test

Jumanne, 16 Juni 2015

Magereza yaaswa kuruhusu wafungwa kujiandikisha BVR>>>




JESHI la Magereza nchini limeshauriwa kuhakikisha wanaruhusu wafungwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa kielektroniki (BVR), unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Hatua hiyo ni kuwawezesha kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi katika uchaguzi ujao.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mratibu wa marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Noel Nnko wakati walipotembelea Gereza la Wilaya ya Same na kutoa misaada mbalimbali kwa wafungwa ikiwemo utoaji wa elimu ya kujiandikisha.

Nnko alisema licha ya kutolewa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura makundi mbalimbali katika jamii yamekuwa yakisahaulika ikiwemo wafungwa waliopo magerezani katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo ni vema viongozi wa Jeshi la Magereza nchi wakatupia macho suala hilo kwa kuhakikisha wafungwa wanaoruhusiwa kujiandikisha katika daftari hilo wanapata haki hiyo kwa mujibu wa sheria.

“Tumepitia sheria tumejiridhisha kuwa wafungwa wasioruhusiwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na kupiga kura ni wafungwa waliohukumiwa vifungo vya maisha na kifo.

“Hivyo natoa rai yangu kwa viongozi wa magereza kutenda haki kwa wafungwa wengine kwani kundi hili limekuwa halipewi kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kijamii,” alisema Nnko.

Katika hatua nyingine, Nnko aliwataka wafungwa hao kuacha tabia ya kushabikia viongozi wa kisiasa bali kujiandikisha katika daftari hilo hatua ambayo itawawezesha kupata viongozi bora kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.

“Pamoja na kwamba kila mtu ana haki ya kumshabikia mgombea yeyote mnawajibu wa kuhakikisha mnaacha kuonyesha hisia zenu ili mchague kiongozi ambaye anaweza kutatua changamoto zinazokabili taifa kwa sasa,” alisema Nnko

Nao baadhi ya wafungwa katika gereza hilo, wameitaka NEC kusimamia zoezi la uchaguzi mkuu kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria jambo ambalo litasaidia kuliweka taifa katika hali ya utulivu na amani.

Walisema hali ya utulivu na amani katika kipindi cha uchaguzi ipo mikononi mwa tume hiyo hivyo ni vema ikatenda haki kwa wagombea hali ambayo itaepusha vurugu na mapigano ambayo yanaweza kutokea kutokana na upungufu ambao unaweza kujitokeza katika zoezi hilo.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni