test

Jumamosi, 28 Aprili 2018

Wanafunzi watoroka wakidai kukwepa viboko


Wanafunzi wanne kati ya watano wa Shule ya Msingi Ndolage, Kata ya Kamachumu, Kagera wamekamatwa wakidaiwa kutoroka shule na kwenda kutafuta kazi za ndani mjini Bukoba.

Wanafunzi hao wenye miaka 11 hadi 14 walitoroka Aprili 25 wakiwa na sare za shule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ndolage, Frederick Byarugaba alisema wanafunzi hao (majina tunayahifadhi) walitoka nyumbani kwao Kitongoji cha Buganda B, Kamachumu na walipata usafiri wa kuelekea Bukoba Mjini.

“Baada ya taarifa hizo kusambaa kuwa wanafunzi wametoroka, uongozi wa shule ulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, Kituo cha Kamachumu, Muleba,” alisema Byarugaba.

Alisema watoto hao walionekana kwa mara ya kwanza, Manispaa ya Bukoba wakitembea pamoja na baadhi ya watu wakiwamo abiria waliwakamata na kutoa taarifa polisi na kwa uongozi wa shule.

“Walikuwa na utoro wa rejareja na mara kadhaa wamekuwa wakikanywa kuhusu tabia mbaya ya utoro, hivyo baada ya wazazi kutoa taarifa ya kutoonekana nyumbani tulianza kusambaza ujumbe wa kuwatafuta,” alisema Byarugaba.

Mmoja wa walezi wa watoto hao, Christopher Kalumuna alisema kuwa baada ya mwalimu wa zamu kudai hawakuonekana shuleni hapo alisambaza taarifa kwenye miji midogo ya Kemondo, Kyetema na Bukoba Mjini hadi kwenye vituo vya magari ili kubaini kama wanaweza kusafiri.

“Huyu ni mtoto wa marehemu kaka yangu (jina tunalihifadhi) na mama yake naye ni marehemu, alikuwa akinifanyia kazi za nyumbani baada ya kutoka shule,” alisema Kalumuna.

Akizungumza kuhusu kilichowafanya kutoroka, mtoto huyo alisema walirubuniwa na mwenzao, ambaye aliiwambia kuwa shuleni kumeandaliwa adhabu ya watoto watoro hivyo watoroke kuepuka viboko au nyaya za umeme.

“Tuliogopa adhabu na ni kweli tumekuwa watoro kila mara na tunachelewa shule. Tulipoondoka tulilala kichakani bila kula huko Kemondo na tulitembea kwa miguu.

“Baada ya kufika Bukoba mjini kiongozi wetu (mwanafunzi mwenzao) alitutoroka na tuliokotwa baada ya kuanza kulia, ndipo tukamweleza aliyetuokota akatupandisha kwenye gari hadi Kamachumu,” alisema mtoto huyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Agustino Olomi alithibitisha kupokea taarifa za watoto hao.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni