WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania waulinde Muungano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na
akawaonya wasitumie Bunge hilo kuupotosha.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 10, 2018) Bungeni mjini Dodoma kwenye
mkutano wa 11 wa Bunge, wakati akihitimisha mjadala wa mapitio ya
utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi
za Serikali kwa mwaka 2018/2019.
Waziri
Mkuu amesema mjadala ulioibuka jana kuhusu suala la Muungano haukuwa na
afya na kwamba hatarajii kuona hali hiyo ikijirudia tena Bungeni
kuhusiana na suala la Muungano.
“Mjadala
wa jana sijaupenda kabisa na wala haukuwa na afya, ulikuwa ni malumbano
baina waheshimiwa wabunge wawili. Hatuzuii Mhe. Mbunge kuuliza jambo
ili apate ufafanuzi lakini pia haturuhusu mtu na mtu watumie Bunge
kupotosha ukweli wa mambo,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu amelieleza Bunge kwamba kuna maboresho ambayo yanafanywa hivi sasa
na Serikali za pande zote mbili lakini akatumia fursa hiyo
kulihakikishia Bunge kwamba majadiliano bado yanaendelea kwenye vikao
halali vya SMT na SMZ ambavyo vinaongozwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia
Suluhu Hassan.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu chanzo cha malumbano hayo, Waziri Mkuu alisema kiini
cha malumbano hayo ni suala la uagizaji sukari kutoka nje ya nchi ili
kufidia upungufu wa sukari uliopo nchini (gap sugar). Alisema katika
kutimiza azma hiyo, Serikali haiangalii kama muagizaji ametoka Tanzania
Bara au Tanzania Zanzibar.
Akitoa
mfano, Waziri Mkuu alisema katika mwaka 2016, upungufu uliojitokeza
ulikuwa tani 140,000 lakini waagizaji waliopewa vibali walikuwa wawili
kutoka Zanzibar, watatu kutoka Bara na kiwanda cha sukari cha Mahonda
kilipewa kibali cha kuagiza tani 390.
“Katika
mwaka 2017, gap sugar ilikuwa tani 140,000 na waliopewa vibali walikuwa
ni wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Bara, lakini kwa mwaka huu
(2018) gap sugar ni tani 135,000. Tofauti na miaka ya nyuma, safari hii
tumewapa vibali wenye viwanda ndiyo waagize sukari kutoka nje. Kwa hiyo,
jambo hili la sukari lisivuruge Muungano wetu,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu alisema nia ya Serikali ni kuzalisha sukari ya kutosha hapa nchini
ili nchi ijitegemee na kawataka Mawaziri wa Biashara wa Zanzibar na
Tanzania wawe makini ili sukari inayoagizwa nje isije kufurika soko la
ndani kwa sababu gharama za uzalishaji sukari ya ndani ni kubwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Chapisha Maoni