Dodoma, April 13, 2018:
Serikali
imefafanua hatua zilizochukuliwa kuhakikisha Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) linafaidika na kampuni ya ubia ya StarMedia, huku
ikisisitiza kuwa uongozi wa sasa chini ya Rais John Pombe Magufuli
umefanya mageuzi makubwa na ya kihistoria katika kuwawezesha
wajasiriamali wadogo na wa kati.
Wakizungumza
mjini hapa jana katika mfululizo wa mawaziri kufafanua utekelezaji wa
hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dkt.
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na
Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
wamesisitiza ripoti ya CAG ni nyenzo muhimu kwao.
Dkt. Mwakyembe: TBC Sasa Kufaidika na StarMedia
Akizungumzia
hoja ya CAG kuhusu mkataba wa StarMedia, Waziri Mwakyembe amewaambia
waandishi wa habari kuwa changamoto kubwa iliyosababisha kampuni hiyo
kutozalisha faida kwa miaka saba sasa ni udhaifu katika uendeshaji wa
kampuni na baadhi ya watendaji wa zamani wa TBC waliotarajiwa kusimamia
maslahi ya Taifa kususa, kujiuzulu na kuuacha uendeshaji chini ya wabia
kutoka China.
Hata
hivyo Waziri Mwakyembe ameongeza kuwa baada ya Serikali kumwagiza CAG
kufanya ukaguzi ikiwemo pia yeye binafsi Kuunda Kamati Maalum ya Waziri
kuchunguza mkataba wa StarMedia, sasa makubaliano yamefikiwa ili kuondoa
dosari zote.
“Baada
ya majadiliano ya muda mrefu na wenzetu wa StarTimes Group (kampuni
mama yenye hisa nyingi katika ubia wa StarMedia), wenzetu hatimaye
wamekubali taarifa ya CAG na mapendekezo yake yote,” alisema Waziri
Mwakyembe.
Aliyataja
baadhi ya makubaliano yaliyosainiwa ili kuigeuza StarMedia kujiendesha
kwa ufanisi zaidi kuwa ni pamoja na: kufanyiakazi hoja zote za CAG,
kuongeza wafanyakazi zaidi wa Kitanzania katika menejimenti, uwazi zaidi
katika uendeshaji wa kampuni na kuanzia sasa Bodi ya ubia inayoongozwa
na Mkurugenzi Mkuu wa TBC kuwa ndio chombo cha juu cha uamuzi badala ya
kusubiriwa maelekezo kutoka Beijing, China.
Aidha,
Waziri Mwakyembe ameeleza kuwa, kwa kuwa kampuni hiyo haikuwa kutoa
gawio kwa wanahisa wake, kuanzia mwaka huu, wakati kasoro zote
zilizobainishwa na CAG na Kamati ya Waziri zikifanyiwakazi, StarMedia
itatoa ruzuku ya Shilingi Bilioni tatu (3) kwa TBC.
“Kwa
niaba ya Serikali, Wizara yangu itafuatilia kwa karibu utekelezaji na
haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa mtendaji wa
upande wowote atakayekuwa kikwazo katika uendeshaji wa kampuni,”
alisema.
Waziri Mwijage: Tumeongeza Bajeti Kuinua Wajasiriamali
Kwa
upande wake, Waziri Mwijage, akifafanua hoja mbalimbali zilizoelekezwa
katika Wizara yake alisema ameshaagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa
taasisi zote zilizo chini ya wizara yake kutekeleza hoja mahsusi za
CAG.
Kwa
upande wa hoja ya mchango mdogo wa Sekta ya Wajasiriamali Wadogo na wa
Kati nchini, Waziri Mwijage amefafanua kuwa wakati lengo kuu ni ifikapo
2025 sekta hiyo kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 40, tayari kwa
ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi, inachangia asilimia 35, ambazo
ni kubwa ikilinganishwa na nchi jirani.
“Kwa
kulinganisha mchango wa sekta hii kwa Tanzania katika pato la taifa na
nchi nyingine bado nchi yetu inafanya vizuri. Kwa Kenya sekta hiyo
inachangia takribani asilimia 25; Uganda asilimia 20; Afrika ya Kusini
asilimia 36; India asilimia 40 na Malaysia 40,” alisema.
Aidha,
Waziri Mwijage amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya
mageuzi makubwa katika utoaji wa mtaji kwa Mfuko wa Kuendeleza
Wajasiriamali (NEDF) na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO)
ambapo mwaka jana Mfuko huo ulipewa Bajeti ya Shilingi bilioni tano (5),
mwaka huu Bajeti iliongezwa hadi shilingi bilioni saba (7.8).
Bajeti
ya SIDO imeongezeka mpaka shilingi bilioni 26.8; kiasi ambacho ni cha
kihistoria kwani hakijapata kutolewa na Serikali kabla ya kuingia Awamu
ya Tano.
“Kama
CAG alivyobaini, sekta hii ni uti wa mgongo wa Taifa kulingana na
uchangiaji wake katika pato la Taifa na ajira. Kutokana na nafasi ya
sekta hii katika kujenga taifa la uchumi wa kati, ni mpango wa Wizara
kuendelea kuiongezea rasilimali zaidi,” alisema.
Katika
mfululizo wa Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kufafanua
utekelezaji wa hoja mbalimbali za CAG, Jumatatu ijayo itakuwa zamu ya
Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo.


0 comments:
Chapisha Maoni