test

Jumamosi, 21 Oktoba 2017

Daktari wa Kanumba Atoa Ushahidi Wake Mahakamani Jinsi Alivyofariki


DAKTARI wa familia ya msanii maarufu wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, Dkt, Paplas Kagaia, ameileza mahakama Kuu ya Tanzania kanda Dar es Salaam Kanumba alifariki toka nyumbani baada ya kumpima na kukuta mapigo yake ya moyo hayakuwepo.

Dk, Paplas amedai hayo jana  Oktoba 20, 2017 huu wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Sam Rumanyika.
 
Amedai kuwa, baada ya mdogo wa marehemu kumfuata hospitali kwake na kumwambia kuwa Kanumba amefariki, alichukua kipimo cha sukari na shindikizo la Damu(pressure) na kwenda moja kwa  moja nyumbani kwake Sinza ambako baada ya kufika nyumbani kwake alimpima sukari na kukuta iko kawaida lakini alipompima pressure haikuwepo kabisa.

Daktari Huyo mwenye elimu ya stashada ya juu (Advanced diploma) aliyejipatia Elimu yake chuo cha uuguzi cha jeshi cha Lugalo amedai kuwa, alikuwa daktari wa familia ya Kanumba kwa zaidi ya miaka mitano na anamiliki Hospitali yake binafsi ya St. Anna iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam alikuwa akimtibu Kanumba magonjwa ya kawaida na hakuwahi kugundua tatizo lake lolote.

==>Mahojiano kati ya Dr Paplas na Wakili wa serikali Batlida Mushi yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili: Ulipata wapi taarifa  ya kuugua kwa Kanumba?
Shahidi: Nikiwa naudumia wagonjwa kama kawaida nilipigiwa simu na Seth akiniomba niende kumuona Kanumba amedondoka, nikamwambia muda ule ulikuwa ni usiku sana aende kumchukua.

Wakili: kwani nini Seth akupigie wewe simu?
Shahidi: Nilikiwa daktari wa familia yao kwa miaka kama mitano hadi sita.

Wakili: Baada ya kukupigia simu, ulifanya nini?
Shahidi: Nilichukua vifaa vya mashine ya sukari na BP, niliingia chumbani kwake nikifuatana na Seth nilipofika nilikuta Kanumba amelala chini chali, nikampima sukari ilikuwa normal nikampima pressure mapigo ya moyo hayakuwepo kabisa.
 
Wakili:Baada ya kujua mapigo ya moyo hayapo ulichukua hatua gani?
Shahidi: Nilimwambia Sethi  umvalishe nguo wafanye utaratibu wa kumpeleka hospitali kubwa ya Muhimbili akafanyiwe Vipimo.

Wakili: Baada ya hapo ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kumvalisha nguo kwa kusaidiana na kijana mmoja wa jirani na mama mwenye nyumba tulimpeleka Muhimbili kitengo cha emergency.
Wakili: Mlipofika Muhimbili kitengo cha Emergency ulifanya nini?
Shahidi: Nilimuomba Dk tuliyemkuta pale ampime Kanumba na alipompima alisema kuwa ameshafariki.

Wakili: Wakati huo anapimwa mlikuwa mahali gani?
Shahidi: Alimpima pale pale nje hata ndani hatukuingia, alitushauri tufuate taratibu za polisi, alituambia twende Kituo cha polisi cha Slender Bridge tukachukue PF3.

Wakili: Mlipokuwa Polisi nini kiliendelea?
Shahidi: Tulipewa askari ili watusaidie kupeleka maiti Mochuari kisha tukaambiwa twende Kituo Osterbay Polisi tukatoe Maelezo.

Wakili: Unamfahamu Lulu?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Unamfahamuje?
Shahidi: Nimemfahamu kwa kupitia Kanumba.

Wakili: Unamfahamu kama nani?
Shahidi: Alikuwa mpenzi wake Marehemu Kanumba.
Wakili: Je Aprili 7 mwaka 2012 baada ya wewe kwenda Polisi Osterbay ulimuona?
Shahidi: Hapana sikumuona.

Wakili: ulimuonea wapi?
Shahidi: Nilimuona usiku kwenye saa 11 alikuwa Sinza sehemu moja inaitwa Bamaga, baada ya yeye kunipigia simu.

==>Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake kwa upande wa mashtaka wakili wa utetezi, Peter Kibatala naye alipata nafasi ya kumuhoji shahidi huyo ambapo mahojiano yao yalikuwa hivi;
 
Wakili Kibatara: Kwa nini ulipofika eneo la tukio ulimpima Sukari?
Shahidi: mtu akianguka ghafla Mara nyingi sukari inaweza kuwa imeshuka
Wakili Kibatala; kabla ya Octoba 7 uliwahi kumfanyia uchunguzi marehemu kuhusu sukari.
Shahidi: Hapana
 
Wakili: Uliwahi kumfanyia vipimo kama anauvimbe kichwani
Shahidi: hapana.
Wakili: je ulimkuta na jeraha lolote?
Shahidi; hapana.
Wakili Kibatara: Ni sahihi kuwa mshtakiwa alikuwa anakupigia simu Mara kwa Mara?
Shahidi: Ni sahihi kweli alikuwa akinipigia hata kabla hajaenda hospitali.

Wakili Kibatara:Ni sahihi kwamba mshtakiwa alikuwa anakupigia simu Mara kwa Mara akifikiria kuwa marehemu alikuwa amezimia tu?
Shahidi; Ndiyo ila alikuwa na hofu kama marehemu amekufa.

Wakili Kibatara: Ni sahihi kuwa mshtakiwa alikuwa anaogopa kuonana na wewe kwa sababu alidhani uko na marehemu na ulikuwa ni mtego tu wa kumkamata ili andeleze tabia yake ya wivu uliopindukia?
Shahidi: hapana.
 
Wakili Kibatala: umesema, mlikutana na mshtakiwa Bamaga, kwa nini mshtakiwa alikubali kuonana na wewe Bamaga?, Ni ushawishi gani ulimwambia hadi akakubali kuja?
 
Shahidi: alikubali tukutane Bamaga alikuwa hajui kwamba Kanumba ameshafariki, yeye ndio alinipigia simu akasema si umesema Kanumba hajafa nikamwambia ndio akasema tukutane Sinza nikasema tukutane Bamaga.

Naye shahidi wa tatu, mrakibu msaidizi wa Polisi PF 16519 ASP Ester Zefania akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na wakili wa Serikali,  Ayoub Abood amedai, Oktoba 7, 2012 akiwa kituoni Osterbay alipewa maelekezo na Mkuu wa upelelezi Wa mkoa Wa Kinondoni Camilius wambura kwenda Sinza kwa Kanumba kufuatilia taarifa alizopata za kifo cha Kanumba.

Amedai aliondoka na askari watatu pamoja na msanii Ray ambaye aliwaongoza hadi  Sinza kwa marehemu ambako alikuta watu wengi wengine wakilia kuashiria hali ya msiba 
==>Mahojiani yake na Wakili Abood yalikuwa hivi;
Wakili: Baada ya kufika hapo nyumbani ulifanya nini?
 
Shahidi : Nilijitambulisha wa watu waliokuwepo pale kuwa Mimi ni askari kutoka kituo cha polisi cha Osterbay, nikaitiwa mdogo wake Kanumba Seth, ambapo nilipomuuliza nini kilitokea alinielezea kwa kifupi.
 
Baada ya hapo mimi pamoja na askari 2 pamoja na Ray tuliiingia chumbani kwa marehemu kwa ajali ya uchunguzi.

Wakili : Baada ya kuingia humo chumbani ulikuta hali gani? na  mliweza kuona kitu gani katika chumba hicho?
 
Shahidi:Kitanda kilikuwa kimevurugwa, pembeni yake kulikuwa na stuli juu yake ilikuwa na chupa ya soda aina ya Sprite, glass iliyokuwa na kinywaji nusu na chupa ya whisky ya Jackie Daniel, pia pembeni chini ya tendegu za kitanda kulikuwa na panga na pembeni yake kulionekana michirizi ya mburuzo wenye rangi kama nyeusi isiyokolea.

Wakili: Baada ya hapo nini kilitokea?
Shahidi: Nilimpigia simu kamanda Wambura na kumpatia taarifa ambaye aliniambia angetuma timu ya wapelelezi wa matukio kutoka mkoani na eneo la tukio libaki vilevile.

Wakili: Baada ya kufika wakuu wa upelelezi ulifanya nini?
Shahidi: Nilindoka nikarudi kituoni.

Wakili: Baada ya kufika kituoni ulimkuta nani?
Shahidi; Nilimkuta kamanda Wambura ambaye alinipa (task) jukumu la kumtafuta Lulu apelekwe kituoni hapo kwani kwa taarifa alizokuwa nazo atakuwa anafahamu nini kilimpata Kanumba.

Wakili: Alikupa Huyo Daktari kwa ajili gani?
Shahidi; Alinipa Daktari Paplas ili tusaidiane nae kumpata Lulu kwani ndio alikuwa akiongea naye  Mara nyingi ambapo alimpigia simu na kukubaliana kukutana nae bamaga ndipo waliweza kumkamata.
 
==>Wakili Kibatala nae alimhoji mrakibu msaidizi wa Polisi PF 16519 ASP Ester Zefania mahojiano yao yalikuwa hivi;

Wakili Kibatala: Mlipomkamata Lulu mlimpeleka hospitali?
Shahidi; Ndio 
Wakili Kibatala: Mlimpeleka Lulu hospitali kutibiwa nini?
Shahidi: sifahamu, sikuingia kwenye chumba cha daktari.
Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba sababu ya kupelekwa Lulu kwa daktari kuwa alipigwa na ubapa wa panga mapajani na alikuwa na maumivu
Shahidi; Sifahamu.

Kesi hiyo itaendelea Oktoba 23, 2017( Jumatatu) na shahidi wa nne atatoa ushahidi wake.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni