Askofu
wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe
amesema yeye siyo unyasi unaotikiswa na upepo.Amesema hata kama yeye na
kanisa lake watapitishwa kwenye magumu, atashinda zaidi.
Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa inatokana na wito wa Idara ya Uhamiaji, ambako ametakiwa kwenda kuhojiwa leo.
Askofu
Kakobe akiwahubiria waumini wake jana katika Ibada ya Jumapili
iliyofanyika kanisani kwake, aliwataka waumini hao kutoishi maisha ya
unyasi yanayotikiswa na upepo bali wasimame imara kila wakutanapo na
changamoto.
Kiongozi
huyo ambaye leo anatarajiwa kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar
es Salaam baada ya kuandikiwa barua ya wito Aprili 5, ikimtaka afike
katika ofisi hiyo saa 4:00 asubuhi, alisema hata wafanye nini atasimama
imara kwa sababu wokovu wake siyo wa dhahabu bandia.
“Hata
wafanye nini, mimi siyo nyasi unaotikiswa na upepo... katika hayo yote
nitashinda zaidi ya ushindi. Kanisa langu siyo la kuombea watu na
kuwaponya magonjwa, hili ni kanisa ambalo hata likipita kwenye magumu
kama Ayubu na Lazaro halitikisiki,” alisema.
Pia,
Askofu Kakobe aliwataka waumini wake wasiyumbishwe na changamoto
zinazojiinua katika maisha yao kwa lengo la kuharibu uhusiano wao na
Mungu.
Akitolea
mfano wa mtumishi wa Mungu, Lazaro na Ayubu namna walivyopitishwa
kwenye majaribu, alisema kuna maisha ya binadamu ambayo watu wa Mungu
wanapitishwa kwenye mambo magumu ili kupima imani zao.
“Shetani
anamuogopa mtu anayemcha Mungu, hufanya kila njia ili kumuyumbisha
aachane na Mungu. Tunapopita katika magumu, tuige mfano wa Ayubu ambaye
mbali na kuyumbishwa na shetani alisimama imara katika imani, tuige
imani hii,” alisema.
Askofu
Kakobe aliwaambia waumini wake kuwa wasiwe walokole ambao wakitikiswa
kidogo wanayumba, bali wawe imara kupambana na mawakala wa shetani
wanaojiinua ili kufifisha Kanisa la Mungu.
“Tusiwe
watu ambao hatuwezi kusimama katika imani eti kwa sababu hatuna mali.
Mali zetu zimeondoshwa lazima tupite katika moto ili tuwe dhahabu mbele
za Mungu,” alisema.
Alisema
hakuna mamlaka wala utawala wowote utakaoweza kuwatenga na Kristo kama
watasimama imara katika imani na kuwataka wasiwe dhahabu bandia.
Askofu Kakombe mbali na kuitwa uhamiaji, amekuwa kwenye misukosuko baada ya kutamka kuwa ana utajiri mkubwa kuliko Serikali.
Kufuatia
kauli hiyo wakati wa mkesha wa sikukuu ya Krismasi Desemba mwaka jana,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianza kumchunguza juu ya uhalali wa
utajiri wake na akaunti zake na watoto wake na kubaini kuwa fedha
zilizopo zinatokana na michango, zaka na sadaka za kanisa.
Pia,
ripoti ya uchunguzi ya TRA ilibainisha kuwa Askofu Kakobe mbali na
kupeleka fedha benki kuna fedha huwa zinahifadhiwa kwenye majaba na ndoo
na kwamba, kanisa hilo lilikwepa kulipa kodi Sh20.8 milioni katika
shughuli zake za kiuchumi, lakini zililipwa baada ya uchunguzi.


0 comments:
Chapisha Maoni