Mbunge
wa Mtama, Nape Nnauye amesema kuzuiwa mikutano ya kisiasa si kuminya
demokrasia kwa kuwa kuna bunge ambalo linaweza kutumika kutolea maoni
yao.
Akihojiwa
na kituo cha Televisheni cha KTN kutoka nchini Kenya katika kipindi
cha siasa za kanda kuhusu demokrasia katika Afrika, Nape amesema
demokrasia inatakiwa kutafsiriwa kulingana na maeneo tuliyopo.
“Afrika hatuwezi kuwa na demokrasia iliyo sawa na Marekani,” amesema.
Nape
alitakiwa kutoa maoni yake kuhusu viongozi wa Chadema kudai kwamba,
Rais John Magufuli anaminya demokrasia hasa kuzuia mikutano ya hadhara.
Akijibu, Nape amesema nchi za Afrika hazitakiwi kutafsiri demokrasia kwa kujilinganisha na nchi zilizoendelea za Magharibi.
“Hapa
kwetu baada ya uchaguzi mkuu tunaruhusiwa kufanya mikutano kwenye
majimbo yetu haturuhusiwi kufanya mikutano nje ya majimbo yetu,”
amesema.
Amesema uchaguzi ukishamalizika siasa zinahamia bungeni ambako wabunge wanaweza kutoa maoni yao.
“Sioni
kama hapa demokrasia inaminywa au kuna udikteta kwa sababu hiyo
inawahusu wabunge wote kutoka chama tawala na vyama vya upinzani,”
amesema.
Nape
ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema
zamani wanasiasa waliruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali
ya nchi.
Nape amesema wakati wa uchaguzi mkuu shughuli nyingi huwa zinasimama kwa sababu ya mikutano ya wanasiasa.
“Kwa hiyo kuna umuhimu wa viongozi wa kisiasa kwenda kutekeleza yale waliyowaahidi wananchi,” amesema.
Nape
amewataka wasomi kutoa tafsiri kwa upana kuhusu dhana ya demokrasia
ili wananchi waweze kuitekeleza kulingana na maeneo waliyopo.
0 comments:
Chapisha Maoni