test

Jumatano, 27 Mei 2015

Madereva Bado Hakijaeleweka......Mgomo Mwingine Wanukia




UMOJA wa Madereva umeilalamikia Kamati ya Waziri Mkuu iliyoundwa kutatua hoja za madai yao kwa kile walichodai inajadili malalamiko ya wamiliki badala ya hoja zao kama ilivyoagizwa.
 
 Akizungumza Katibu Mkuu wa Madereva Tanzania, Rashid Salehe, alisema kuwa tangu kuundwa kwa kamati hiyo kwa ajili ya kujadili hoja za madereva ni kikao kimoja ndicho kilichojadili hoja moja tu ya namna ya kuboresha mikataba ya awali ya wamiliki waliokuwa wakiitumia pindi walipokuwa wakitaka kuchukua lessen kutoka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
 
Alisema kati ya vikao vitatu walivyokaa na kamati hiyo vikao viwili vyote vilikuwa vikijadili malalamiko ya wamiliki ambayo walikuwa wakilalamikia kutozwa malipo kwa dola kwenye mizani, ubovu wa barabara,  faini za barabarani, kuuziwa vipuri feki ikiwa ni pamoja na kulilalamikia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutokuwa makini na kazi yao hali inayosababisha kuingia kwa matairi yasiyokuwa na viwango.
 
Alisema mpaka sasa hawaoni dalili ya kutatuliwa hoja za madai yao na badala yake kinachofanyika ni danganya toto huku madereva wakiendelea kufanya kazi katika mazingira yale yale magumu bila ya kuwa na mikataba ya ajira.
 
“Madereva wenzetu wametutuma ili tukawawakilishe kwenye vikao lakini mpaka leo kwa vikao vitatu tulivyokutana Mei 12 na mei 19 na kingine mei 21 hatujaona chochote cha kueleweka na badala yake wanajadili malalamiko ya wamiliki wakati hoja za madai yetu ndizo zilizosababisha kuundwa kwa kamati hiyo.
 
“Kama wamiliki wana malalamiko yao wasubiri kwanza tumaliziwe sisi ambao ndio tulioanza kulalamika alafu ndio watoe ya kwao kwani madereva tumechoka kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kama hayo,” alisema Salehe.
 
Alisema baada ya kikao cha Mei 21 kamati hiyo iliahidi kukutana nao katika kingine mwezi mmoja badae  ambao hawajui kitakachoendelea kujadiliwa kama ni hoja za madai yao au ni malalamiko ya wamiliki.
 
Alisema kutokana na hali hiyo wanatarajia kukutana na madereva wote Juni 7 jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuwapa mrejesho wa vikao vyote walivyokaa na kamati hiyo na kwamba baada ya majadiriano ndipo watakapotoa maamuzi.
 
Aliongeza kuwa wameshapeleka taarifa za malalamiko yao juu ya kamati hiyo ya waziri mkuu kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda kutokana na kuwa yeye ndiye aliyekubali kubeba hoja za madai yao siku ya mkutano uliofanyika siku ile ya mgomo wa pili.
 
April 19 madereva walifanya mgomo wao wa kwanza kwa masaa saba kabla ya kufanya mgomo mwingine uliodumu kwa siku nne wakiishinikiza serikali kutatua hoja za madai yao ya siku nyingi ikiwa ni pamoja na kupinga kurudi shule kila baada ya miaka mitatu pindi wanapotakiwa kurejesha leseni zao.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni