test

Jumamosi, 12 Septemba 2015

BREAKING NEWS: Sheria ya Makosa ya Mitandao yapingwa mahakamani




Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu THRDC pamoja na kituo cha haki za binaadamu LHRC wameamua kufungua kesi kupitia wakili Jebra Kambole kupinga baadhi ya vipengele kwenye sheria ya makosa ya mtandao mpaka pale vitakapofanyiwa marekebisho.

Vipengele vinavyopigwa ni kifungu cha 4, 5 na 45 (4) cha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ambacho kinazuia haki ya kupata na kutoa taarifa ambacho kinakinzana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania.

Vipengele vingine ni Kifungu cha 6, 7, 8, 10, 11, 14, 19, 21 na 22 ambavyo vina maneno yasiyo na tafsiri na kuweza kusababisha tafsiri mbaya kwa watekeleza sheria na hivyo kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu ambavyo vinakiuka Ibara ya 17 ya Katiba.

Vifungu vya 31,33,34,35 na 37 vya sheria hiyo vinatoa mamlaka kwa Polisi kufanya upekuzi  bila idhini ya Mahakama hivyo ni uvunjufu wa haki za binadamu na inakinzana na Ibara ya 16 ya Katiba.

Vipengele vingine, Kifungu cha 38 cha sheria hiyo kinanyima haki ya mtu kusikilizwa na Mahakama huvyo inakinzana na Ibara ya 13 (6) ya Katiba pamoja na kifungu cha 47 (1) cha sheria hiyo kinanyima Polisi kufanya kazi zao kama ilivyo katika Sheria hii.

Hatua hiyo ya kufungua kesi imekuja baada ya Aprili mwaka huu Bunge kupitisha sheria ya makosa ya mitandaoni (Cybercrime Act 2015) ambapo watetezi wa haki za binadamu hapa nchini kwa kushirikiana na mashirika ya Kimataifa yalifanya uchambuzi na kubaini kuwa baadhi ya vipengele katika sheria hiyo vilikuwa na mapungufu makubwa.

Akizungumza jana  na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam nje ya Mahakama Kuu, Mkurugenzi wa  THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uchumbuzi uliofanyika ulibaini kuwa sheria iliyopitishwa ni mwiba kwa uhuru wa vyombo vya habari, haki ya falagha na haki ya watu kupata taarifa  na kutoa maoni.

Olengurumwa alidai, baada ya wadau hao kuyagundua makosa hayo ambayo yalikuwa yanafinya haki za binadamu waliamua kutoa maoni  ambayo serikali iliahidi kuyafanyia marekebisho. Lakini licha ya sheria hizo kufanyiwa marekebisho bado kunavipengele ambavyo vinamakosa.

Ndani ya sheria hizo waligundua kuwa endapo sheria hiyo itaendelea kutumika itakuwa imekiuka haki za binadamu kama, Uhuru wa habari, uhuru wa maoni, uhuru wa kutafuta habari, Haki ya faragha, Haki ya kuifikia Mahakama na Haki ya kusikilizwa.

Anasema Mei 22 mwaka huu Serikali ilitangaza kutumika sheria ya makosa mitandaoni pasipo kufanyiwa marekebisho ambayo yalipendekezwa na wadau wa haki za binadamu.

“Ikumbukwe kuwa kabla ya sheria hiyo kupitishwa Mashirika yasiyopungua 55 mwaka huu chini ya uratibu wa THRDC yalimwandikia barua Rais Kikwete ya kumsihi asitie saini kabla ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho lakini pia ilipuuzwa”. anasema Olengurumwa.

Aidha alisema, kutokana kwamba sheria hiyo imeanza kutumika THRDC pamoja na mashirika mbalimbali ya Haki za Binadamu wakiungana na jopo la wanasheria saba tumeamua kumuunga mkono na kufungua kesi kupitia wakili wa kujitegemea Jebra Kambole ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo katika kuhakikisha kuwa baadhi ya vipengele katika sheria hiyo vinapigwa.

“Ikumbukwe kuwa taratibu za kisheria  zinapendelea zaidi kesi kama hizi zifungukuwe na mtu binafsi na si shirika hivyo tunamuunga mkono hadi  mwisho. Na endapo Mahakama itashidwa kutenda haki katika kesi hii basi tutaipeleka mbele zaidi katika Mahakama ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata utatuzi,” anasema Kambole.

Jopo la Mawakili hao saba ni, John Seka, Massawe Fulgence, Harold Sungusia, Benedict Ishabakakaki, Jebra Kambole (wakili wa kujitegemea), Boka Iyamuya, Neema Ndemno na Geremia Mtobesia ambapo kesi imepewa jarada la Miscellaneous Civil Case namba 32 ya mwaka 2015.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni