa hadithi (Habari za kutunga).
“Waandishi
wa habari mnatakiwa kufuata maadili ya kazi yenu kwa kuandika habari
zenye ukweli ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko na migogoro
isiyo ya lazima” Alisema Naibu waziri huyo.