Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema
amepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha
mwanasiasa mkongwe katika siasa za mageuzi nchini, Mwenyekiti wa DP
Mchungaji Christopher Mtikila.
Katika
salaam zake za pole kwa familia ya Mchungaji Mtikila, Katibu Mkuu wa
DP, viongozi na wanachama wa chama hicho kwa ujumla, Mwenyekiti Mbowe
amesema kuwa kifo cha Mchungaji Mtikila kimeacha pengo kubwa katika
siasa za mageuzi nchini hasa katika kupigania Tanganyika na suala la
mgombea huru kuwa haki ya kikatiba nchini.
“Mwenyekiti
wa DP Mtikila atakumbukwa kwa msimamo wake usioyumba katika mambo
makubwa mawili, kwanza kwa msimamo wake wa kuipigania Tanganyika kwa
muda mrefu bila kuchoka akitumia kila njia na majukwaa mbalimbali
kujenga hoja za kudai Tanganyika.
“Suala
jingine ambalo nalo pia alilipigania kwa ujasiri kisiasa na kisheria
lilikuwa ni agenda ya mgombea huru ili iwe mojawapo ya haki za msingi
zinazotambulika katika katiba yetu ya nchi.
“Ni
jambo la kusikitisha sana Mchungaji Mtikila ameaga dunia bila kuona
mambo hayo makubwa mawili yakitimia akingali hai. Ni imani yangu kuwa
kizazi cha sasa ambacho kinapigania mabadiliko katika nchi yetu hasa
kupitia uchaguzi huu, kitajifunza mengi kutoka kwa kiongozi huyo wa
kisiasa na kuyaenzi yale yote mazuri aliyoyapigania kuhakikisha
yanatimia kwa manufaa ya watanzania,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;
“Kwa
masikitiko na majonzi makubwa natoa pole kwa familia ya marehemu,
ndugu, jamaa na marafiki kwa kumpoteza mpendwa wao na moja ya guzo
muhimu katika maisha. Mwenyezi Mungu awasimamie na kuwatia nguvu katika
wakati huu mgumu wa majonzi katika kuukabili ukweli wa msiba huo mkubwa
katika familia.
“Kwa
niaba ya viongozi wenzangu wa CHADEMA, wapenzi, wafuasi, mashabiki na
wanachama wote kwa ujumla, pia natoa pole na salaam za rambirambi kwa
Katibu Mkuu wa DP kwa niaba ya viongozi na wanachama wa chama hicho kwa
kuondokewa na kiongozi wao mkuu,” amesema Mwenyekiti Mbowe katika salaam zake.
0 comments:
Chapisha Maoni