Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewapongeza madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI) iliyopo Jijini Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa iliyoyapata
katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ametoa pongezi hizo hizo tarehe 18 Aprili, 2018 alipotembelea taasisi hiyo na kuwajulia hali wagonjwa wanaopatiwa matibabu akiwemo Waziri Mstaafu Dkt. Juma Ngasongwa.
Mhe.
Rais Magufuli amesema JKCI ambayo imepata mafanikio katika matibabu ya
moyo kwa njia ya upasuaji wa tundu dogo na kufungua kifua imesaidia
kuokoa vifo kwa Watanzania wengi waliokuwa wanakosa uwezo wa kifedha wa
kwenda kutibiwa nje ya nchi, imepunguza gharama za kutibiwa nje ya nchi
na imeijengea heshima Tanzania.
“Prof.
Janabi, madaktari wote na wauguzi wa taasisi hii nawapongeza sana kwa
kazi nzuri mnayoifanya, natambua kuwa wapo baadhi ya waliokuwa
wananufaika na wagonjwa kupelekwa nje ya nchi hawatafurahia kazi
mnayoifanya lakini nyinyi chapeni kazi na Serikali ipo na nyinyi”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli
kwa kuitembelea taasisi hiyo na kuwatia moyo na ameahidi kuwa
wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi ili kuimarisha zaidi huduma za
matibabu ya moyo.
Amefafanua
kuwa JKCI imefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wanakwenda
kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 83 na kwamba tangu mwaka 2015 idadi ya
wagonjwa waliotibiwa katika taasisi hiyo ni zaidi ya 2,420 ambao
wangehitaji wastani wa Shilingi Milioni 30 kwa kila mmoja kutibiwa nje
ya nchi.
Kabla
ya kutembelea JKCI Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth
Magufuli wamekwenda Kariakoo Jijini hapa kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Bw. Mrisho Gambo ambaye amefiwa na Mama yake Bi Rehema Paulo
Mombuli, ambaye mwili wake unasafirishwa kwenda Arusha na baadaye Moshi
mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Chapisha Maoni