Serikali
imehitimisha ubia kati ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na Kampuni
ya Bhart Airtel ya India kwa kuilipa kampuni hiyo Shilingi Bilioni 14.9
na hivyo kuirudisha TTCL mikononi mwa Serikali kwa asilimia miamoja.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hatua
hiyo ni mkakati wa Serikali wa kuiwezesha TTCL kujitegemea ili
kuzalisha faida, Kuimarisha Miundombinu yake, na kutoa gawio Serikalini......
“Tunawataka TTCL mjipange vizuri mjitangaze ili muwe kampuni kubwa na bora ya mawasiliano hapa nchini”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
Prof. Mbarawa amesema katika kuiongezea nguvu TTCL Serikali itawapa
kituo cha Kutunza Taarifa cha Kijitonyama (Internet Data Center) ili
ikisimamie na hivyo kujipatia mapato kupitia gharama za uendeshaji na
usimamizi wa kituo hicho.
Amewataka
wafanyakazi wa TTCL kufanya kazi kwa bidii, kasi, uaminifu, ubunifu na
kuulinda Mkongo wa Taifa ili uwawezeshe kuwa na huduma bora na za
uhakika wakati wote.
“Tumetumia
fedha za mkongo wa taifa kumlipa mbia mwenzenu bhart airtel ili
kuiwezesha TTCL kumilikiwa na Serikali kwa asilimia miamoja hivyo
changamoto inayowakabili sasa ni kufanya mabadiliko makubwa katika
upande wa kutafuta masoko ili kuweza kuongeza idadi ya wateja na kufanya
kazi kwa faida”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha
Prof Mbarawa amesema katika kuijali TTCL, Serikali imeipa masafa ya
1800 na masafa ya 2100 na itawaongezea masafa ya 800 yatakayowawezesha
kuwa na huduma ya 4G LTE yenye mtandao wenye kasi na hivyo kuiongezea
wateja hususani katika huduma za data.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete amesema
TTCL imejipanga kutoa huduma zake katika maduka makubwa, hospitali,
stesheni za treni, mabasi ya mwendokasi na viwanja vya ndege katika jiji
la Dar es salaam na Miji mikubwa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na
huduma za mtandao na data wakati wote.
Naye,
Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura, ameishukuru Serikali kwa
fursa mbalimbali inazoipa kampuni hiyo na kumhakikishia Waziri Prof
Mbarawa kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo matokeo ya mkakati wa
mabadiliko ya kibiashara yataanza kuonekana.
Dkt.
Kazaura amesema kuwa tayari watumishi wenye mtazamo wa mabadiliko ya
kiteknolojia wameajiriwa na wengine watapewa mafunzo ili kuhimili soko
la kibiashara na kuiwezesha TTCL kunufaika na miundombinu yake iliyopo
nchi nzima.
Waziri
Prof. Mbarawa alikuwa akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL
ikiwa ni utaratibu aliojiwekea kuzungumza na wafanyakazi na taasisi
zilizopo chini ya Wizara yake.