Na Thobias Robert-Maelezo
Serikali
imesema kuwa itaendelea kushirikiana na umoja wa mataifa katika kuleta
maendeleo, katika sekta za kiuchumi na kijamii, kulinda amani,
kuimarisha sekta ya viwanda na kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi
kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Hayo
yamebainishwa jana Oktoba 24 Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya
Karimjee na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia
Suluhu Hassan katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa (UN) ya
kutimiza miaka 72 tangu kuanzishwa kwake.
Makamu
wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyokuwa
na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda na utunzaji wa mazingira kwa
maendeleo endelevu,” alisema umoja wa mataifa umekuwa washirika wakubwa
wa maendeleo katika sekta nyingi hapa nchini hususan maeneo ya vijijini
katika huduma za maji, elimu pamoja na afya.
“Umoja
wa mataifa umekuwa ukifadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini,
katika kutekeleza malengo yake ya millennium ya umoja huo, hivyo naomba
wadau na wafadhili wa maendeleo kutoka umoja huu kuendelea kushirikiana
na serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikishirikiana nao kwa mafanikio
makubwa na kutambua jitihada zao katika kuleta maendeleo,” alieleza Mh.
Samia.
Aidha
alisema kuwa katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 serikali
inatoa wito kwa wadau wote na washirika wa UN kuja kuwekeza na
kushirikiana na Tanzania katika kujenga viwanda, vilevile aliongeza kuwa
uwepo wa amani, usalama pamoja na jitihada za vita dhidi ya ubadhilifu
wa rasilimali, rushwa pamoja na urasimu ni nguzo kubwa ya wawekezaji
kuja kuwekeza hapa nchini.
“Serikali
chini ya Mhe. Rais Magufuli inaendelea kupambana dhidi ya rushwa,
matumizi mabaya ya rasilimali za umma, wizi wa nyara za serikali na
matumizi mabaya ya fedha za umma, serikali pia inatekelezamalengo 17 ya
umoja wa mataifa kwa kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani, kuongeza
makusanyo ya kodi pamoja na kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi,”
alifafanua Makamu wa Rais.
Samia
aliongeza kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na UN katika harakati za
kulinda amani katika mataifa mbalimbali barani Afrika kama vile Jamhuri
ya Kidemkrasia ya Kongo. Vilevile alitoa wito kwa umoja huo kufanya
mabadiliko katika baraza la usalama ili kuimarisha ulinzi, amani na
ushrikiano dhidi ya makundi ya kigaidi yanayozidi kuongezeka kila uchao.
Kwa
upande wake Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkaazi wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez
alisema kuwa, UN itaendelea kushirikina na Tanzania hasa katika kipindi
hiki ambacho taifa linapita katika mabadiliko ya kiuchumi kuelekea
uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
“Wakati
huu ambapo Tanzania inafanya mageuzi makubwa, inapoelekea kuwa nchi ya
hadi ya kipato cha kati, msaada wa UN hauna budi kuendana na mahitaji na
changamoto mpya, kwahiyo hatuna budi kuchukua mwelekeo mpya katika
kazi. Kupitia malengo ya maendeleo endelevu, tutahakikisha kwamba hakuna
mtu hata mmoja anayeachwa nyuma,” alisisitiza Rodriguez.
Mratibu
huyo wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa, kwa kushirkiana na serikali ya
awamu ya tano UN watashawishi wadau na wawekezaji wengi kuja kusaidia
shughuli za maendeleo ikiwemo kuwasaidia wakimbizi pamoja na kufadhili
miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa viwanda, uhifadhi wa mazingira
pamoja na kuwawezesha na kuwalinda wanawake, watoto na vijana dhidi ya
ukatili wa kijinsia.
Sherehe
ya kuadhimisha kuanzishwa kwa Umoja wa Matiafa imekuwa ikifanyika kila
mwaka tarehe 24, Oktoba tangu kuanzishwa kwake mwaka1945 Jijini New
York. Maadhimisho ya hivi karibuni yamekuwa yakitilia mkazo maendeleo
endelevu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya viwanda.
Kwa
sasa UN hapa nchini inatekeleza mpango uliozinduliwa hivi karibuni
kwaajili ya Mkoa wa Kigoma (The Kigoma Joint Programme) ambao
utatekelezwa kati ya 2016-2021 katika Wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na
Kakonko pamoja na mkakati wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa watu na
uhifadhi wa mazingira.
0 comments:
Chapisha Maoni