Na Benny Mwaipaja
Serikali
imeeleza kuwa kiasi chote cha dola za Marekani milioni 65 zilizokopwa
na Kiwanda cha Sukari cha Kagera kutoka Benki ya CRDB kwa udhamini wa
Serikali mwaka 2004 kimewekezwa nchini na hakijapelekwa kuwekeza katika
nchi ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa aliyetaka kujua sababu za
Serikali kumdhamini mwekezaji wa Kiwanda hicho kukopa kiasi hicho cha
fedha ambacho kimepelekwa kuwekezwa nchini Kongo wakati Tanzania ina
uhaba wa sukari.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa uwekezaji uliofanywa katika Kiwanda
cha Kagera ni wa takribani dola za Marekani milioni 250 hivyo
haiwezekani mwekezaji kukopa dola milioni 65 na kuzipeleka Congo ili
hali kiwango cha uwekezaji nchini ni kikubwa.
“Mwekezaji
wa Kiwanda hicho ni wa ndani na amejitahidi kuajiri watanzania wengi
hivyo Serikali ipo katika mchakato wa kukiwezesha kiwe cha mfano ili
kiendelee kuleta matokeo chanya kwa watanzania”, alisema Dkt. Kijaji.
Katika
swali la msingi la Mbunge huyo, alitaka kujua kiwango cha hisa ambacho
Serikali inamiliki katika kiwanda cha Sukari cha Kagera na kiasi cha
fedha kilichokopwa na kulipwa na mwekezaji huyo kupitia udhamini huo wa
Serikali.
Dkt.
Kijaji alieleza kuwa Serikali kwa sasa haimiliki hisa zozote katika
kiwanda hicho na kuongeza kuwa hisa zake katika kiwanda hicho ziliuzwa
mwaka 2001 baada ya kukibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Kagera
Saw Mills Limited.
Aidha
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa mwekezaji wa Kiwanda hicho alikopa kiasi
cha dola za Maerekani milioni 65 kwa kutumia udhamini wa Serikali mwaka
2004, ikiwa ni udhamini (guarantee) wa kipindi cha miaka 12.
Alisema
kuwa mpaka sasa kiwanda hicho mimerejesha zaidi ya dola za Marekani
milioni 56.88, sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote, na kwamba marejesho
ya mkopo uliobaki wa Dola milioni 8.12 yatafikia ukomo wake mwezi
Julai, 2019.
0 comments:
Chapisha Maoni