Wakati
uongozi unaosimamia barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT), ukipiga
marufuku magari ya wagonjwa na polisi kutumia barabara hizo, Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema
watalazimika kuzitumia barabara hizo wakati wa dharura.
Barabara za mabasi yaendayo haraka zimejengwa kwa ajili ya kutoa huduma zake kwenye barabara za Morogoro na Kawawa.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imesisitiza kuwa hakuna chombo
chochote cha moto kitakachoruhusiwa kupita katika barabara hizo zaidi ya
mabasi ya mwendokasi.
Akifafanua
zaidi taarifa hiyo, mkurugenzi wa wakala wa mabasi hayo (Dart), Ronald
Lwakatare alisema ni kweli magari ya wagonjwa hayaruhusiwi kupita katika
barabara hizo mpaka ruhusa ya polisi wa usalama barabarani.
Katika
kusimamia sheria za barabara hizo, alisema zipo kanuni na taratibu
mbalimbali ikiwamo sheria za barabarani, halmashauri na nyinginezo.
“Ieleweke
kwamba ni marufuku kutumia barabara hizo na mtu yeyote, kwani
zimetengenezwa kwa ajili ya magari hayo tu na kama ikatokea likapita
basi iwe ni kwa ruhusa ya polisi wa usalama barabarani ambao wao wanajua
ni muda gani na sababu gani ya kuyaruhusu magari mengine
yapite,”alisema Lwakatare.
Pia
mkurugenzi huyo alisema tayari Rais (John Magufuli) alishatoa maagizo
ya magari yafanywe nini inapobainika kutumia njia hizo na kuwataka
wanachi kuwa makini ili kuepuka kuingia katika matatizo
yatakayowapotezea mali na muda wao bila sababu za msingi.
Taarifa
hiyo imeeleza pia kuwa magari ya vyombo vya ulinzi na usalama
yanapopita katika barabara hizo, huchangia kwa kiasi kikubwa magari ya
watu binafsi kufanya hivyo.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa kuanzia jana hakuna gari lolote litakaloruhusiwa
kupita kwenye barabara hizo na kwamba hata magari ya wagonjwa
hayaruhusiwi kwa kuwa yana utaratibu wake uliozoeleka sehemu zote
duniani.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa kuna baadhi ya magari ya wagonjwa hasa yanayotokea
mjini kwenda Kimara yamekuwa yakitumia barabara hizo bila kubeba abiria
kwa kigezo cha kupitisha wagonjwa.
Jana, Mambosasa alisema anawaunga mkono BRT, lakini polisi itatumia barabara hizo endapo watakuwa na dharura.
“Kama hatuna dharura tutapita barabara za kawaida. Lakini tukiwa na dharura tutapita barabara zote,”alisema Kamanda Mambosasa.
0 comments:
Chapisha Maoni