NA BASHIR NKOROMO
Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka amewataka Wanawake
kote nchini wasione fahari kuitwa ‘Dume-Jike’ bali wawe wanawake wenye
msimamo imara na jasiri kwa maendeleo yao na ya nchi kwa jumla.
Gaudentia
ameto mwito huo, wakati akiwasilisha salaam maalum za pole kwa ndugu
jamaa, marafiki na hasa wanawake wote hapa nchini na duniani kote
kufuatia kifo cha Winnie Mandela aliyemwelezea kuwa alikuwa amwanamke
shupavu katika kupigania haki na vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini
Afrika Kusini.
“Tazama
Winnie Mandela alikuwa mpambanaji hata kabla ya kuwa mke wa Rais Nelson
Mandela, kwa hiyo tukiangalia historia yake tunabaini kuwa hakuhitaji
msukumo wa nguvu za mwanaume katika kuonyesha ushupavu wake”, alisema.
Alisema
Winnie Mandela aliyefariki dunia Aprili 2, mwaka huu, aliendelea
kuonyesha ushupavu wake katika kupambana na udhalimu na ubaguzi wa rangi
nchini Afrika Kusini hata wakati Mandela akiwa gerezani
“Winnie
atakumbukwa na Watanzania na dunia nzima kwa ujasiri wake pia
atakumbukuwa kwa umaarufu alioupata hata akiwa bado mwanafunzi, msichana
kabla ya kuolewa. Alichukia kuona Mwafrika anabaguliwa, anatengwa
asifike kwenye maeneo walipokuwa weupe. Kwa hiyo umaarufu wa Winnie
haukutokana tu kwa kuwa ni mke wa Rais yaani “First lady “ lakini
umarufu wake ulikuwa wa kwake mwenyewe. Alijitambua, akajiamini,
akatimiza wajibu wake kama Binadamu, kama Mwafrika, baadaye kama Mke,
Mama, Mwanasiasa na Kiongozi” alisema Gaundetia
“Wanawake
wa Tanzania hasa wanasiasa tuna mengi ya kujivunia na kujifunza kutoka
kwa mwana mama huyu mtoto wa Afrika. Tumejifunza kuishi sisi wenyewe na
sio kutegemea tufanyiwe, tupendelewe ndipo tuonekane tunaweza.
Tunatambua
uwezo tulionao wanawake lakini pia tuwe wastahimilivu tunapokumbana na
magumu tupambane hadi mwisho. Kama Winnie Madikizela Mandela aliweza
kutetea Waafrika wenzake hata baada ya mume wake kufungwa; kwa sababu
hiyo kwa nini sisi wengine tusiweze kujitokeza waziwazi na kuiunga
Serikali na Rais wetu Dk. John Magufuli katika juhudi zake za kupiga
vita ufisadi, wizi wa mali ya umma, kutowajibika”, Alisema Gaudentia.
“Wanawake
wa Tanzania na wa Afrika nzima tunapomlilia Winnie Mandela kwa nini
tusiige ujasiri wake kwa kukemea bila woga tabia mbaya kama mahusiano ya
jinsia moja, ubakaji na utumiaji dawa ya kulevya, katika jamii yetu.
Wanawake wa Tanzania tumapomlilia Winnie Mandela kwanini tusijitokeze
waziwazi kupinga mfumo dume unaoendelea kwenye baadhi ya maeneo hapa
nchini kwetu na kusababisha kina mama kutojiamini”, alisema.
Alisema,
kama Winnie Mandela alivyotimiza wajibu wake katika harakati za
Waafrika kuing’oa Serikali dhalimu ya kibaguzi nchini Afrika kwa nafasi
yake kama mwanamama, na wanawake wa Tanzania kila mmoja kwa nafasi yake
wanaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini.
“Tunafahamu
kuna wanawake wa nchi yetu ambao wameonyesha ujasiri kama huo wa
Winnie Mandela wakiiwakilisha nchi yetu Kimataifa. Sisi UWT tunajiandaa
kuwatambua hivi karibuni, nia yetu ni kutambua michango yao wakiwa
wanafanya kazi nje ya nchi yetu na hivyo wametuleta sifa wanawake wa
Tanzania, lakini pia kuwatia moyo wengine watimize wajibu wao, Alisema
Gaudentia.”, alisema Gaudentia.
Akizungumzia
mrejesho wa ziara aliyoifanya hivi karibuni aliwapongeza wanawake
wanaowajibika ipasavyo Mijini na Vijijini hapa nchini akisema yeye na
timu yake walitembelea Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Nyanda ya Juu
Kusini na kubaini kuwa wanawake ni wajasiriamali wazuri, ni wakopaji na
walipaji wazuri na kuzitaka Halmashauri kuwapa mikopo wanawake hao ili
wapanue shughuli zao za ujasiriamali na kwamba hicho ndicho kilio chao
kikubwa, akihimiza halmashauri hizo kutenga asilimia kumi ya mapato ya
ndani.
“Tunapenda
ifahamike kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mwelekeo wa Sera zake
kwa Mwaka 2010 – 2020 na Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020 kwa
pamoja zimeweka msisitizo wa kuyawezesha makundi Maalum ikiwemo
Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu na katika kutekeleza maelekezo
CCM, Serikali imeshatoa Maelekezo kwa Halmashauri za Majiji, Manispaa,
Wilaya na Miji Midogo kutenga asilimia kumi za makusanyo yao ya ndani
kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Alisema Gaudentia na
kungeza;
“Tunapenda
kuwakumbusha wale wote wenye dhamana katika Mamlaka hizi kwamba ni
Maelekezo ya CCM kutoa bila kukosa fedha hizi ili kuwawezesha wananchi
katika makundi haya muhimu. Kuanzia sasa UWT itafuatilia kwa ukaribu
suala hili na hatutasita kupendekeza kwa Mamlaka za uteuzi kuchukuliwa
hatua za kinidhamu kwa wale wote wanaosuasua au kutenga kutoa fedha hizi
ili kujihakikishia kuwa wanawake hawa wachapakazi wapate mahali pa
kupata mikopo kwa bei nafuu kwa maana ya riba nafuu”.
“Tunawaomba
Maafisa Maendeleo ya Jamii watimize wajibu wao wa kutembelea vikundi
vya wakina mama ili kuwapatia elimu ya kujisajili, Kuendesha shughuli
zao, Kupata mikopo ya Halmashauri, Kupata mikopo kutoka benki kwa wale
watakaoweza. Tunawapongeza Wakurugenzi na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii
ambao tulikuta wanatimiza wajibu wao kikamilifu, kwa mfano, Mkurugenzi
wa Maendeleo Halmashauri ya Chunya ambayo inaongozwa na Wanawake (Mkuu
wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Maendeleo ya Jamii) ndiyo
Halmashauri ya mfano kwa kutenga asilimia kwa wanawake, pia Halmashauri
ya Njombe (V) inaongozwa na Mwanamke na ina fanya vizuri ikifuatiwa na
Halmashauri ya Mufindi”, alisema Daudentia.
Kuhusu
Maadili, Gadentia alisema UWT wataendelea kukemea maadili
yaliyoporomoka kwa vijana wa kike na wa kiume jambo ambalo ni hatari kwa
kizazi kijacho na kuhumiza wazazi na walimu kukemea uvunjaji wa Maadili
na hasa mimba za utotoni.
“UWT
inashauri kwenye maeneo tunakoishi ambako kuna Kamati mbalimbali kama
vile polisi jamii na nyingine, Jamii iongeze Kamati ya za Maadili
zitakazosimamia maadili kwa vijana wa kike na wa kiume kwa kila Kata,
ambazo zitakuwa na wajumbe wafuatao, Viongozi wa Dini zote, Madiwani wa
Kata na Viti Maalum, Wazee na watu wazima wanaoishi ndani ya Kata hizo,
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata. Kamati hizo zisimamie kikamilifu
zoezi hilo na viongozi waliotajwa hapo juu na ikibidi watakaokiuka
wachukuliwe hatua za kinidhamu kama wahalifu wengine”, alisema Gaudentia
Alisema,
baada ya kukamilisha ziara hiyo UWT iliandaa Mafunzo ya kuwajengea
uwezo na uelewa wa pamoja Viongozi na Watendaji wa UWT wa ngazi ya
Wilaya na Mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini. Mafunzo hayo yalifanyika
tarehe 26 – 27/03/2018 katika Mkoa wa Mbeya na kwamba ziara na mafunzo
haya yataendelea kufanyika katika Mikoa yote.
0 comments:
Chapisha Maoni