HOTUBA YA WAZIRI
MKUU, MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA
SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA
OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2018/2019
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge
lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya
Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na Mwelekeo wa
Kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali
kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019.
2.Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi
wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena kujadili
Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na
Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019.
3.Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutokana na fikra
na uongozi wao makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa juhudi zao
katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali, zinaleta
manufaa makubwa kwa wananchi.
4.Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumewapata Waheshimiwa Wabunge wapya
kutokana na chaguzi ndogo zilizofanyika. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mhe.
Dkt. Godwin Mollel (Mbunge wa Jimbo la Siha) na Mhe. Maulid Mtulia (Mbunge wa
Jimbo la Kinondoni) kwa kuchaguliwa na kisha kuapishwa na Bunge lako Tukufu ili
waendelee kuwatumikia wananchi wa majimbo yao na Watanzania kwa ujumla. Ni
matumaini yangu kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kuwapatia ushirikiano wa
kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
5. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Bunge lako
lilimpoteza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Leonidas T.
Gama. Vilevile, baadhi ya waheshimiwa Wabunge na wananchi tunaowawakilisha
walipata misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. Aidha, kulitokea maafa na majanga
ambayo yalisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Pia, kumekuwepo na
ajali za barabarani ikiwemo ajali mbaya iliyotokea tarehe 24 Machi 2018
wilayani Mkuranga na kugharimu maisha ya Watanzania 26. Ninaomba Mwenyezi Mungu
awajalie afya njema waliopata majeraha. Aidha, ninatoa pole kwa ndugu jamaa na
marafiki kwa misiba iliyotokea. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu
mahala pema peponi. Amina!
6.Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa salamu za pole kwa
Waheshimiwa Wabunge wenzetu waliopata majeraha mbalimbali kufuatia ajali ya
gari tarehe 29 Machi 2018 walipokuwa wakitoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam.
Wabunge hao ni Mheshimiwa Haji Ameir Haji (Mbunge wa Makunduchi), Mheshimiwa
Khamis Ali Vuai (Mbunge wa Mkwajuni), Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria
(Mbunge wa Chwaka), Mheshimiwa Makame Mashaka Foum (Mbunge wa Kijini) na
Mheshimiwa Juma Othman Hija (Mbunge wa Tumbatu). Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu
awajalie afya wenzetu hawa ili waweze tena kuungana nasi kutekeleza majukumu
yao katika Bunge lako hili Tukufu.
7.Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za
Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali
za Mitaa. Kipekee, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria inayoongozwa na Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa
Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mhe.
Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi; na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini.
Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Aidha, nichukue
nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za
Kudumu za Bunge kwa kuaminika na kuchaguliwa kuongoza Kamati hizo.
8.Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri,
Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu
Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na
Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza
majukumu yangu. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake
kwa kutekeleza majukumu yao na kukamilisha kuandaa Bajeti ya Serikali ya mwaka
wa fedha 2018/2019.
9. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa, napenda kumshukuru Mhe.
Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu; Mhe. Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Mhe. Stella Alex Ikupa, Mbunge Viti Maalumu na
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Makatibu Wakuu Bibi Maimuna K.
Tarishi, Profesa Faustin R. Kamuzora, na Bwana Eric F. Shitindi, Wakurugenzi,
Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa
ushirikiano wao mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu.
10.Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo
nchi marafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na
mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea nchi maendeleo.
11.Mheshimiwa Spika, ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa
kuendelea kuniunga mkono na niwapongeze kwa kutekeleza shughuli za maendeleo
jimboni kwa ufanisi, wakati mimi Mbunge wao nikitekeleza majukumu ya kusimamia
utendaji wa Serikali. Kipekee, ninamshukuru mke wangu mpendwa, Mary na familia
yangu kwa upendo wao, uvumilivu na maombi yao wakati wote ninapotekeleza
majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru
sana.
MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI
12.Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa kazi za
Serikali kwa mwaka 2018/2019 ni kuboresha utendaji wa Serikali na kuwezesha
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/2019. Aidha, Mpango na Bajeti
umezingatia azma ya Serikali ya kufikia malengo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo
wa Miaka Mitano ambao umepangwa kuhitimishwa mwaka 2020/2021 ukiwa na dhima kuu
ya “kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya
watu”. Vilevile, Mpango huu umezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015
na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa
mwaka 2015 pamoja na utekelezaji wa hotuba yake wakati akizindua Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015.
MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
13.Mheshimiwa Spika, tukiwa tunaingia kwenye Bunge
la tatu la bajeti kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatuwezi kumsahau Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa
kazi nzuri anayoifanya ya kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania kwa kujenga
nchi yenye uchumi imara. Katika kipindi hiki, tumeshuhudia mambo makubwa
aliyoyafanya yakiwemo kujenga ari ya uzalendo kwa kuilinda na kuisemea nchi
yetu bila woga; kudumisha amani, utulivu na mshikamano; kuimarisha ulinzi na
usalama kwa kukomesha vitendo vya mauaji yaliyojitokeza Mwanza, Amboni (Tanga),
Mkuranga, Kibiti, Rufiji (Pwani) pamoja na kudhibiti na kupambana na dawa za
kulevya.
14.Mheshimiwa Spika, kazi nyingine alizofanya ni
kujenga nidhamu ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe; kuendesha vita
dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma; kuanzisha mahakama ya rushwa
na ufisadi; kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi zikiwemo za madini na
maliasili. Aidha, amefufua Shirika la Ndege la Tanzania; ameanzisha ujenzi wa
reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR); ameendeleza ujenzi wa barabara
zikiwemo barabara za juu (flyovers) na amenunua meli na vivuko. Kazi nyingine
ni ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme kama vile Stiegler’s Gorge; usambazaji
umeme hadi vijijini na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi
Tanga (Tanzania).
15.Mheshimiwa Spika, mambo mengine makubwa
aliyoyafanya ni kuimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa, vifaa na
vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya; kutoa elimumsingi bila
malipo kwa watoto wa Kitanzania; ujenzi wa miradi ya maji; na kuimarisha bei za
mazao ya kibiashara. Aidha, Mheshimiwa Rais ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa,
hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali
mjini Dodoma. Haya ni baadhi tu ya mambo aliyoyafanya na yatatolewa ufafanuzi
wa kutosha kupitia wizara za kisekta.
HALI YA UCHUMI
16.Mheshimiwa
Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo uchumi
wake unakua kwa kasi. Viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika kipindi cha
kuanzia Januari hadi Septemba 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8, kiwango
ambacho kilikuwa juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambapo Uchumi wa Kenya ulikuwa kwa asilimia 6.1, Rwanda asilimia
6.0, Uganda asilimia 5.5, Burundi asilimia 0.0 na Sudan Kusini asilimia hasi
6.3. Hata hivyo, takwimu za hivi
karibuni kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kwamba katika
kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2017, Pato halisi la Taifa lilikua kwa
kiwango cha asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016.
Shughuli
zilizochangia ukuaji huo kwa viwango
vikubwa ni pamoja na uchimbaji wa madini na mawe asilimia 17.5; huduma za usambazaji maji safi na majitaka asilimia 16.7; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo
asilimia 16.6; habari na mawasiliano
asilimia 14.7 na ujenzi asilimia 14.1.
Aidha, sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ilikua kwa asilimia 3.6, kiwango
ambacho hakijawahi kufikiwa tangu mwaka 2010.
17.Mheshimiwa Spika, kufikia Desemba 2017, deni la Taifa
lilikuwa Dola za Marekani milioni 25,419.6. Viashiria vyote vya deni vinaonesha
kuwa deni linahimilika kwani, thamani ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni Asilimia
19.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya deni la nje kwa uuzaji
wa bidhaa nje ni asilimia 81.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na
thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 117.1 ikilinganishwa na
ukomo wa asilimia 200. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, bado tuna uwezo wa
kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ili kugharamia shughuli za maendeleo. Kwa
ujumla viashiria vya kuimarika kwa uchumi, vinatoa mwelekeo mzuri wa kufikiwa
kwa malengo yetu ya kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa
viwanda ifikapo mwaka 2025.
SIASA
18.Mheshimiwa Spika, ni miaka 26 sasa imepita tangu
mfumo wa siasa wa vyama vingi uanzishwe nchini. Katika kipindi hicho tumeona
ushiriki wa Watanzania katika siasa ukiendelea kuongezeka na uhuru wa kujiunga
na vyama vya siasa kwa kuridhishwa na itikadi za vyama hivyo pia ukiongezeka.
Ni vyema tukajenga utamaduni wa kuheshimu wananchi pale wanapoamua kujiunga na
chama cha siasa watakachokipenda. Jukumu
letu kama viongozi wa siasa ni kunadi sera zetu kwa wananchi na kuhamasisha ujenzi
wa demokrasia inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa
aina yoyote pamoja na kudumisha amani, utulivu, mshikamano na kujenga umoja wa
kitaifa.
19.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, kumefanyika
chaguzi ndogo za Wabunge katika majimbo matano na Madiwani katika kata
59
kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali. Chaguzi
hizi
zilisimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ufanisi. Katika chaguzi
ndogo za ubunge zilizofanyika katika majimbo ya Songea Mjini,
Singida Kaskazini, Longido, Kinondoni na Siha, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kilishinda
majimbo yote. Vilevile, katika uchaguzi wa Madiwani, CCM ilishinda
katika kata
58 na CHADEMA ilishinda katika kata moja. Nichukue nafasi hii
kuvipongeza vyama
vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo na kipekee
nakipongeza Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata ushindi mkubwa na wa kishindo katika
maeneo
mengi.
20.Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili imeendelea kuhakikisha kuwa demokrasia ya vyama vingi
vya siasa inaimarika. Katika mwaka 2017/2018, Ofisi ya Msajili iliratibu kikao
cha Baraza la Vyama vya Siasa ambacho pamoja na kufanya uchaguzi wa Viongozi wa
Kamati za Baraza hilo, kilijadili mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria Mpya ya
Vyama vya Siasa na marekebisho ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya siasa.
Vilevile, Ofisi ya Msajili inaendelea kukusanya maoni ya wadau kwa lengo la
kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992
pamoja na kanuni zake.
MUUNGANO
21.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, kumefanyika vikao mbalimbali vya kisekta vya
ushirikiano kati ya Wizara za SMT na SMZ kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi
changamoto mbalimbali za Muungano wetu. Baadhi ya changamoto hizo ni masuala ya
fedha, biashara na ajira katika taasisi za Muungano. Katika kipindi hicho, viongozi na wataalamu wa pande mbili za Muungano
walikutana kwa ajili ya kujadili hoja zinazohusu sekta za fedha, biashara,
viwanda na uwekezaji, ujenzi na uchukuzi, maliasili na utalii.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
22.Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza zoezi
la kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Tangu utekelezaji wa zoezi hilo
uanze mwezi Septemba 2016, jumla ya watumishi wa umma 3,829 kutoka Wizara na
taasisi mbalimbali wamehamia Dodoma katika awamu ya kwanza na ya pili, na awamu
ya tatu inaendelea. Katika kufanikisha azma hii, Serikali inaboresha
miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, umeme, mifumo ya maji safi na
maji taka, ofisi, makazi na kuimarisha huduma za elimu, afya, mawasiliano na
michezo.
23.Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga kuijenga Dodoma
kuwa mji bora na wa kisasa unaoendana na mahitaji na mifumo ya miji bora
duniani. Ili kufikia azma hiyo, Serikali inashirikiana na wadau ikiwemo sekta
binafsi na mashirika ya kimataifa kuujenga Mji wa Dodoma. Napenda kumpongeza
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye mara tu baada ya kuhamia Dodoma amezindua “Kampeni ya Kijanisha
Dodoma” inayolenga kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Kampeni hiyo inahusisha
kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya ukanda wa kijani.
24.Mheshimiwa Spika, niupongeze Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa kufungua ofisi zake za muda
mjini Dodoma mwezi Desemba 2017. Natoa wito kwa mashirika mengine ya kimataifa
na mabalozi waige mfano huu wa kuhamishia ofisi zao Dodoma. Serikali itaendelea
kutoa ushirikiano wa karibu kwa Mashirika ya Kimataifa na wanadiplomasia katika
kurahisisha maandalizi yao ya kuhamia Dodoma. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji
wa ndani na nje kuendelea kuwekeza Dodoma kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji
ikizingatiwa nafasi yake kijiografia inayosaidia mikoa yote hapa nchini
kufikika kwa urahisi na haraka zaidi. Nichukue fursa hii kuipongeza Kamati
inayoratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma inayosimamiwa na Mheshimiwa
Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Bibi
Maimuna K. Tarishi, Katibu Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge).
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
25.Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
mipango mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na wananchi kujiletea maendeleo.
Moja ya jitihada zilizofanywa na Serikali ni kuanzisha mifuko ya
uwezeshaji ambayo inatoa mikopo kupitia vikundi vya vijana, wanawake, wazee,
watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
26.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Mfuko wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulidhamini mikopo yenye thamani ya takriban
shilingi bilioni 13 kwa SACCOS 58, VICOBA 172 na kampuni mbili. Aidha, Mfuko wa
Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi umetoa mikopo ya Shilingi bilioni 62.8 kwa wajasiriamali
85,982. Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 3.4 kwa vikundi 5,169 katika Halmashauri 153. Mfuko wa Kilimo Kwanza
ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 62.7 kwa miradi 189 katika
wilaya 76.
27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Mfuko wa Taifa wa
Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 783 ambapo
vijana 840 kutoka Halmashauri mbalimbali walinufaika. Aidha, katika kipindi
hicho, Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia asilimia 5 ya mapato yao ya ndani
zilitenga shilingi bilioni 15 ikiwa ni mikopo ya masharti nafuu kwa vijana.
Vilevile, Halmashauri 48 zilitenga ekari 217,882 kwa ajili ya shughuli za
uzalishaji mali kwa vijana nchini. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea
kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
28. Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inaratibu jumla
ya mifuko na programu 31 za uwezeshaji ambazo usimamizi wake upo katika Taasisi
mbalimbali za Serikali na za binafsi. Kila mfuko au programu imeanzishwa kwa
sheria yake au taratibu maalumu zinazosimamia utendaji wa mfuko husika.
Serikali imeona kuna umuhimu wa kupunguza idadi ya mifuko kwa lengo la kuongeza
ufanisi wa utendaji wake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Hivyo, tumeanza
kufanya mapitio ya utendaji wa mifuko hiyo kwa nia ya kuunganisha baadhi ya
mifuko yenye majukumu yanayofanana. Hatua hiyo, itasaidia kuwa na mifuko
michache yenye tija ambayo itaharakisha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ukuzaji Ujuzi
29.
Mheshimiwa Spika, suala la kukuza ujuzi wa nguvukazi
tuliyonayo ni miongoni mwa ajenda muhimu ya kisera katika kuwezesha wananchi
kujikwamua kiuchumi. Serikali inatoa msukumo wa kipekee kupitia Programu ya
Ukuzaji Ujuzi nchini kwa lengo la kuwapatia ujuzi na stadi za kazi wananchi
hasa kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kumudu
ushindani katika soko la ajira na hivyo kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa
uchumi jumuishi wa viwanda.
30.Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Serikali kwa
kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2014, unaonesha kuwa asilimia 79.9 ya
nguvukazi ni yenye kiwango cha chini cha ujuzi, asilimia 16.6 kiwango cha kati
wakati ni asilimia 3.6 tu ndiyo yenye kiwango cha juu. Ili kufikia uchumi wa
viwanda, Serikali imedhamiria kubadili mwenendo huo kwa kuhakikisha nguvukazi
yenye kiwango cha juu cha ujuzi inafika asilimia 12 na kiwango cha kati
asilimia 34. Kwa msingi huo, Serikali inaendelea kutekeleza programu ya kukuza
ujuzi pamoja na programu nyingine ili kukidhi matakwa ya uchumi wa viwanda.
31.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, jumla ya
vijana 7,817 wamewezeshwa kupata ujuzi kupitia programu hiyo. Kati yao, vijana
220 walipata mafunzo kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam na vijana
3,440 kupitia Taasisi ya Don Bosco. Mafunzo waliyopewa ni katika fani za ufundi
stadi wa ushonaji nguo, useremala, uashi, TEHAMA, uchongaji wa vipuri, ufundi
magari, umeme, bomba, vyuma, terazo, vigae na ujuzi wa kutengeneza bidhaa za
ngozi. Aidha, kupitia VETA vijana 3,989 walipata mafunzo ya kurasimisha ujuzi
uliopatikana kwa mfumo usio rasmi kwa fani za uashi, useremala, ufundi magari,
upishi na uhudumu katika hoteli.
32.
Mheshimiwa Spika, mafunzo ya vitendo yalitolewa pia
kwa wahitimu 168 kupitia viwanda na kampuni mbalimbali katika fani ya
utengenezaji wa bidhaa za ngozi. Vilevile, Serikali imeandaa na kuzindua
Mwongozo wa Kitaifa wa Uanagenzi na Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo ya Vitendo
kwa wahitimu kwa lengo la kuweka utaratibu wa utoaji wa mafunzo hayo kwa wadau
wote ili waweze kuajirika. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa mafunzo ya
ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 10,500 katika fani mbalimbali.
Ninazishukuru kampuni binafsi ambazo zinaendelea kutoa nafasi za mafunzo ya
vitendo kwa wahitimu wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi
katika nyanja mbalimbali ili tuweze kukuza ujuzi wa rasilimali watu ya taifa.
Ajira
33.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali
imeendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini. Hadi kufikia mwezi Februari
2018, jumla ya ajira 482,601 katika sekta rasmi zimezalishwa nchini. Kati ya
ajira hizo, ajira 345,547, sawa na asilimia 72 zimezalishwa kutokana na
shughuli za umma ikiwemo miradi ya maendeleo ya Serikali kama vile ujenzi wa
reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na miradi ya
TASAF; na ajira 137,054 sawa na asilimia 28 zimezalishwa katika sekta binafsi.
34.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaandaa mpango mkakati wa
kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa wanashiriki na kunufaika na miradi mikubwa
ya kitaifa. Vikao kati ya Serikali na wafanyabiashara vimefanyika ili kuwaandaa
kuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo. Katika mwaka 2018/2019, Serikali
itaendelea kuratibu masuala ya ukuzaji ajira nchini ikiwa ni pamoja na
kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ili iendane na mahitaji ya sasa
ya soko la ajira.
Masuala ya Kazi na Wafanyakazi
35.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo
tija, ufanisi na mahusiano mema mahala pa kazi, Serikali inasimamia Sheria Na.6
ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria Na.7 ya Taasisi za Kazi. Sheria hizo
zinalenga kuhakikisha haki na wajibu kwa mfanyakazi na mwajiri vinapatikana. Ili
kufikia azma hiyo, Serikali imehimiza kuanzishwa kwa mabaraza ya wafanyakazi,
kufunga mikataba ya hali bora pamoja na kufanya kaguzi mbalimbali mahala pa
kazi ili kujiridhisha kuwa viwango vya kazi vinazingatiwa.
36.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi
Februari 2018, jumla ya kaguzi 102,860 zimefanyika katika maeneo mbalimbali ya
kazi nchi nzima. Sambamba na kaguzi hizo, elimu kuhusu sheria za kazi, wajibu
na majukumu ya wajumbe wa baraza kwa waajiri na wafanyakazi kupitia vyama vyao
ilitolewa. Jumla ya waajiri 640 na wafanyakazi 3,624 walipatiwa elimu hiyo. Aidha, mabaraza 441 ya wafanyakazi
yaliundwa na 46 yalihuishwa upya.
37.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Usuluhishi
na Uamuzi ilipokea na kusajili migogoro ya kikazi 6,113 ambapo migogoro 4,816
sawa na asilimia 79, ilitatuliwa kwa njia ya usuluhishi na
uamuzi. Katika mwaka 2017/2018, utafiti kuhusu sekta na vyanzo
vinavyoongoza kwa migogoro ya kikazi umefanyika. Sekta ya usafirishaji
iliongoza kwa kuwa na migogoro 547; ulinzi binafsi 512; viwanda 434; elimu 420;
huduma za hoteli 399 na taasisi za umma 321. Aidha, aina ya vyanzo
vinavyoongoza kusababisha migogoro ya kazi ni kuachishwa kazi bila kufuata
taratibu sahihi; madai mbalimbali na kuvunjwa kwa mikataba isivyokuwa halali.
Utafiti huu utaisaidia Serikali kwa kushirikiana na waajiri na vyama vya
wafanyakazi kuweka mipango ya pamoja na kuzuia migogoro sehemu za kazi kabla
haijatokea.
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa waajiri na
wafanyakazi na kuendeleza mijadala yenye tija ili kupunguza migogoro mahala pa
kazi. Serikali pia itaendelea
kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi, kusajili,
kusuluhisha na kuamua migogoro katika maeneo ya kazi. Aidha, itashirikiana kwa
karibu na vyama vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya mara
kwa mara kwa lengo la kuongeza tija na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
SEKTA BINAFSI
39.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa sekta
binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa letu. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali
inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja
na kuanzisha na kuboresha miundombinu wezeshi kama vile reli, barabara, umeme
na maji. Hatua nyingine ni kupunguza na kufuta baadhi ya kodi zinazoathiri
ufanisi wa sekta binafsi; kuhuisha sera na sheria pamoja na kuimarisha
majadiliano yenye manufaa baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. Katika
kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018, jumla ya miradi 175 yenye thamani ya
Dola za Marekani bilioni 4.4 ilisajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini
(TIC). Miradi hiyo inatarajiwa kutoa fursa za ajira 20,178.
40.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kuimarisha majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa nia ya
kuondoa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta binafsi. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imefanya
mikutano minne na wawakilishi wa sekta binafsi. Miongoni mwa mikutano hiyo, ni
ule uliofanyika tarehe 19 Machi, 2018 ambao uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais
ametoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi za umma kukutana na wawakilishi wa sekta
binafsi ili kutatua kwa haraka changamoto zilizobainishwa katika mkutano huo.
Serikali inawahakikishia wafanyabiashara na sekta binafsi kwamba inawathamini
na itaendelea kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili ili kujenga
uchumi wa viwanda.
SEKTA YA HIFADHI YA JAMII
41.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea
kusimamia utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii
ikiwemo kutungwa kwa sheria inayounganisha Mifuko ya Pensheni ya PSPF, LAPF,
PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma unaojulikana
kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma. Sheria hiyo pia, imefanya
marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii ili kuufanya
Mfuko huo uhudumie wafanyakazi wa sekta binafsi pamoja na kutoa huduma ya
hifadhi ya jamii katika sekta isiyo rasmi.
42.
Mheshimiwa Spika, kutungwa kwa sheria hiyo kutasaidia kuondoa
changamoto iliyotokana na wingi wa mifuko ya hifadhi ya jamii inayolipa mafao
yanayotofautiana kwa watumishi wa umma wenye masharti ya kazi yanayofanana.
Vilevile, sheria hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya baadhi ya mifuko
kutokuwa endelevu kutokana na idadi ndogo ya wanachama, ushindani usiokuwa na
tija na gharama kubwa za uendeshaji. Sheria imeweka kipindi cha mpito cha miezi
sita kitakachoanza tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo. Lengo ni
kuwezesha maandalizi ya utekelezaji wake kufanyika pasipo kuathiri shughuli na
huduma muhimu kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa ikiwa ni pamoja na
kupokea mafao yao.
Napenda kuwataarifu Watanzania kupitia Bunge
hili kwamba tayari Mheshimiwa Rais amesaini muswada huo kuwa sheria ya nchi.
Utekelezaji wa sheria hii utaboresha mafao ya wafanyakazi.
43.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali
itakamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 na
hivyo kuandaa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ambayo itakuwa jumuishi. Lengo la
Serikali ni kuwezesha huduma za hifadhi ya jamii kuwafikia wananchi wengi zaidi
hususan waliopo katika sekta isiyo rasmi na kurahisisha upatikanaji wa huduma
hizo.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
44.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uratibu na
utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kwa
kuhakikisha upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika
kutimiza azma hiyo, Serikali imeunda kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa
12 ya Geita, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Singida, Rukwa,
Shinyanga, Simiyu na Tabora. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha
kuwa mikoa mingine nayo inaunda kamati hizo.
45.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa
kushirikiana na wadau imeendelea kutoa vifaa saidizi kwa jamii ya watu wenye
ulemavu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila utegemezi. Baadhi ya vifaa
vilivyotolewa ni viti mwendo 240, bajaji 6, magongo ya kutembelea 350, kofia
pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum kwa wenye uoni hafifu 70, shime sikio
20, vyerehani 8, vifaa vya kukuzia maandishi 65, mafuta maalum ya kukinga ngozi
dhidi ya mionzi ya jua 35, viti maalum vya kuogea 50 na nyenzo nyingine za
kujimudu. Vilevile, Serikali imeendelea kuviboresha vyuo vya watu wenye ulemavu
vya Yombo, Dar es Salaam na Sabasaba, Singida. Serikali pia inakamilisha
uanzishwaji wa kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu kutoka vyuo mbalimbali
nchini ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa za ajira zinazopatikana kwenye
sekta binafsi na umma.
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Mtoto kwa kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa watoa huduma
katika vituo vinavyolea watoto wenye ulemavu wa ngozi kwenye mikoa ya
Shinyanga, Mara, Tabora, Simiyu, Tanga, Mwanza, Kigoma na Singida. Lengo la
utoaji elimu ni kuwajengea uelewa na kuwapa mbinu watoa huduma waendelee
kuimarisha ulinzi kwa watoto pamoja na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii waone
umuhimu wa kulea watoto hao kwenye ngazi ya familia.
47.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2018/2019, Serikali
itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kukamilisha
uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu. Serikali pia
itaendelea na zoezi la kuanzisha madawati ya watu wenye ulemavu na kuhamasisha sekta binafsi na umma kuweka
miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Serikali itahimiza waajiri
wote nchini kuajiri watu wenye ulemavu wenye sifa kwenye nafasi mbalimbali na
pia kutoa matangazo ya ajira yanayohamasisha wenye ulemavu kuomba nafasi
zinazotangazwa. Vilevile, itahamasisha na kuelimisha jamii kuhusu mahitaji
maalum ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwaheshimu, kuwatambua, kuwathamini na
kutowanyanyapaa.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
Hali ya Upatikanaji wa Chakula
48.
Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea
kuimarika. Katika msimu wa 2016/2017 na 2017/2018, uzalishaji ulifikia tani
milioni 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.3 ya chakula kwa
kipindi hicho. Kutokana na uzalishaji huo, nchi ilikuwa na ziada ya tani
milioni 2.6 za mazao yote ya chakula na hivyo, kujitosheleza kwa asilimia 120.
Aidha, hadi kufikia Januari, 2018 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulikuwa
umenunua jumla ya tani 26,038 za mahindi na akiba ya chakula iliyopo ghalani ni
tani 92,074.
Mazao ya Biashara na Kuimarisha Ushirika
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua
kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni
chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima,
kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea
kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni. Uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji
wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto
kadhaa. Miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi
ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu
mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza vema wajibu wao, wizi,
dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia kilimo cha
kitaalamu.
50.
Mheshimiwa Spika, sababu nyingine za kushuka
uzalishaji wa mazao hayo ni huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu
wa pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu
vya ushirika. Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba ulipungua kutoka tani
456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande wa
tumbaku, uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624
mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 mwaka 2015/2016.
51.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua za
kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia chaguzi za
vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532 na kufanya
kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika zinaendelea. Pamoja na hatua
hiyo, Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja kupitia
maafisa kilimo na Bodi za Mazao. Hatua nyingine ni kufuta baadhi ya tozo
zilizokuwa kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba
mauzo yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.
52.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusimamia mazao makuu ya
biashara, tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa kuongezeka uzalishaji wake.
Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara
ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la mavuno
ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la uzalishaji wa mazao ya
biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo wa bei za mazao hayo
hususan korosho na kahawa.
53.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuimarisha vyama vya msingi
vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya kimkakati ya
biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa
stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya
ushirika kwa njia ya minada. Pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo
limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa
yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora
wakinufaika na bei ya juu zaidi.
Pembejeo za Kilimo
54.
Mheshimiwa Spika, Serikali imerahisisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima baada ya kuanza
kuagiza mbolea kwa kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja. Hadi kufikia
mwezi Machi 2018, upatikanaji wa mbolea hapa nchini ulikuwa tani 310,674, sawa
na asilimia 64 ya mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka. Kwa upande wa mbegu bora
za kilimo, upatikanaji umefikia tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji
ya tani 60,000 kwa mwaka. Kwa mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuboresha
Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ili uendelee kuleta ufanisi na tija
iliyokusudiwa.
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
55.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imekamilisha maandalizi ya Awamu ya Pili
ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo. Programu hiyo itatekelezwa kwa miaka
10 katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Katika mwaka 2018/2019,
Serikali itaweka mkazo katika kutekeleza malengo makuu ya Programu hiyo.
Msukumo utawekwa kwenye kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ya kipaumbele
kwa kuimarisha upatikanaji na matumizi ya pembejeo na zana za kilimo; kuimarisha
huduma za ugani; kuimarisha kilimo cha umwagiliaji; kuimarisha huduma za
utafiti wa mazao ya kilimo na kuhakikisha matokeo ya utafiti yanawafikia
wakulima; kuweka na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kilimo;
kuimarisha usindikaji wa mazao ya kilimo na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya
mazao.
56.
Mheshimiwa Spika, naomba
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tumeamua kwa dhati kusimamia kwa karibu sekta ya kilimo ambayo ndiyo inayoajiri
Watanzania wengi. Tutahakikisha kuwa mkulima ananufaika na kilimo chake kwa
kuwafikishia wakulima pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu kwa wakati; kuimarisha
miundombinu ya kilimo na kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika. Pia,
Serikali itatoa kipaumbele katika kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda kwa
lengo la kuongeza thamani na faida kwenye shughuli za kilimo.
Mifugo
57.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba mifugo bora na ya kisasa ni fursa kubwa ya
kupunguza umaskini hapa nchini. Hata hivyo, ili mifugo hiyo iweze kuleta
matokeo makubwa, hususan upatikanaji wa soko la uhakika ndani na nje ya nchi,
hapana budi mifugo itambuliwe bayana. Kutokana na mahitaji hayo ya utambuzi,
Serikali inatekeleza zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya chapa ya moto
ambapo hadi Februari 2018, ng’ombe 16,408,022 wamepigwa chapa. Idadi hiyo ni
sawa na asilimia 94.4 ya ng’ombe 17,390,090 waliotegemewa kupigwa chapa. Zoezi
hili ni endelevu na ninawaomba wadau watoe ushirikiano wa kutosha kwa Serikali
ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Maliasili na Utalii
58.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa sekta ya
maliasili na utalii katika ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira, Serikali
inaongeza juhudi za kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo misitu, wanyamapori,
malikale, ufugaji nyuki, uvuvi, pamoja na kuhakikisha rasilimali hizo
zinanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Serikali pia
imechukua hatua za kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato katika sekta hizo,
kupambana na ujangili, kuzuia upotevu wa mazao ya misitu na kutatua migogoro ya
mipaka kati ya vijiji na hifadhi.
Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeanza mapitio ya Sera za Taifa za
Utalii, Misitu na Ufugaji Nyuki ili ziendane na mazingira ya sasa na kuimarisha
zaidi ulinzi wa rasilimali hizo.
59.
Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya
utalii, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2017 imeongezeka hadi kufikia
watalii milioni 1.33 ikilinganishwa na watalii milioni 1.28 mwaka 2016. Pia, mapato yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka
2017 ikilinganishwa na Dola za Marekani
bilioni 2.13 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia sita. Takwimu hizo
zinabainisha kwamba, sekta ya utalii ina fursa kubwa ya kulipatia taifa fedha
za kigeni na kuzalisha ajira kwa wingi.
Tutaendelea kuimarisha sekta hii kwa kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha
miundombinu ya maeneo ya utalii pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani, utalii
wa mambo ya kale na kihistoria katika miji ya zamani ikiwemo Bagamoyo, Kilwa na
Mikindani.
Viwanda
60.
Mheshimiwa Spika,
sote
tunatambua kwamba kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi wa
Taifa unaotegemea viwanda. Hadi kufikia mwezi Februari 2018, viwanda vipya
3,306 vimeanzishwa. Aidha, Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa
kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri; kuendeleza na
kuboresha miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji.
Pia, kuhuisha sera, sheria
na kanuni pamoja na kufuatilia
utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki
walioenda kinyume na mikataba ya mauzo. Vilevile, Mikoa na
Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda.
61.
Mheshimiwa Spika, sekta ya hifadhi ya
jamii inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo, pamoja
na miradi mingine, NSSF na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza
wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari mkoani Morogoro. Lengo la
Mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme MW 40. Mradi huo
unatekelezwa katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere lenye ukubwa wa hekta
63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo
Dakawa.
Hadi sasa ekari
2,000 za mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la Mkulazi na ekari 1,100
zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya kwanza ya ufungaji
wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo mwezi Desemba, 2018 ili uzalishaji
uanze mwaka 2019. Miradi hii itakapokamilika itazalisha zaidi ya ajira 100,000.
Aidha, tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu mwezi Juni, 2017 ajira za moja
kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja
24,000 ikijumuisha wakulima wadogo wa mbegu na kilimo cha nje
zimezalishwa.
62.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali
itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo, uanzishwaji wa kanda
maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia
uwekezaji katika sekta ya viwanda. Vilevile, Serikali itaweka msisitizo katika
kubuni mikakati ya uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati.
Madini
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha usimamizi katika sekta ya
madini ili kuiwezesha sekta hiyo kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi,
kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja
na kukusanya taarifa za uzalishaji wa madini, kuimarisha ukaguzi wa uzalishaji
na mauzo kwenye migodi mikubwa na midogo na kufuatilia ukusanyaji wa maduhuli.
Zoezi la ukaguzi limewezesha kukamatwa kwa madini yaliyokuwa yakitoroshwa yenye
thamani ya Dola za Marekani takriban 898,523 na shilingi milioni 557.
64.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Februari,
2018 maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kutoka sekta ya madini yalifikia
shilingi bilioni 180.4. Pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yametokana na
usimamizi makini katika sekta ya madini na uamuzi wa Serikali kufungua soko la Tanzanite nchini. Aidha, Serikali
imeimarisha soko la madini nchini kwa kuhakikisha kuwa madini yanauzwa kwa
ushindani.
65.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, tarehe 20 Septemba 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alielekeza ujengwe
ukuta katika eneo linalozunguka mgodi wa Tanzanite
uliopo Mererani ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi
wa ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 24.5 umekamilika. Nitumie fursa hii,
kuwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
kwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea
kujenga uwezo wa wazawa ili washiriki kikamilifu katika sekta ya madini.
Uwezeshaji huo utakwenda pamoja na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu
teknolojia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kwa lengo la kupunguza athari za mazingira
na maafa katika maeneo ya migodi. Aidha, Serikali itakamilisha taratibu za
kumpata mwekezaji
atakayejenga mitambo ya kuchenjua madini nchini.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
67.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa rasilimali ya
ardhi kama kitovu cha uzalishaji mali, Serikali inachuka hatua madhubuti za
kuiendeleza. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza Mpango Kabambe wa Majiji,
Manispaa na Miji; udhibiti wa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na
uimarishaji wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi nchini. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Mipango Kabambe ya Manispaa za Iringa na
Singida na Mji wa Kibaha imekamilika na mipango mingine 20 ipo katika hatua
mbalimbali za uandaaji. Hadi sasa,
michoro 1,110 ya mipango miji iliidhinishwa kati ya 1,148 iliyopokelewa kutoka
Halmashauri za miji mbalimbali.
Natoa wito kwa
wananchi wote nchini wanapofanya shughuli za maendeleo kuzingatia mipango
kabambe inayoandaliwa na mamlaka za upangaji miji.
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa za
kukabiliana na changamoto ya migogoro ya ardhi miongoni mwa watumiaji ikiwemo
migogoro ya mipaka ya vijiji, wakulima na wafugaji, wanavijiji na hifadhi na
mapori ya akiba. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuunda timu ya kisekta ya
kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo imetembelea Mikoa ya Geita, Kagera,
Katavi, Morogoro na Tabora na kufanya majadiliano na wadau 1,106. Hatua
mbalimbali za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinaendelea kuchukuliwa.
Nishati
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imechukua hatua thabiti kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa kutosha na wa
uhakika kwa ajili ya uchumi wa viwanda.
Hatua zilizochukuliwa zinalenga kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya
usafirishaji wa umeme na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na
mijini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa
ya Kinyerezi I (MW 185), Kinyerezi II (MW 240) na Mradi wa Umeme wa maji wa Mto
Rufiji (Stiegler’s Gorge) utakaozalisha MW 2,100.
70.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imepanua na kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme kwa
kutekeleza miradi mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na: Mradi wa Rufiji -
Chalinze - Dodoma wenye msongo wa kV 400; Mradi wa Singida – Arusha – Namanga
wenye msongo wa kV 400; na Mradi wa Makambako – Songea wenye msongo wa kV 220. Utekelezaji wa miradi hii umeongeza hali ya
upatikanaji umeme nchini kufikia asilimia 67.5. Aidha, uunganishaji umeme kwa
watumiaji umefikia asilimia 49.5.
71.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Awamu ya
Tatu ya Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) ambao umepangwa
kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji
7,873 ambavyo havijapata umeme nchini. Kati ya hivyo, vijiji 7,697
vimepangwa
kupatiwa umeme wa Gridi ya Taifa na vijiji 176 pamoja na visiwa
vitapatiwa
umeme nje ya gridi kwani ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa.
Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaongeza fedha
za mfuko wa REA ili kuhakikisha vijiji vilivyosalia pamoja na taasisi
zinazotoa
huduma za kijamii vijijini zinapata umeme. Serikali pia, itaendeleza
miradi ya
kuunganisha Gridi ya Taifa na gridi za nchi jirani za Zambia, Kenya,
Burundi na
Rwanda.
Bomba la Mafuta (Hoima – Tanga)
72.
Mheshimiwa Spika, tarehe 5 Agosti
2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa
Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni waliweka Jiwe la
Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
bandari ya Tanga. Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi
huo kwa upande wa Uganda ulifanyika katika eneo la Hoima tarehe 11 Novemba,
2017. Bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litakuwa na urefu wa kilometa
1,445 ambapo kilometa 1,115 zitajengwa Tanzania. Mradi huo utakuwa na manufaa
kwa wananchi wa pande zote mbili ambapo ajira takriban 10,000 zitazalishwa
wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1,000 wakati wa uendeshaji wake.
Barabara
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea
kuboresha mtandao wa barabara nchini. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi
Februari 2018, ujenzi wa Km. 776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami
umekamilika na Km. 1,760 zinaendelea kujengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa
Km. 17,054 zimekarabatiwa katika kipindi hicho. Vilevile, ujenzi wa madaraja ya
Kilombero na Kavuu umekamilika na ujenzi wa madaraja ya Sibiti, Mto Mara,
Lukuledi, Ruhuhu, Momba na Mlalakuwa unaendelea. Madaraja mengine 996 katika
maeneo mbalimbali nchini yamekarabatiwa.
74.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea
na jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Hadi kufikia Februari 2018, ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la TAZARA
ulifikia asilimia 70 na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo
(Ubungo Interchange) umeanza. Aidha, maandalizi ya Awamu ya Pili hadi ya Nne ya
Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka yanaendelea. Katika
mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kujenga kilometa 597 za barabara kuu na za
mikoa kwa kiwango cha lami na kilometa 72 za kiwango cha lami zitakarabatiwa.
Barabara za Vijijini na Mijini
75.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency – TARURA) kwa lengo la
kurahisisha huduma za usafirishaji na kuongeza kasi ya wananchi kujiletea
maendeleo. TARURA
imepewa jukumu la kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara zenye
urefu wa kilometa 108,946.2 za vijijini na mijini. Katika mwaka
2017/2018, TARURA imesimamia
matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 4,183.3, madaraja 35, makalavati makubwa 43
na madogo 364 na drift nne. Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa TARURA
kuwaelimisha wananchi, viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuhusu majukumu na mfumo wa utendaji kazi wake.
Reli
76.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) itakayokuwa na urefu wa Km. 1,219. Hadi
sasa, ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye Km. 300
umeanza na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2019. Aidha, tarehe 14 Machi 2018,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha kutoka Morogoro hadi
Makutupora chenye urefu wa kilomita 422. Ujenzi wa reli hii utasaidia kukuza
sekta nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda, madini, utalii pamoja na
kutoa fursa nyingi za ajira. Utekelezaji wa mradi huu unakadiriwa kutoa ajira
30,000 za moja kwa moja na nyingine 600,000 zisizo za moja kwa moja.
Bandari
77.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali
imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu
cha usafiri wa majini. Uboreshaji huo utaanza na Gati Na. 1 – 7; kuongeza kina
na upana wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli; kuimarisha
mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga gati maalumu la kuhudumia meli za
magari. Vilevile, Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua ofisi katika baadhi ya
nchi jirani kwa lengo la kuongeza urahisi wa kutoa huduma. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea na uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga
na Mtwara. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa dirisha moja la forodha
(Tanzania Electronic Single Window System-eSWS) ili kuwaweka pamoja wadau wote
wa kuondosha shehena bandarini na mipakani. Kukamilika kwa mradi huo,
kutarahisisha na kupunguza muda na gharama za utoaji na upitishaji wa shehena
bandarini.
Mawasiliano
78.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali
imeendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa miundombinu ya itifaki
(Internet Protocol – Multiplier Label Switching) pamoja na ujenzi wa kituo cha
kuhifadhi data ambacho hadi sasa
mifumo ya taasisi 27 imeunganishwa ukiwemo mfumo wa ukusanyaji mapato wa TRA.
Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutaongeza usalama, usiri wa data, kujikinga na majanga na
kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na muingiliano wa mifumo katika Kituo
cha Data cha Taifa na vituo vingine
vitakavyojengwa nchini.
79.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa
miundombinu ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini ambapo vijiji 1,921
vimepatiwa huduma hiyo. Aidha, Serikali imeimarisha huduma za simu na intaneti
katika taasisi za umma zikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na
ofisi za posta. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake hadi katika ngazi ya wilaya.
Vilevile, kuendelea kusimamia kampuni za simu nchini ili ziweze kutoa
kumbukumbu sahihi kwa lengo la kukokotoa mapato yatokanayo na malipo ya huduma
za simu za kitaifa na kimataifa.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
80.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio
mpango wa utoaji wa elimu ya awali na elimumsingi bila malipo. Tangu kuanza kwa
mpango huo, Serikali imekuwa inapeleka kwa wakati na moja kwa moja shuleni
fedha zote za ruzuku ya elimumsingi. Kiasi cha shilingi bilioni 20.8
kinapelekwa kila mwezi kwa shule zote za msingi na sekondari nchini,
ikijumuisha fedha za posho maalum kwa Walimu Wakuu, Waratibu wa Elimu Kata na
Wakuu wa Shule.
81.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji mzuri wa mpango wa
elimumsingi bila malipo umechangia kuimarika kwa mahudhurio ya wanafunzi
darasani; kuongezeka kwa ubora wa elimu inayotolewa shuleni kutokana na
kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuongezeka kwa udahili
wa wanafunzi. Kwa mfano, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza
imeongezeka kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,120,667 mwaka 2016, sawa na
ongezeko la asilimia 35.2. Kwa mwaka huu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa
darasa la kwanza ni 2,078,379. Vilevile, wanafunzi waliofaulu mtihani wa
kuhitimu darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kutoka
wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 538,826 mwaka 2016; na mwaka 2017
wanafunzi 562,695 wamechaguliwa kuingia sekondari.
82.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali
imejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari ikiwemo
ukarabati wa shule za sekondari kongwe 89 ili kuboresha mazingira ya shule na
kuinua ubora wa elimu. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza vifaa vya maabara
vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kwa shule za sekondari 1,696 kwa ajili
ya kuimarisha ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa nadharia na vitendo.
Vilevile, walimu 3,347 wa masomo ya sayansi na hisabati na mafundi sanifu wa
maabara 386 wameajiriwa.
83.
Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya kutoa kipaumbele kwenye elimu, imeleta hamasa kubwa kwa wananchi kuchangia
maendeleo ya elimu. Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wananchi na wadau
mbalimbali kuendelea kuchangia kwa hiari maendeleo ya elimu kupitia Ofisi za
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri. Aidha, naziagiza Halmashauri zote nchini
kuratibu na kusimamia ipasavyo michango ya hiari ya elimu inayotolewa na
wananchi na matumizi yake, hususan kwa kuanzisha Mfuko Maalum wa Elimu katika
Halmashauri husika ambao utasimamiwa na Bodi.
84.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015 hadi
shilingi bilioni 483 mwaka 2017. Hatua hiyo imewezesha idadi ya wanaonufaika na
mikopo hiyo kuongezeka kutoka wanafunzi 98,300 mwaka 2015 hadi wanafunzi
119,435 mwaka 2017/2018. Serikali pia inaendelea kujenga na kukarabati
miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu nchini ili kuboresha mazingira ya vyuo
hivyo na kuviwezesha kuzalisha wataalam mahiri wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa
katika soko la ajira. Natoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa
kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na wadau wa elimu kufanya tathmini na
kuboresha mfumo wa ufundishaji wa
wanafunzi wa elimu ya juu nchini ili kuwapatia mbinu zitakazowawezesha
kujiajiri.
85.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu wa mwaka 2017
hadi 2021 pamoja na mpango kazi wake unaolenga kutekeleza vipaumbele vya Mpango
wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Utekelezaji wa mpango huo wa sekta ya elimu utasaidia kuongeza idadi ya
wataalam wenye ujuzi wa kati na wa juu ifikapo mwaka 2021. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya ukarabati wa shule
kongwe, kujenga ofisi za udhibiti ubora katika wilaya mbalimbali nchini,
kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari na kujenga vyumba vya
madarasa katika shule za msingi na sekondari.
Maji
Huduma ya Maji Vijijini
86.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa
wananchi waishio vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji. Katika kipindi cha Julai 2017
hadi Machi 2018, jumla ya miradi 71 imekamilishwa vijijini na mingine
366 inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa miradi hiyo, umewezesha
kuongezeka idadi ya wananchi wanaopata maji vijijini. Pia, Serikali imepanga kubadilisha mitambo
inayotumia nishati ya dizeli kusukuma maji na kufunga mitambo inayotumia
nishati ya jua ili kuwapunguzia wananchi gharama za uendeshaji na matengenezo.
87.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itakamilisha
ujenzi wa miradi ya
maji 387 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuanza miradi mipya ya maji
vijijini; kutekeleza miradi ya maji vijijini katika maeneo kame na yenye shida
kubwa ya maji; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa mabwawa pamoja na upanuzi wa
miundombinu ya maji kutoka kwenye mabwawa na visima vilivyochimbwa. Vilevile,
Serikali itaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika maeneo ya
Tabora, Kigoma na Same - Mwanga- Korogwe.
Huduma ya Maji Mijini
88.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018,
Serikali imejenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo
mbalimbali mijini ili kufikia malengo yaliyowekwa. Juhudi hizo zimewezesha hali
ya upatikanaji wa maji kwenye miji mikuu ya mikoa kufikia wastani wa asilimia
78. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na DAWASA,
upatikanaji wa maji umefikia asilimia 75. Aidha, upatikanaji wa maji katika
miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya kitaifa
umefikia asilimia 60. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kukamilisha
miradi mingi ya maji iliyopo.
Afya
Utoaji wa Chanjo
89.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inasimamia shughuli za utoaji wa chanjo nchini ili kuhakikisha kuwa malengo
yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.
Hadi sasa, Tanzania imefikia kiwango cha juu cha asilimia 97 ya utoaji
wa chanjo ya pentavalent kwa watoto
inayokinga magonjwa ya kifaduro, dondakoo, pepopunda, homa ya ini na mafua.
Kutokana na kufikia kiwango hicho, mwezi Desemba 2017, Serikali ya Tanzania
ilipongezwa na Shirika la Afya Duniani kwa hatua hiyo kubwa. Lengo la Shirika
la Afya Duniani ni kila nchi kufikia kiwango cha uchanjaji wa asilimia 90.
90.
Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo
yamefikiwa kutokana na usimamizi madhubuti wa Serikali katika utoaji wa chanjo.
Niwapongeze sana viongozi na watendaji wa sekta ya afya pamoja na mamlaka zote
zinazohamasisha na kutoa huduma za chanjo hapa nchini.
Upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba
91.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na
vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya. Bajeti kwa ajili
ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
imeongezwa kutoka shilingi bilioni 252 mwaka 2016/2017 na kufikia shilingi
bilioni 269 mwaka 2017/2018. Kutokana na ongezeko hilo, upatikanaji wa aina 135
ya dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini umeimarika na
kufikia asilimia 89.6.
Huduma za Tiba za Kibingwa
92.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha na
kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini. Huduma
zilizoimarishwa ni pamoja na upandikizaji wa figo na vifaa vya
kuongeza usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji kwa
kutumia
tundu dogo na kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Vilevile, Serikali imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya
katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambapo dawa zinapatikana na muda wa
kupata
huduma ya mionzi ya saratani umepungua. Kutokana na
maboresho hayo, idadi ya wagonjwa waliopewa rufaa ya matibabu nje ya
nchi
imepungua kutoka wagonjwa 304 mwaka 2016/2017 na kufikia 103 mwaka
2017/2018.
Hatua hiyo imesaidia kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali ingetumia
kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.
ULINZI NA USALAMA
93.
Mheshimiwa Spika, hali ya mipaka ya
nchi yetu ni salama. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuliimarisha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutoa mafunzo na mazoezi ya kijeshi,
kulipatia vifaa, zana, mitambo bora na ya kisasa pamoja na kuweka na kuimarisha
miundombinu muhimu na ya kimkakati ili kuliwezesha jeshi kutekeleza jukumu lake
la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Vilevile, Serikali imeweka alama za mipakani
ili kuimarisha ulinzi na kulinda vema mipaka ya nchi. Aidha, Jeshi la Wananchi
linashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mamlaka za kiraia na
mataifa mengine kupambana na matishio mapya ya kiusalama yakiwemo ugaidi, uharamia,
uhamiaji haramu, biashara haramu za dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa
binadamu.
94.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu limeendelea kudumisha
ushirikiano na nchi nyingine duniani kupitia mafunzo ya pamoja na operesheni za
kikanda na kimataifa chini ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Katika
kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani, tarehe 7 Desemba 2017 nchi yetu
ilipoteza askari 15 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mashambulizi
mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa askari wetu wanaolinda amani. Kwa mara
nyingine, naomba kuungana na Mheshimiwa Rais na Watanzania wote kuzipa pole
familia za mashujaa hawa waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi wa
amani. Licha ya changamoto zinazojitokeza, Tanzania itaendelea kushirikiana na
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani
kwenye nchi mbalimbali duniani ili kuendelea kuifanya dunia kuwa mahala salama
pa kuishi pamoja na kuyaongezea majeshi yetu uzoefu na mbinu za kisasa za ulinzi wa amani.
95.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
usalama wa raia, Serikali imelipatia Jeshi la Polisi vitendea kazi muhimu
ikiwemo vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uchunguzi ili liweze kupambana na
ujambazi na matukio mengine ya kihalifu nchini. Aidha, imejenga Kituo cha
Kisasa cha Mawasiliano (Call Centre) Dar es Salaam ambacho kinawezesha wananchi
kutoa taarifa ya matukio hayo kwa urahisi. Pia Serikali imehamasisha jamii
kushiriki katika ulinzi wao na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
lengo la kuwapatia taarifa za wahalifu na uhalifu. Natoa wito kwa wananchi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola ili
kudhibiti matukio ya kihalifu nchini.
96.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
mradi wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration)
ambapo mwezi Januari 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Pasi Mpya ya Kusafiria ya
Kielektroniki ya Kimataifa ya Afrika Mashariki. Kuzinduliwa kwa pasi hii
kutapunguza vikwazo vya kusafiri mipakani baina ya raia wa nchi wanachama,
kuimarisha mahusiano na kuchochea shughuli za kiuchumi miongoni mwa raia wa
Jumuiya hii. Natoa rai kwa Watanzania kuanza kutumia pasi hii na kuendelea
kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, ajira na elimu
zinazopatika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
97.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hiyo, Serikali
imedhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa sababu
mbalimbali. Aidha, ofisi tisa mpya za uhamiaji zimefunguliwa katika wilaya za
Gairo, Iramba, Kakonko, Kilosa, Kiteto, Manyoni, Mvomero, Siha na Songwe kwa
lengo la kuongeza udhibiti wa wahamiaji haramu. Katika mwaka 2018/2019,
Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa uhamiaji mtandao.
BUNGE
98.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2017/2018, kumekuwa na mikutano mitatu ya Bunge ambapo masuala mbalimbali
yalijadiliwa na kutolewa ufafanuzi na Serikali. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge,
Mkutano huu wa Bajeti utakuwa unahitimisha idadi ya mikutano minne ya Bunge kwa
mwaka huu wa fedha unaoishia Juni, 2018. Katika mikutano mitatu iliyopita,
maswali ya msingi 359 na maswali ya nyongeza 1,002 yaliulizwa na Waheshimiwa
Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, katika utaratibu wa maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu, maswali ya msingi 17 pamoja na mawili ya nyongeza
yaliulizwa na kujibiwa. Miswada 15 ya Sheria ya Serikali iliwasilishwa,
kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
99.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Bunge liliratibu na
kusimamia shughuli za vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za hansard, utafiti, utawala na kutoa
mafunzo kwa Waheshimiwa wabunge na watumishi wa Ofisi ya Bunge. Pia, Bunge
lilijadili na kuridhia Maazimio matano yanayohusu utekelezaji wa Mikataba ya
Kimataifa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge
kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
MAHAKAMA
100. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kutoa kipaumbele katika kuongeza ufanisi wa utendaji wa mhimili wa Mahakama
nchini. Katika mwaka 2017/2018, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri
494,525 kati ya 513,329, sawa na asilimia 96.3 ya mashauri yote katika ngazi
zote za Mahakama. Hatua hii imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri katika
mahakama zetu. Hali kadhalika, katika kipindi hicho Serikali imekamilisha
ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Mara. Aidha,
Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Wilaya na za Mwanzo
katika maeneo mbalimbali nchini.
MASUALA MTAMBUKA
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali
101.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali ilizindua Mfumo wa
Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Shughuli za Serikali. Mfumo huo
unalenga kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali na kuiwezesha
Serikali kufanya tathmini ya utoaji huduma kwa wananchi na mipango ya
maendeleo. Mfumo huo umeanza kufanya kazi ambapo kwa sasa Wizara zote
zinawasilisha utekelezaji wa shughuli zao kupitia mfumo huo. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaimarisha matumizi ya mfumo huo hasa katika ngazi za
Mikoa na Halmashauri na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.
Hifadhi ya Mazingira
102. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza jukumu la usimamizi na
uhifadhi wa mazingira nchini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeongeza hamasa
na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika suala la usafi, utunzaji na uhifadhi
wa mazingira katika maeneo yote ikiwemo makazi yao. Hatua hiyo imetokana na ushiriki mkubwa wa viongozi wa kitaifa,
mikoa na watendaji wa ngazi zote katika shughuli za usafi na uhifadhi wa
mazingira.
103. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi ya
mazingira nchini, Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira kutoka 62
hadi kufikia 512. Aidha, kaguzi 380 zimefanyika kwenye viwanda kwa lengo la
kufanya tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji
endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji bora wa mazingira.
104. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza
katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili, napenda kusisitiza kwamba halmashauri
zote nchini ziweke mpango mahsusi wa kuhifadhi mazingira unaojumuisha kupanda
na kutunza miti. Serikali itaweka utaratibu wa upimaji wa utendaji wa wakuu
wote wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri unaozingatia
uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
105.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018,
Serikali imeimarisha utendaji wa Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuipatia wataalamu, vifaa
na
kuongezea fedha. Aidha, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya ya
mwaka 2015, imefanyiwa marekebisho ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza
katika
utekelezaji wake. Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola,
ilikamata jumla ya watuhumiwa 11,071 na kati yao, watuhumiwa 3,486 ni
wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao walifikishwa mahakamani.
Watuhumiwa wengi waliokamatwa, walijihusisha na
dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na heroine.
106.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, jumla ya tani moja na kilo 561.28 za dawa aina ya heroin zilikamatwa. Kati ya hizo, kilo
196.28 zilikamatwa kwenye eneo la maji ya Tanzania na nchi kavu na tani moja na
kilo 365 zilikamatwa kwenye bahari kuu kwa kushirikiana na washirika wa
kimataifa na kuteketezwa. Aidha, kilo 5.2 za cocaine, tani 47.7 za bangi na tani 7.4
za mirungi zilikamatwa. Mamlaka pia ilikamata lita 304,513 za vimiminika vya
kemikali bashirifu na kilo 22,143 za kemikali bashirifu yabisi. Katika
operesheni za uteketezaji wa mashamba ya bangi na mirungi, ekari 572.75 za
bangi na ekari 64.5 za mirungi ziliteketezwa.
107. Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia
methadone katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke jijini Dar es Salaam.
Vilevile, Serikali
imeanzisha vituo vipya vya tiba hiyo ili kuwafikia waathirika wengi zaidi nchini
ambapo kliniki saidizi za kutibu waathirika wa dawa za kulevya zimeanzishwa
katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mbeya na Mwanza. Hadi kufikia Januari
2018, zaidi ya watumiaji 5,560 walikuwa wakipatiwa huduma za tiba ya methadone katika vituo mbalimbali
nchini. Serikali pia imekuwa ikisimamia uanzishwaji wa nyumba za upataji nafuu
(Sober House) ambazo hadi sasa idadi yake ni 22. Aidha, mwezi Februari 2018,
Serikali ilizindua mwongozo wa uendeshaji wa sober houses unaolenga kuwawezesha wamiliki wa nyumba hizo
kuwasaidia waathirika hao ipasavyo.
108.
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2018, nchi yetu
ilishiriki katika Mkutano wa 61 wa Kimataifa wa Commission for Narcotic Drugs (CND) uliofanyika Vienna, Austria na
kushirikisha zaidi ya nchi 150. Katika mkutano huo, Tanzania ilitambuliwa kama
nchi ya mfano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya barani Afrika na kupewa
heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Vyombo vinavyopambana na
Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani (HONLEA) kutoka Afrika, utakaofanyika
Septemba 2018. Mkutano huo utatoa fursa kwa wataalam nchini kubadilishana
taarifa, uzoefu, kujenga mahusiano na kujifunza mbinu zinazotumiwa na nchi
nyingine katika kukabiliana na dawa za kulevya.
109. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa
viongozi na watendaji kuwaelimisha vijana kuhusu madhara yatokanayo na matumizi
ya dawa za kulevya. Aidha, wananchi waendelee kushirikiana na Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kutoa taarifa kuhusu
wanaojihusisha na dawa hizo. Pia ni vema wazazi, walezi na jamii kuwa karibu na
vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili kuwaepusha kuingia kwenye mkumbo wa
matumizi ya dawa za kulevya.
Vita dhidi ya Rushwa
110.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea
kupambana na rushwa pamoja na ufisadi. Katika kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya majalada 325
yalifanyiwa uchunguzi na TAKUKURU na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka
ambapo majalada 214 kati ya hayo yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa
mahakamani.
Aidha, kesi 727 ziliendeshwa mahakamani na kesi 219
ziliamuliwa na watuhumiwa 138 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Kutokana na
operesheni zilizofanywa na TAKUKURU katika maeneo ya ukusanyaji mapato, uzuiaji
wa malipo hewa na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni
58.4 ziliokolewa na kurejeshwa Serikalini.
111.
Mheshimiwa Spika, TAKUKURU pia imefuatilia miradi ya
maendeleo 195 yenye thamani ya shilingi bilioni 154.1 katika sekta za elimu,
afya, maji na ujenzi ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kama
zilivyokusudiwa na thamani ya fedha inapatikana. Katika ufuatiliaji huo, miradi
73 yenye thamani ya shilingi bilioni 30.9 ilibainika kuwa na kasoro katika
utekelezaji wake. TAKUKURU imetoa mapendekezo ambayo yanafanyiwa kazi na
Serikali na tayari hatua za kinidhamu na kisheria zimechukuliwa kwa wahusika.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
112. Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhamiria kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika jamiii.
Ili kutekeleza azma hiyo, Mpango wa Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama
kwenda kwa Mtoto umepewa kipaumbele. Aidha, elimu ya UKIMWI imetolewa kupitia
vyombo vya habari, majarida na vipeperushi. Vilevile, elimu imetolewa kwa
kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu rika pamoja na kuwashirikisha
viongozi na watu mashuhuri, viongozi wa dini, sekta binafsi na kutekeleza
programu za kupambana na UKIMWI mahali pa kazi.
Kutokana na juhudi hizo, matokeo ya utafiti uliofanyika katika ngazi
ya kaya kuanzia mwezi Oktoba 2016 hadi Agosti 2017 yanaonesha kuwa wastani wa
kitaifa wa maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni
asilimia 4.7. Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba kiwango cha maambukizi
mapya ya VVU kwa mwaka ni asilimia 0.27.
113.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa huduma kwa wananchi wanaoishi na
virusi vya UKIMWI (WAVIU) nchini. Hadi kufikia Septemba 2017, WAVIU 972,127
sawa na asilimia 70 ya WAVIU wote walikuwa wanapatiwa dawa za kufubaza makali
ya VVU (ARV’s). Katika mwaka 2017/2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau
wamechangia zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwenye Mfuko Maalum wa UKIMWI ili
kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili. Katika mwaka 2018/2019, Serikali
itaanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka
2018/2019 hadi 2022/2023. Vilevile, kampeni maalum za kushawishi wanaume
kushiriki katika kupima afya zao na vijana kujitambua zitaendeshwa.
Uratibu wa Maafa
114.Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa
kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa
kukabiliana na maafa pindi yanapotokea. Aidha, mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za
mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa taarifa za tahadhari za awali ili
kupunguza madhara ya maafa umeboreshwa. Serikali pia imekamilisha kusimika
mashine 36 za kisasa za kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika wilaya
mbalimbali nchini pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa hali ya hewa.
Jitihada hizi zimeongeza uhakika wa utabiri wa hali hewa nchini kufikia
asilimia 87.
115.Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa maafa
kupitia Umoja wa Afrika na jumuiya za SADC, EAC na IGAD. Ushirikiano huo,
umewezesha nchi wanachama kubadilishana taarifa za kuandaa utabiri wa hali ya
hewa na matumizi yake katika kupunguza madhara ya maafa. Vilevile, nchi hizo
zinabadilishana uzoefu pamoja na kutoa mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa
wataalam wa nchi wanachama. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea
kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na Wilaya na kuratibu
shughuli za kupunguza madhara ya maafa na misaada ya kibinadamu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru
116. Mheshimiwa Spika, Serikali iliratibu mbio za Mwenge wa Uhuru kwa lengo la kukuza mshikamano
na kuhimiza shughuli za maendeleo. Katika mbio hizo ambazo kilele chake
kilikuwa tarehe 14 Oktoba 2017 Mjini Magharibi Zanzibar, miradi 1,512 yenye
thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.06 iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa. Kati ya miradi hiyo,
miradi 150 yenye thamani ya shilingi bilioni 568.8 ilikuwa ya viwanda. Uzinduzi wa mbio za mwenge kwa mwaka 2018 ulifanyika
mkoani Geita tarehe 2 Aprili 2018 na kilele chake kitafanyika mkoani Tanga,
tarehe 14 Oktoba 2018. Ninawasihi wananchi kushiriki kwa wingi wakati wa mbio
za Mwenge wa Uhuru kwani zinalenga kuleta umoja na mshikamano kwa wananchi
pamoja na kuhimiza shughuli za maendeleo.
MAHUSIANO YA KIMATAIFA
117. Mheshimiwa Spika, jukumu la kuimarisha mahusiano na
mataifa mengine duniani, mashirika ya kimataifa na washirika wetu wa maendeleo
limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali katika kutekeleza Sera yetu ya Mambo
ya Nje. Katika kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi, Serikali inafanya mapitio
ya Sera ya Mambo ya Nje ili iweze kukidhi mahitaji na matakwa ya sasa ya
Tanzania katika kushughulikia siasa za kimataifa na diplomasia pamoja na
masuala ya mtangamano wa kikanda na kuendeleza Umoja wa Afrika.
118. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa
kuvutia wawekezaji na watalii; kutafuta
fursa za mafunzo; kuendelea kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni
kuchangia katika maendeleo ya nchi yao pamoja na kutafuta ajira na masoko ya
bidhaa za Tanzania nje. Aidha,
Serikali itaimarisha sera ya ujirani mwema kwa lengo la kukuza mahusiano
na kufungua milango ya ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya
kipaumbele hususan, reli, barabara,
nishati na biashara na majirani zetu.
Vilevile, Serikali itatoa msukumo kwa Mabalozi kutumia ushawishi wao
kuitangaza vyema
miradi ya kipaumbele na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini na kutangaza lugha
ya Kiswahili ambayo ikitumika vizuri inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa
Watanzania.
HITIMISHO
119.Mheshimiwa Spika, wananchi wanashuhudia mafanikio makubwa ya
kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi cha takriban miaka miwili na nusu
tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie
madarakani. Mafanikio hayo yanatoa matumaini kwa Watanzania kwamba yale
yaliyoahidiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano yatatekelezwa.
120.Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya Mpango na
Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali pamoja na mambo mengine, itaweka mkazo
katika kudhibiti upotevu wa mapato; kuimarisha mfumo wa kukusanya mapato
hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kudhibiti matumizi ya fedha na
rasilimali nyinginezo za umma. Aidha, msukumo utawekwa katika kuhimiza
uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi ya
maendeleo.
121. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge lako
Tukufu tarehe 20 Novemba 2015, pamoja na mambo mengine aliweka wazi dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kutengeneza
ajira nyingi kwa Watanzania.
Ili kufikia azma
hiyo, Serikali itaendelea kufanya yafuatayo:
Mosi: Kuimarisha na
kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta
maendeleo endelevu;
Pili: Kuboresha
mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na utoaji huduma;
Tatu: Kujenga miundombinu
muhimu ikiwemo reli, bandari, viwanja vya ndege, barabara na madaraja;
Nne: Kuimarisha
uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika sambamba na kuongeza kasi ya
upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi na viwanda;
Tano: Kusimamia viongozi
na watendaji wote ili kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia
wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote; na
Sita:
Kusimamia
kikamilifu rasilimali zilizopo ili zitumike kwenye maeneo yanayochochea ukuaji
uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi.
122. Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa kila mwananchi kuendelea
kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu uaminifu na kupiga vita
rushwa.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2018/2019
123.Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/2019, Ofisi ya Waziri Mkuu
na Taasisi zilizopo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya
Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Nne, Milioni Mia Tisa Hamsini na Nne, Mia
Mbili Thelathini Elfu na Mia Sita Tisini
na Nane (Shilingi 124,954,230,698). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sitini na Sita, Milioni
Mia Moja Sitini na Mbili, Mia Saba Themanini na Tisa Elfu na Mia Sita Tisini na
Nane (Shilingi 66,162,789,698) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Hamsini na Nane,
Milioni Mia Saba Tisini na Moja, Mia Nne Arobaini na Moja Elfu (Shilingi 58,791,441,000)
ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
124. Mheshimiwa Spika, vilevile, naliomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Ishirini na Tano, Milioni Mia Tano Ishirini na Moja, na Mia
moja Elfu (Shilingi 125,521,100,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya
fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja
Kumi na Saba, Milioni Mia Mbili na Tano, Mia Nne Themanini na Saba Elfu (Shilingi
117,205,487,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Tatu
Kumi na Tano, Mia Sita Kumi na Tatu Elfu (Shilingi 8,315,613,000) ni kwa ajili
ya Matumizi ya Maendeleo.
125.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
0 comments:
Chapisha Maoni