Baadhi
ya wazazi katika shule ya Msingi St. Florence iliyoko Mikocheni, jijini
Dar es Salaam, wameanza kuhamisha watoto wao baada ya taarifa za
mwalimu wa shule hiyo anayetambuliwa kwa jina la Ayoub Mlugu kudaiwa
kuwadhalilisha watoto wanne wa darasa la saba katika shule hiyo.
Wazazi hao ambao (majina yanahifadhiwa) wamesema kitendo hicho kimewatisha na kusababisha hofu juu ya usalama wa watoto hao.
“Tulipopata
taarifa za kubakwa kwa baadhi ya wanafunzi tumeogopa sana, mimi
mwanangu yuko darasa la saba na kitendo hicho kimefanywa kwa wanafunzi
wa darasa la saba, nimeogopa, nimeamua kuchukua uhamisho niwapeleke
shule nyingine,” amesema mzazi huyo.
Naye
mzazi mwingine ambaye mwanawe anasoma darasa la nne amesema kitendo
kilichofanywa na mwalimu huyo ni kibaya na kwamba serikali inabidi
ifuatilie na kuwachukulia hatua wahusika.
“Tumeshangaa
kusikia mwalimu amekimbia wakati uongozi wa shule unajua suala hili
wiki mbili zilizopita, siwezi kumuacha mwanangu, namhamisha,” amesema.
Wakati
huo huo, Diwani wa Kata ya Mikocheni Venus Kimei amefika kwenye shule
hiyo baada ya kupata taarifa za kubakwa kwa watoto hao ambapo amesema
anasubiri kikao cha maofisa wa polisi na uongozi wa shule ili kujua
kinachoendelea kuhusu suala hilo.
Amesema
kama mzazi hawezi kuvumilia suala hilo kwa sababu ni kinyume na maadili
lakini pia linadhalilisha watoto na kuwaumiza kisaikolojia.
“Nasubiri
nipate taarifa za ndani kuhusu suala hilo ili nijue kinachoendelea
ikiwamo kushirikiana na jeshi la polisi kwa ajili ya kuchukua hatua
stahiki za kisheria kwa mhusika aliyefanya kosa hilo,” amesema.
0 comments:
Chapisha Maoni