Waziri
wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amefuta vibali vyote vya
uwindaji kwa kampuni kuanzia Oktoba 22,2017 na kutoa siku 60 kwa
watendaji ili waratibu mchakato upya utakaowezesha vitalu kugawiwa kwa
mnada.
Dk
Kigwangalla pia amemwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, ndani ya muda
mfupi kuwaandikia Hazina ili kuzichukua hoteli 10 kati ya 17
zilizobinafsishwa ambazo zimeshindwa kutimiza masharti.
Ametoa maagizo hayo jana alipohitimisha mazungumzo na wadau wa sekta ya utalii na maliasili aliokutana nao mjini Dodoma.
“Kwa
mamlaka niliyonayo katika sheria, natamka kwamba, nafuta rasmi vibali
vyote vya uwindaji kwa kampuni vilivyotolewa na wizara yangu kwa mwaka
huu. Pia, naagiza watendaji wote wanaosimamia hili wahakikishe wanaandaa
mchakato ndani ya siku 60 ili mnada ufanyike na uwe wa uwazi,” aliagiza
Dk Kigwangalla.
Kuhusu vitalu vyenye migogoro vikiwemo vya Loliondo na Natroni, ameagiza visigawiwe hadi migogoro itakapokwisha.
"Kwenye
hili la hoteli, nataka katibu uwasiliane na mamlaka husika, ikiwemo
Msajili wa Hazina ili ndani ya siku 60 uje na majibu tutangaze kwa
wawekezaji watakaokwenda na masharti," amesema.
0 comments:
Chapisha Maoni