Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali
ilizindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ili kuhakikisha
wakopaji wakiwemo wajasiriamali wadogo wanalindwa na kupata haki zao
bila kudhurumiwa wanapo hitaji mikopo na huduma zingine za kifedha
zitakazowasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge Mhe.
Khatibu Said Haji aliyetaka kujua hatua za Serikali kuhusu taasisi za
huduma ndogo za kifedha (Microfinance) kuwatoza wananchi riba kubwa
wanapochukua mikopo.
Dkt.
Kijaji, alisema kuwa mwezi Desemba, 2017 Serikali ilizindua sera ya
huduma ndogo ya fedha itakayosaidia kuwatambua wakopeshaji na
kuwalinda wakopaji wanaohitaji huduma katika taasisi hizo zikiwemo za
mikopo.
“Tunataka
kuhakikisha tunawalinda wakopaji na kuhakikisha wanakopa kwa kuzingatia
sheria na taasisi hizo za fedha zinazingatia sheria, utaratibu na
kanuni za utawala bora”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
kukamilika kwa sheria ya huduma ndogo ya fedha hivi karibuni kutakua ni
muarobaini wa kutatua changamoto za kifedha kwa wananchi wanaohitaji
mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Akijibu
swali la Msingi la Mbunge huyo kuhusu hatua za Serikali za kuhakikisha
Benki nchini zinapunguza riba ili kuchochea shughuli za biashara, Dkt.
Kijaji alisema kuwa Sekta ya Benki inafanya biashara huria na ilianza
tangu mwaka 1991 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Benki na
Vyombo vya Fedha ya Mwaka 1991.
“Kupitia
Sheria hiyo, wawekezaji walifungua benki binafsi nchini na gharama za
huduma na bidhaa kuamuliwa na nguvu ya soko hivyo Serikali haina mamlaka
ya moja kwa moja ya kupunguza viwango vya riba katika soko”,
alisisitiza Dkt. Kijaji.
Hata
hivyo alizitaja hatua ambazo Serikali imezichukua kwa upande wake kuwa
ni pamoja na kuzitaka benki za biashara kutumia Mfumo wa kuhifadhi na
kutoa taarifa za wakopaji, Benki Kuu kuanza kutoa mikopo ya muda mfupi
kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89 na pia kushusha riba
kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.
Hatua
zingine ni Benki Kuu kupunguza kiwango cha chini cha amana
kinachotakiwa kuwekwa na Benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi
asilimia 8.0 na pia Serikali kuendelea kulipa malimbikizo ya madai
yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na
kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha
Naibu Waziri huyo ameipongeza benki ya CRDB, NMB na Benki ya ABC kwa
kupunguza riba ya mikopo kutoka asilimia zaidi ya 20 hadi kufikia
asilimia 17 hivyo kuwa na tumaini kuwa Benki zingine zitaendelea kufanya
hivyo.
Imetolewa na;
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
0 comments:
Chapisha Maoni