MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa adhabu ya faini kwa vituo vitatu vya televisheni nchini kwa kuonyesha vipindi vilivyokiuka kanuni za huduma ya utangazaji (maudhui ) ya mwaka2005.
Uamuzi
huo ulitolewa jijini Dar es salaam jana na kamati ya Maudhui ya TCRA
chini ya mwenyekiti wake Mhandisi Margaret Munyagi ambapo alivitaja
vituo hivyo kuwa ni Channel Ten, Star TV na TBC1.
Munyagi
alisema ushahidi ulionyesha kuwa vituo hivyo kwa nyakati tofauti na
katika vipindi tofauti walikiuka kanuni za Huduma ya utangazaji .
Akizungumzia
Kituo cha Channel Ten alisema kimepewa onyo kali na kutakiwa kulipa
faini ya Sh Milioni 2.5, kwa kukiuka kanuni kwa makosa mawili Mei 30
mwaka huu kupitia kipindi cha Kanjanja Time kilichorushwa hewani kuanzia
2:45 hadi 3:10 usiku ambapo walionyesha picha ya mgonjwa akiwa katika
wodi ya Hospitali ya Serikali mjini Songea huku sehemu ya makalio yake
yakiwa wazi na kuonyesha vidonda.
Alisema taarifa hiyo ilirudiwa mara kadhaa huku watangazaji
wakisikika wakishabikia uchochezi dhidi ya serikali kwamba madaktari wafukuzwe na hospitali ifungwe
“Kipindi
hicho pia kilionyesha taarifa ya walemavu wawili wakipigana hadharani
huku watangazaji wa kipindi wakishangilia kitendo hicho na kufananisha
na pambano la ngumi za kulipwa” alisema Munyagi.
Alisema
kituo hicho kimekiuka kanuni namba 5(c), (h), 9(1), 18(1), (b), (i),
(ii) za huduma ya utangazaji ya 2005 zinazotaka kituo kuhakikisha
kinazingatia ubora wa vipindi pamoja na staha, ambavyo havileti
uchochezi wala kujenga chuki katika jamii, kutokungilia masuala
binafsi, na kutochochea vurugu na ukatili.
Kwa
upande wa kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), Munyagi alisema
kimetakiwa kutoa faini ya Sh 500,000 kukiuka kanuni za huduma ya
utangazaji (maudhui) 2005 namba 9(2) na 9(3) katika kipindi cha Taarifa
ya Habari, Machi 21 mwaka huu kwa kuonyesha utambulisho wa mtoto
aliyelawitiwa.
“Taarifa
hiyo ilionyesha utambulisho wa picha na majina ya wazazi wa mtoto, eneo
analoishi, nyumba , shule anayosoma na sehemu ya mwili wa mtoto wakati
akiwa anatembea jambo ambalo ni ukiukwaji wa kanuni za huduma za
utangazaji” alisema Munyagi.
Alisema
Kituo cha Star TV nacho kimetakiwa kutoa faini ya Sh 500,000, kwa
kukiuka kanuni za huduma za utangazaji 2005 namba 5(c), 5(g), 14(1),
16(3), 26(1) na 26(2) katika kipindi cha Min Buzz kilichorushwa hewani
Juni 3 mwaka huu saa 12:30 jioni hadi 1:00 usiku na kujadili mada
inayohusu ubakaji katika ndoa wakati ambao watoto pia hupata fursa ya
kuangalia na kusikiliza.
Alisema
vituo vyote vinatakiwa kulipa faini hizo ndani ya siku 30 na pia
vinahaki ya kukata rufaa dhidi ya uamu huo ambapo ni ndani ya siku 30
tangu uamuzi ulipotolewa.
0 comments:
Chapisha Maoni