Makamu
wa Rais, Mama Samia Suluhu amezitaka taasisi za kifedha nchini
kuboresha huduma kwa kufungua matawi maeneo ya vijijini ili kuwafikia
wananchi wengi na hasa wanawake ili wazitumie huduma hizo kwa shughuli
za maendeleo.
Mama
Suluhu aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa Women’s World Banking ambao unalengo la kuangalia namna bora
ya kuwafikia wanawake katika maeneo mbalimbali duniani ili wapate huduma
za kifedha.
Makamu
wa Rais alisema takwimu za matumizi ya huduma za kifedha nchini sio
mbaya lakini ni muhimu jitihada za kuwafikia wanawake wengi zikaongezwa
ili kuwawezesha kupata huduma hizo ambazo wanaweza kuzitumia katika
shughuli za maendeleo.
“Kwetu
Tanzania tumefanya vizuri, kuna watu wengi bado wapo nje ya mfumo rasmi
wa mabenki lakini asilimia 70 ya wananchi wanatumia simu na kama
mnavyojua kuna huduma kama Tigo Pesa, M-Pesa na zimesambaa Tanzania
nzima, kumfikia kila mtu tumepiga hatua kidogo,
“Lakini
kuna mambo mengi inatakiwa tuyafanye kwa mfano mabenki yetu yaendelee
zaidi kwenda kwa wananchi, wafungue matawi zaidi huko kwa wananchi
lakini pia benki yetu ya wanawake ambayo imeundwa kwa dhumuni hilo na
yenyewe ijitahidi kusambaza matawi kwenda mikoani kwenda wilayani
kuwafikia wanawake,” alisema Suluhu.
Naye
Meneja wa Wateja Wadogo na Kati wa NMB, Abdulmajid Nsekela amezungumza
kuhusu mkutano huo na kueleza kuwa mkutano ambao unalengo la kuangalia
namna ya kuwezesha wanawake wanapata huduma za kifedha utakuwa na
mijadala mbalimbali ambayo itawezesha kupatikana suluhisho la namna ya
kuwafikia wanawake hata waliopo vijijini kwa njia ya teknolojia.
“Sisi
kama NMB tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na waandaji wa mkutano huu
na tumekuwa tukianzisha huduma ambazo zinawawezesha wananchi, wakulima
wanawake kupata mikopo kwa riba nafuu … mkutano utaangalia namna bora ya
kuwafikia wanawake hata wa vijijini kwa kutumia teknolojia kwani
yenyewe inauwezo wa kufika popote,” alisema Nsekela.
Katika
mkutano huo wa siku mbili ambao benki ya NMB imekuwa mwandaaji kwa hapa
nchini watu 300 kutoka mataifa 40 wamepata nafasi ya kushiriki mada
mbalimbali ambazo zitatoa njia mbadala ya kuitumia kuwafikia wananchi na
hasa wanawake waliopo vijijini.
0 comments:
Chapisha Maoni