Mameneja
wote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchi nzima wameagizwa kuwa na
utaratibu wa kuwatembelea wafanyabiashara mara kwa mara ili kujua
changamoto zao na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kodi kwa
wafanyabiashara hao.
Agizo
hilo limetolewa leo na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere jijini
Dodoma alipohitimisha ziara yake ya kikazi ya kujiridhisha utendaji
kazi wa Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) ambazo mfumo
wake ulipata hitilafu ya kiufundi hivi karibuni na kusababisha mashine
hizo kutokufanya kazi.
"Nimepita
katika baadhi ya maeneo mengi kuanzia Dar es Salaam, Kibaha, Mlandizi,
Morogoro, Gairo na sasa nimemalizia Dodoma. Katika maeneo yote
niliyopita nimekuta wafanyabiashara wana changamoto ambazo zinaweza
kutatulika kirahisi na Mameneja bila ya kusubiri mpaka Kamishna Mkuu
apite, hivyo nawaagiza Mameneja kuwatembelea wafanyabiashara katika
maeneo yao, kujua changamoto wanazozipata ili kuzitatua mara moja
kinyume na hapo nitachukua hatua," alisema Kichere.
Aidha,
Kamishna Mkuu Kichere alieleza kuwa, tatizo la Mashine za EFD
limekwisha na tayari zimeanza kufanya kazi, hivyo Mameneja wote wa mikoa
wanatakiwa kupita katika maeneo yao ili kufanya ufuatiliaji wa mashine
hizo na kuzitolea taarifa zile zitakazokutwa bado zina matatizo kwa
ajili ya kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
"Ninasema
Mameneja wawatembelee wafanyabiashara mara kwa mara kwasababu nimepita
katika maduka mbalimbali nimekuta kuna baadhi ya wafanyabiashara tangu
Mfumo wa EFD upate hitilafu mpaka leo hawajawasha mashine zao na
nilipoziwasha nimekuta zinafanya kazi vizuri, hivyo kinachotakiwa ni
Mameneja kupita katika maeneo yao na kufanya ukaguzi wa mashine husika
na kuwapa elimu," alifafanua Kichere.
Kamishna
Mkuu Charles Kichere amehitimisha ziara yake iliyoanzia Dar es Salaam
mpaka Dodoma akipita katika maduka na vituo mbalimbali vya mafuta kwa
ajili ya kujiridhisha kama mashine za EFD zinafanya kazi vizuri baada ya
mfumo wake kupata hitilafu ya kiufundi tangu Mei 11, mwaka huu
kutengemaa na kuruhusu mashine hizo kuanza kufanya kazi kama
inavyotakiwa.
Mwisho.
0 comments:
Chapisha Maoni