Na Rehema Isango, Tarime, Mara
Timu
za watalaamu wa upimaji ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Tanzania na taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini
Kenya zimekutana wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuanza
utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina
ya nchi hizi mbili.
Mapema
mwezi Machi, Naibu Waziri wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.
Angeline Mabula alitangaza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuanza kuimarisha mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na
Uganda baada ya ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika
Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.
Hatua
ya uhakiki na uimarishaji wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na
mpaka huu kuwa wa siku nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia
baadhi ya alama hizo kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo
kusababisha Serikali pande zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli
za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama.
Katika
uimarishaji wa alama hizo za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya
ndogo zinazoonana kwa umbali wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la
ardhi huru kwa kila upande wa nchi (buffer zone).
Mpaka
kati ya Tanzania na Kenya una jumla ya urefu wa Kilommita 760 kuelekea
bahari ya Hindi ambapo awamu ya kwanza ya kazi ya uimarishaji mpaka
inayofanyika hivi sasa itahusisha urefu wa Kilomita 238 kutoka kando ya
Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.
Baadaye,
kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka itaendelea katika mikoa ya
Kilimanjaro na Tanga na kisha itafanyika katika maeneo yote yanayohusika
na mipaka ya kimataifa nchini.
Uimarishaji
wa mipaka ya kimataifa nchini umefanyika mara ya mwisho mwaka 1975 kwa
kurudishia alama ambazo ziliondolewa na kuongeza nyingine mpya kwa
kuzingatia alama zilizopo.
Mbali
na Kenya nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ni; Msumbiji, Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja
na visiwa vya Komoro na Shelisheli.
0 comments:
Chapisha Maoni