WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk.Mwigulu Nchemba amesimamisha kazi Msajili
wa Taasisi za Dini Maryline Komba huku akiwaomba viongozi wa dini
kuendelea na shughuli zao za kutoa huduma za kiroho.
Waziri Mwigulu ameyasema hayo wizarani hapo wakati alipotangaza kumsimamisha kazi na kupisha uchunguzi wa kina na iwapo atabainika kutohusika na matamko hayo au nyaraka ambazo zinasambaa mtandaoni basi atarudi kwenye majukumu yake.
Wizara yake inaendelea kuchunguza aliyeandika na kusambaza nyaraka katika mitandao ya kijamii ambayo imeibua sintofahamu kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla ili sheria ichukue mkondo wake.
“Serikali na viongozi wa dini wamekuwa na ushirikiano mkubwa na hakuna mahali ambapo wanaonekana kutoaminiana.Hivyo aliyesambaza nyaraka hizo tunachunguza na kisha tutachukua hatua zinazostahili,”amesema Dk.Mwigulu.
Amesema viongozi wa dini na watanzania kwa ujumla wafahamu kuwa nyaraka na matamko ambayo yamesambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina baraka za Wizara yake wala Serikali na hivyo ni vema zikapuuzwa tu.
Amewaomba viongozi wa dini kupuuza nyaraka zinasambazwa kwenye mitandao na kusema “Endeleeni na shughuli zenu kama kawaida kwani nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria hivyo hakuna sababu ya kuhofu.
Amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu viongozi wa dini zote huku akionya wanaotaka kutumia dini kama kigezo cha kufanya siasa au kuigawa nchini.
“Wale ambao wanataka kutugawa kwa misingi ya kidini ni vema wakaacha kwani haitakuwa na tija kwao wala kwa Taifa letu .Hivyo tusiwe sehemu ya kushabikia mambo yanayohusu dini,”amesema.
0 comments:
Chapisha Maoni